Trump kuongoza utiaji saini wa makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda

Muda wa kusoma: Dakika 4

Viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Rwanda wako tayari kusaini makubaliano ya amani yanayolenga kumaliza mzozo wa muda mrefu katika eneo hilo, katika mkutano unaoandaliwa na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington.

Kuelekea mkutano huo, kumekuwa na kuongezeka kwa mapigano katika eneo la mashariki mwa DRC lenye utajiri wa rasilimali, kati ya majeshi ya serikali na waasi wanaodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.

Jeshi la DRC liliwashutumu wapinzani wao kwa kujaribu "kuhujumu" mchakato wa amani, lakini waasi wa M23 walisema jeshi ndilo lililoanzisha mashambulizi kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.

Mwanzoni mwa mwaka, waasi wa M23 waliteka maeneo makubwa ya mashariki mwa DRC katika mashambulizi yaliyosababisha maelfu ya watu kuuawa na wengine wengi kulazimika kuyakimbia makazi yao.

Unaweza kusoma

Rais wa DRC Félix Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame wamekuwa wakirushiana maneno mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, kila mmoja akimshutumu mwenzake kwa kuanzisha mzozo huo.

Trump aliwafanya mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo mbili kusaini makubaliano ya amani mwezi Juni, akiyataja kama "ushindi wa kifahari".

Tshisekedi na Kagame sasa watayathibitisha, huku viongozi wengine kadhaa wa Afrika na Kiarabu, wakiwemo wa Burundi na Qatar, wakitarajiwa kuhudhuria hafla ya utiaji saini.

M23 haitakuwepo, linafanya mazungumzo na serikali ya DRC katika mchakato sambamba wa amani unaoongozwa na Qatar.

Utawala wa Trump umeongoza mazungumzo kati ya DRC na Rwanda, ukitumaini kwamba kutatua tofauti kati ya majirani hao wawili kutafungua njia kwa Marekani kuongeza uwekezaji katika eneo hilo lenye utajiri wa rasilimali.

Rwanda inakanusha kuunga mkono M23, licha ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kusema kuwa jeshi la Rwanda liko katika "udhibiti wa moja kwa moja wa oparesheni za M23".

M23 iliteka miji muhimu katika mashariki mwa DRC mapema mwaka huu, ikiwemo Goma na Bukavu.

Katika taarifa, msemaji wa jeshi la DRC Jenerali Sylvain Ekenge alisema kuwa waasi hao wameanzisha mashambulizi mapya siku ya Jumanne kwenye vijiji vya mkoa wa Kivu Kusini.

Vijiji hivyo viko takribani kilomita 75 kutoka jiji la Uvira, lililo mpakani mwa Burundi, na ambalo limekuwa makao makuu ya serikali ya mkoa wa Kivu Kusini tangu waasi walipoteka Bukavu.

Kwa upande wake, M23 ilisema jeshi la DRC ndilo lililoanzisha mashambulizi ya anga na nchi kavu dhidi ya ngome zake, na kwamba hilo lilifanywa kwa ushirikiano na wanajeshi wa Burundi.

Burundi haijatoa maoni kuhusu tuhuma hizo. Ina maelfu ya wanajeshi katika mashariki mwa DRC kusaidia jeshi la nchi hiyo linalokabiliwa na wakati mgumu.

Licha ya sherehe na uwepo wa viongozi hao wawili mjini Washington, baadhi ya wachambuzi wana wasiwasi kuhusu iwapo makubaliano hayo yataweza kuleta amani ya kudumu.

Mtafiti wa DRC anayefanya kazi katika taasisi ya South Africa ya Institute for Security Studies, Bram Verelst, aliiambia BBC kwamba kwa sasa "hakuna kusitishwa kwa mapigano, na uasi wa M23 unaendelea kuenea na kuimarisha udhibiti wake".

"Shughuli ya utiaji saini haiwezi kubadilisha hali hii, ingawa kuna matumaini madogo kwamba inaweza kuongeza uwajibikaji kwa viongozi wa Congo na Rwanda kutimiza ahadi zao," alisema.

Rwanda inasema imechukua "hatua za kujilinda" katika mashariki mwa DRC kutokana na tishio lililotolewa na kundi la waasi la FDLR, ambalo linajumuisha wapiganaji waliotekeleza mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994.

Kagame anasisitiza upunguzaji wa silaha wa kundi hilo, huku DRC ikidai kuondolewa kwa wanajeshi wa Rwanda kama sharti la amani.

Makubaliano yatakayosainiwa yanabainisha kwamba yote haya yanapaswa kutekelezwa.

Hata hivyo, makubaliano kadhaa ya amani yaliyofanywa tangu miaka ya 1990 yameshindwa baada ya Rwanda kushutumu serikali za awali za Congo kwa kushindwa kupunguza silaha za FDLR, na hili bado ni kikwazo kikuu katika juhudi za sasa za kumaliza mzozo.

Serikali ya DRC pia imekuwa ikidai kwamba M23 irudishe ardhi iliyotekwa, jambo ambalo hadi sasa wameshindwa kufanya katika mazungumzo yanayoendeshwa na Qatar.

Qatar na Marekani zinaendesha pamoja juhudi zao za usuluhishi. Qatar ina uhusiano mzuri na Rwanda, huku Marekani ikionekana kuwa karibu zaidi na DRC.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema mwaka 2023 kwamba DRC ina makadirio ya akiba ya madini yenye thamani ya dola trilioni 25 ($25trn / £21.2trn).

Hii inajumuisha cobalt, shaba, lithiamu, manganese na tantalum, muhimu katika vifaa vya kielektroniki kama kompyuta, magari ya umeme, simu za mkononi, mitambo ya upepo na vifaa vya kijeshi.

"Tunapata, kwa upande wa Marekani, haki nyingi za madini kutoka Congo kama sehemu ya makubaliano haya," alisema Trump, kabla ya makubaliano kusainiwa mwezi Juni.