Hali ya maisha katika nchi yenye furaha zaidi duniani

Muda wa kusoma: Dakika 5

Finland imeshika tena nafasi ya kwanza duniani kama nchi yenye furaha zaidi, kwa mwaka wa nane mfululizo.

Hata hivyo, kwa Wafinlandi wengi, uzuri wa nchi yao haupo tu katika tuzo au takwimu, bali katika maadili ya msingi ya maisha usawa, mshikamano na kuridhika na hali ya kila siku.

Wakazi wa Finland hupokea habari za kutangazwa kwao kuwa na furaha zaidi duniani, kupitia ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Machi 2025, kwa mtazamo wa utulivu wa pamoja wakati mwingine hata kwa hisia ya kuchoshwa.

Hata hivyo, sekta ya utalii imefurahia hali hiyo, kwani watalii wanazidi kuona uhusiano wa kweli kati ya Finland na furaha, na wengi hutamani kufika nchini humo ili kuonja maisha ya Finlandi.

Hata hivyo, mgeni asitarajie mapokezi ya vicheko vya shangwe au gumzo la furaha anapowasili katika Uwanja wa Ndege wa Helsinki, au anaposhuka kutoka meli ya kitalii kwenye bandari za Bahari ya Baltiki.

Watu wa Finland ni wakweli, wapole na wa kawaida.

Kwao, furaha haimaanishi mbwembwe au shamrashamra.

Ingawa wanathamini utambuzi wa kimataifa, wengi hawaoni neno "furaha" likiwakilisha kikamilifu hali yao ya maisha.

Wanapendelea kutumia maneno kama "kuridhika," "ustawi," au "mafanikio ya maisha."

Rais wa Finland, Alexander Stubb, aliandika hivi karibuni kwenye ukurasa wake wa Facebook:

"Hakuna mwanadamu anayeweza kuwa mwenye furaha kila wakati. Wakati mwingine mazingira na hali hutufanya tusihisi furaha. Lakini hatua ya kwanza kuelekea furaha ni kuwa na haki za msingi kama usalama, uhuru na usawa."

Pia unaweza kusoma:

Ingawa dhana ya furaha nchini Finland inaweza kuwa na maana maalum ya kitamaduni, inafungamana na maisha ya kila siku ya watu.

Raia wa Finland wana maono kulingana na usawa, kushikamana, na kuridhika.

Maisha ya usawa na uhusiano wa asili

Helsinki, jiji la mji mkuu na sehemu ambayo wengi huanzia au kumalizia safari zao, linaakisi kwa undani maadili ya Finland ya kuridhika.

Jiji hili la pwani limesambaa kwenye rasi ya asili na maeneo yaliyopatikana kwa urekebishaji wa ardhi kutoka baharini.

Ni rahisi kwa mtu kukodi baiskeli kutoka kwenye vituo vya umma na kupita kwenye njia maalumu kando ya pwani, au kuingia msituni kupitia bustani kuu ya jiji eneo la misitu linaloanzia katikati ya jiji hadi pembezoni mwa kaskazini.

Uzoefu huu wa kuunganishwa na mazingira kwa uhuru huchochea hisia chanya, na unaendana na vigezo vya Umoja wa Mataifa vya furaha, vinavyohusisha maisha marefu, uhuru wa kuchagua, na afya ya akili.

Uvumilivu na msimamo katika nyakati ngumu

Pamoja na hayo, Finland haijanusurika na changamoto.

Shinikizo la kiuchumi, mabadiliko ya kisiasa ya kimataifa, na majira marefu ya baridi kali huathiri afya ya akili ya baadhi ya raia wake.

Katika muktadha wa Finland, furaha pia inahusishwa na dhana ya sisu neno la Finland lisilo na tafsiri sahihi kwa Kiswahili, lakini lenye maana ya ujasiri, uvumilivu, ustahimilivu na msimamo katika nyakati ngumu.

Katja Pantzar, mwandishi wa Finland na Mkanada, ambaye ameandika kwa mapana kuhusu sisu, anaeleza kuwa ni mtazamo wa maisha unaowawezesha watu na jamii kushikamana wanapokabiliwa na changamoto, badala ya kukata tamaa, kulaumiana au kujiengua.

Anaongeza kuwa nchi zote nne zinazoongoza kwenye orodha ya furaha duniani ambazo zote ni za Skandinavia zina mifumo imara ya hifadhi ya kijamii inayounga mkono ustawi wa watu wake.

Anasema: "Furaha na ustawi ni sehemu ya utamaduni wetu. Hapa Finland, kuna fursa nyingi za furaha ya kila siku zinazopatikana kwa kila mmoja: mazingira ya asili, kwani kwa wastani kila mtu yuko mita 200 tu kutoka kwenye msitu, fukwe, maji safi ya bahari au ziwa; sauna za umma, maktaba za bure, usafiri wa umma ulio salama na afya kwa wote.

Pantzar pia anazungumzia mazoea ya tiba tofauti yaani kutumia sauna ya moto kisha kuogelea kwenye maji baridi kama njia ya kawaida ya kuburudisha mwili na akili.

"Ni rahisi sana kufanya hivyo hapa Helsinki kwa sababu bahari ipo karibu," anasema.

"Mtu hahitaji kusafiri mbali au kutumia pesa nyingi, hivyo kila mtu anaweza kufanya hivyo kabla ya kazi, baada ya kazi, au hata wakati wa mapumziko."

Ingawa baadhi ya Wafinland wanahoji usahihi wa kuitwa nchi yenye furaha zaidi duniani, wengi wao wanakubali kwa namna yao ya utulivu.

"Sioni kwa urahisi kwamba Finland ndiyo yenye furaha zaidi duniani," anasema Juha Roha, mstaafu.

"Katika nchi maskini kama Thailand au Nepal, licha ya changamoto zao, watu huonekana kuwa na utulivu wa ndani. Hapa Finland, watu huenda hawacheki sana hadharani, lakini mioyoni mwao wanaridhika na maisha yao."

Mada zinazohusiana:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid