Kwanini watanzania hawana furaha? Fahamu vigezo vya jinsi wanavyopima furaha ya nchi

Muda wa kusoma: Dakika 7

Na Yusuph Mazimu

Ripoti ya furaha duniani inayosimamiwa na Umoja wa Mataifa (World Happiness Report 2025) imetangazwa, na kwa mara nyingine tena, Tanzania iko chini katika orodha ya nchi zenye furaha duniani.

Wakati Finland ikiendelea kushika nafasi ya kwanza kwa mwaka wa nane mfululizo, Tanzania imeshika nafasi ya 136 kati ya nchi 147, ikishuka kwa nafasi tano kutoka nafasi ya 131 mwaka uliopita. Nafasi ya sasa inaiweka nchi hiyo kuwa miongoni mwa nchi 11 za mwisho duniani kwa viwango vya furaha.

Cha kushangaza ni kwamba Tanzania, licha ya kuwa na amani na utajiri mkubwa wa maliasili, imepitwa hata na mataifa yenye migogoro kama Somalia. Nchi jirani kama Kenya na Uganda, ambazo mara kwa mara hukumbwa na changamoto za kisiasa na kiusalama, zimepata nafasi za juu zaidi. Hapa chini ni orodha ya nchi zenye furaha kwa mujibu wa World Happiness Report 2025, kuonyesha kumi bora na zilizoshika mkia. Kwa Afrika Mauritius inaongoza, wakati Lebanon, Sierra Leone na Afghanistan ni nchi tatu za mwisho duniani.

1. Finland

2. Denmark

3. Iceland

4. Sweden

5. Netherlands

6. Costa Rica

7. Norway

8. Israel

9. Luxemborg

10.Mexico

78. Mauritius

79. Libya

84. Algeria

115. Kenya

116. Uganda

122. Somalia

136. Tanzania

145. Lebanon

146. Sierra Leone

147. Afghanistan

Lakini kwanini Tanzania imebaki nyuma? Je, furaha inapimwaje, na ni vigezo gani vinatumika kuamua ni nchi zipi zinafuraha zaidi?

Nini maana ya furaha na vigezo vinavyotumika kupima furaha ya taifa

Muhemko chanya unaotokana na kuridhishwa na jambo fulani, kucheka na kutabasamu ni tafsiri ya furaha inayojulikana sana. Yaani jinsi gani watu wanavyohisi kila siku, kupitia viashiria vya kihisia kama vile tabasamu, furaha, huzuni, au wasiwasi. Lakini kwa mujibu wa World Happiness Report (WHR), furaha si tu hali ya kihisia kama vile kutabasamu au kucheka, bali pia ni tathmini ya maisha kwa ujumla.

Ripoti ya WHR hutumia vigezo sita vikuu katika kupima furaha ya nchi. Mshikamano wa kijamii ni moja ya vipengele muhimu, ambapo mataifa yenye furaha zaidi huwa na jamii zinazosaidiana na kushirikiana kwa karibu. Tanzania inajulikana kwa mshikamano wake wa kijamii, lakini changamoto za kiuchumi na kijamii zimechangia watu wengi kuhisi kama wanapambana pekee yao na maisha. Lugete Musa Lugete, mchambuzi wa siasa za Afrika, analiona hili mpaka kwenye mahusiano ya kawaida.

'Upungufu wa mguso chanya yaani mtu kukosa kuwa na hisia chanya na mwenzake na kupelekea kumuona kama mnyama mfano wanandoa kukosa mguso chanya hivyo kupelekea kuishi kwenye ndoa bila kuwa na mapenzi', anasema Lugete.

Pato la taifa kwa mtu mmoja mmoja (GDP per capita) ni kipimo kingine muhimu kinachoonyesha uwezo wa kiuchumi wa watu. Ingawa uchumi wa Tanzania unakua, ukuaji huu haujawa shirikishi vya kutosha ili kuwafaidisha wananchi wa kawaida. Kipato cha mtu mmoja mmoja bado ni cha chini, na hali ya mfumuko wa bei inafanya maisha kuwa magumu zaidi kwa watu wengi.

Matarajio ya kuishi kwa afya ni kipengele kingine kinachoathiri furaha ya wananchi. Upatikanaji wa huduma bora za afya una mchango mkubwa katika maisha ya watu, lakini nchini Tanzania, huduma za afya bado zina changamoto kubwa, hasa vijijini, ukilinganisha na mataifa mengi hasa yaliyo katika 20 bora. Watu wengi hawapati matibabu bora kwa wakati, jambo ambalo linaathiri hali yao ya maisha kwa ujumla.

Uhuru wa kufanya maamuzi ya maisha ni kiashiria kingine kinachopimwa na WHR. Mataifa yenye furaha zaidi ni yale ambayo watu wake wana uhuru wa kuchagua namna wanavyotaka kuishi. Hali ya ajira Tanzania bado ni changamoto kubwa, huku vijana wengi wakikosa fursa za kazi na mazingira ya ujasiriamali yakiwa magumu. Hili linapunguza uwezo wa watu kupanga maisha yao kwa uhuru.

"Kijana akiwa Chuo Kikuu anakuwa kwenye msongo wa mawazo na sonono kuhusu hatma ya maisha yake mara baada ya kuhitimu Chuo. Ndio maana asilimia 77 ya Vijana vyuo Vikuu wamejikita kwenye kamari, pombe, mapenzi na mambo mengine ambayo yanaongeza sonono", anasema Mchambuzi Lugete.

Ukarimu pia ni moja ya vipengele muhimu katika kupima furaha ya taifa. Katika nchi zenye furaha, watu huwa tayari kusaidiana na kuna utamaduni wa ukarimu na kutoa msaada kwa wenye uhitaji. Ingawa Tanzania ina utamaduni wa ukarimu, hali ngumu ya maisha inawafanya watu wengi kuwa waangalifu zaidi na kile walicho nacho, jambo ambalo linaweza kupunguza mshikamano wa kijamii.

Huwezi kuwa na furaha kama una 'tatito la madeni na mikopo yenye riba kubwa maarufu kama kausha damu na kuishi nje ya bajeti', anaongeza Mugete katika uchambuzi wake.

Rushwa ni kigezo kingine kinachoathiri furaha ya wananchi. Katika mataifa yenye furaha, wananchi huwa na imani na serikali na taasisi zake, kwani kuna uwazi na uadilifu. Tanzania imepiga hatua katika mapambano dhidi ya rushwa, lakini bado kuna malalamiko kuhusu ufisadi katika sekta mbalimbali kama afya, elimu, na ajira.

Vigezo sawa, Je wanapimaje furaha ya nchi?

Bado kuna mjadala mkubwa sana kuhusu upimaji wa furaha ya watu kwenye taifa fulani ili kufikia hitimisho kwamba ni taifa lenye wananchi wenye furaha zaidi kuliko taifa ama mataifa mengine.

Ili kupima furaha ya nchi, WHR hutegemea data kutoka Gallup World Poll, ambayo imekuwa ikikusanya taarifa hizi tangu mwaka 2005. Zaidi ya watu 100,000 kutoka nchi zaidi ya 140 huhojiwa kila mwaka.

Katika kila nchi, wastani wa watu 1,000 hufanyiwa mahojiano kwa njia ya simu au ana kwa ana. Hapa ndipo wakosoaji wanapoegemea, wakihoji nchi kama Tanzania yenye watu milioni 65, kwa kuwahoji watu 1,000 utaweza kupata uhalisia kamili? Kitafiti, kigezo cha idadi ya watu wanaohusika kwenye mahojiano (sample size) ni muhimu. Inaweza kutetewa idadi hiyo ya watu 1,000 kisayansi. Lakini wanapatikanaje hao watu 1,000? Bado haijawa wazi sana.

Ili kuhakikisha matokeo yana usahihi wa hali ya juu, WHR yenyewe hutumia data ya miaka mitatu iliyopita, kwa mfano, matokeo ya mwaka 2025 yaliyochapishwa sasa yanatokana na takwimu zilizokusanywa kati ya 2022 na 2024.

Kwa ripoti ya sasa, ili kupima furaha ya taifa, WHR inaangalia vipengele mbalimbali vya kisayansi, ikiwemo hali ya ustawi wa mtu binafsi, tathmini yake kuhusu maisha yake kwa ujumla, na kiwango cha kuridhika na maisha.

Ustawi wa mtu (Wellbeing) ni kipimo cha ndani kinachoonyesha jinsi mtu anavyohisi kuhusu maisha yake. Hali hii inaweza kuathiriwa na vipengele kama afya, mahusiano, na hali ya kiuchumi.

Tathmini ya mtu binafsi kuhusu maisha yake hujulikana kama Subjective wellbeing, ambapo watu huombwa kuweka kiwango cha furaha yao kwa namba kati ya 0 na 10.

Mbinu maarufu inayotumiwa kupima furaha duniani inaitwa Cantril Ladder, ambapo watu huulizwa waweke maisha yao kwenye mizani kati ya sifuri (maisha mabaya kabisa) hadi kumi (maisha bora kabisa).

Swali hili huulizwa kila mshiriki na linawapa watu uwezo wa kujitathmini wenyewe bila kupangiwa vigezo vya furaha kutoka nje. Pia, halihusishi moja kwa moja dhana kama "furaha," "ustawi," au "kuridhika na maisha," hivyo hufanya tafsiri na uelewa wake kuwa rahisi kwa lugha na tamaduni mbalimbali.

Kwa nini nchi ndogo kama Finland zinafuraha zaidi? Na Je, Tanzania inaweza kupanda?

Orodha ya kila mwaka ya viwango vya furaha inaendelea kuongozwa na nchi za Nordic, ambazo hujumisha nchi kama Denmark, Finland, Iceland, Norway, na Sweden, huku Finland ikiendelea kushikilia nafasi ya kwanza miongoni mwao toka mwaka 2018. Denmark ni ya pili, Iceland (3), Sweden (4), na Norway ya 7.

Viwango vya furaha vya nchi kupitia maeneo ma matatu ya ukarimu ambayo ni utoaji wa misaada, kujitolea, na kusaidia wageni vilifuatiliwa na kuonyesha kutofautiana sana na vikileta tofauti kubwa ya matokeo kutokana na tofauti za kitamaduni na mifumo ya taasisi.

Nchi za ukanda huu wa Nordic, kama Finland zinafuraha zaidi kwa sababu zina mfumo mzuri wa usaidizi wa kijamii, ambapo wananchi wake wana uhakika wa huduma za afya, elimu, na fursa za kiuchumi.

Tanzania inashika nafasi ya chini kwa sababu mazingira yake ya sasa hayawezeshi vigezo vya furaha kupanda. 'Utaweza kumsaidia mwenzako, wakati wewe mwenyewe unahitaji kujisaidia?', Alihoji Juma Shomvi wa Tanzania na kuongeza 'Kutulinganisha sisi na nchi kama Denmark, Finland, kwa vigezo hivi ni kutuonea tu, maisha yetu hayalingani na utamaduni wetu haulingani, tukisimama kiuchumi sawa, kwa sasa bado'.

Mfano mzuri kwa nchi inayoshika nafasi ya kwanza, huduma za afya zinagharamiwa na serikali (ikifikia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa - GDP), na ubora wa hewa unakidhi viwango madhubuti vya Shirika la Afya Duniani (WHO). Katika taifa lenye misitu mingi zaidi barani Ulaya, asilimia 74 ya ardhi imefunikwa na miti, na asilimia 90 ya wakazi wa mijini wanaishi ndani ya umbali wa mita 300 kutoka eneo la kijani kibichi. Mazingira ya asili, kijani, na tulivu huwafanya watu kuwa na furaha kama chombo cha habari cha Telegraph kilivyoripoti.

Kinachoonekana kwa Tanzania na nchi zingine zilizo chini ni mfumo wa maisha uliojengwa na tabia na tamaduni za enzi na enzi.

"Mfumo mzima wa maisha yetu ambapo hatupati tunachotaka bali kilichopo kulingana na changamoto za kiuchumi na kijamii", anasema Mguto.

Tanzania inaweza kupanda kwenye orodha ya furaha duniani ikiwa itachukua hatua madhubuti za kuhakikisha kunakuwa na uchumi shirikishi zaidi, inabendelea kuboresha huduma za afya, kufikia kutolewa bure, na kujenga mazingira tulivu kwa watu wake. Ingawa si rahisi, kufanyika mara moja, Ikiwa hatua hii zitachukuliwa kwa dhati, basi Tanzania inaweza kuboresha hali ya maisha ya watu wake na kupanda juu kwenye orodha ya furaha duniani. Hii ndio njia rahisi zaidi kupitia vigezo vilivyopo.