Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, China inauza makombora na ndege za kivita kwa Iran?
Ubalozi wa China nchini Israel tarehe 8 Julai ulikanusha ripoti za vyombo vya habari vya kigeni kwamba Iran hivi karibuni ilipokea mfumo wa makombora ya masafa marefu ya ulinzi wa anga ya HQ-9B kutoka China.
Gazeti la habari na tovuti ya lugha ya Kiingereza ya London, Middle East Eye, liliripoti Julai 7, likimnukuu afisa wa Kiarabu ambaye jina lake halikujulikana na "aliyefahamishwa" kwamba mifumo ya makombora ya kutoka ardhini hadi angani iliyotengenezwa na China ilikabidhiwa kwa Iran muda mfupi baada ya kutangazwa kwa usitishaji vita wa Iran na Israel mnamo Juni 24, na kwamba Marekani na washirika wake wa Kiarabu "wanafahamu" juhudi zake za ulinzi wa anga za Tehran.
Katika kujibu ripoti hiyo, Ubalozi wa China mjini Tel Aviv uliambia gazeti la Israel Hayom kwamba maudhui ya ripoti hiyo "si sahihi."
Ubalozi huo umesisitiza kuwa, "China inapinga vikali kuenea kwa silaha za maangamizi na mifumo ya utoaji wao na inazidisha mara kwa mara uwezo wake wa kufanya kazi katika uwanja wa kukabiliana na uenezaji huo.
Israel Hume imeunukuu ubalozi wa China ukisema: "China haiuzi silaha kamwe kwa nchi zinazohusika na vita na inadhibiti vikali usafirishaji wa bidhaa zinazotumika mara mbili.
Kama mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, China inachukua mtazamo wa tahadhari na uwajibikaji katika usafirishaji wa bidhaa za kijeshi."
Hata hivyo, si tovuti rasmi ya ubalozi wa China wala vyombo vya habari vya serikali vilivyochapisha taarifa hii.
Wakati huo huo, Songlin Kan Shijie, mwanablogu wa Kichina asiye na uhusiano na serikali, aliandika Julai 10 kwenye jukwaa la kublogu la Baidu la Baijiahao kwamba ripoti ya shirika la habari la Iran la Mehr kuhusu utoaji wa China wa mfumo wa ulinzi wa anga "inaonekana zaidi kama vita vya habari vilivyopangwa kufanywa na Tehran."
Blogu hiyo, ikitaja matatizo yanayohusiana na uhamisho na mafunzo ya wanajeshi wa kuendesha mfumo huo wa ulinzi wa HQ-9 katika muda mfupi, iliibua uwezekano kwamba Iran inaweza kutumia jina la China ili kuzuia Israel na Marekani, ili kuonyesha kwamba inaungwa mkono na nguvu kubwa.
Uwezekano wa kuuza ndege za kivita za G-10 kwa Iran?
Vyombo vya habari vilitilia maanani zaidi ripoti kwamba Iran imeanza tena mazungumzo ya kununua ndege za kivita za J-10C zilizotengenezwa China, ambazo zilivutia watu wengi duniani kote baada ya utendaji wao katika mzozo wa hivi majuzi wa Pakistan na India mwezi Mei.
Katika ripoti ya Juni 27, gazeti la Hong Kong Tsingtao Daily liliandika, likirejelea historia ya suala hili kwamba China na Iran zimeshindwa kuafikia makubaliano juu ya makubaliano haya mara kadhaa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Chapisho hilo, likinukuu gazeti la Urusi la Kommersant, liliandika kwamba Tehran ilikaribia kununua ndege 150 za J-10C mnamo 2015, lakini ilishindwa kwa sababu China haikukubali malipo ya mafuta au gesi asilia, na Iran ilikuwa inakabiliwa na uhaba wa fedha za kigeni na vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa.
Mazungumzo yalianza tena 2020 baada ya vikwazo kuondolewa, lakini kwa sababu hizo hizo, hakuna makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa.
Chombo cha habari cha Taiwan NewTalk pia kiliripoti Julai 5 kwamba Waziri wa Ulinzi wa Iran Aziz Nasirzadeh alitoa wito wa kununuliwa kwa ndege za kivita za J-10C pembezoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai mjini Qingdao mnamo Juni 26.
Chombo hicho pia kilitaja vyanzo vya habari nchini Iran vikisema kuwa Iran inahitaji takriban ndege 400 za kivita.
Tarehe 8 Julai, Wizara ya Ulinzi ya China ilitoa jibu la jumla kwa maswali kuhusu "baadhi ya nchi" katika mazungumzo na China kununua ndege za kivita aina ya J-10, ikisema kwamba Beijing "inachukua mtazamo wa tahadhari na uwajibikaji katika uuzaji wa bidhaa za kijeshi nje ya nchi na iko tayari kushirikisha mafanikio yake katika maendeleo ya vifaa vya China na nchi marafiki na kuchukua jukumu la kujenga katika amani na utulivu wa kikanda na kimataifa."
Mbali na ripoti ambazo hazijathibitishwa kuhusu nia ya Iran kuagiza ndege za kivita za J-10 kutoka nje, Indonesia pia inasemekana kuwa katika mazungumzo ya kununua ndege hizo.
Hatari za kijiografia
Mnamo tarehe 10 Julai, Dao Lanijiang, mwanablogu wa kijeshi na mwanajeshi wa zamani wa jeshi la China, alionyesha shaka juu ya manufaa ya kununua ndege za kivita za J-10C katika hali ya sasa katika makala katika chombo cha habari cha serikali cha Guangcha.
Alidai kwamba Tehran inachohitaji sasa sio ndege za kivita za hali ya juu, lakini rada halisi za kuzuia ndege na mifumo ya kuaminika ya ulinzi wa anga ili kukabiliana na ndege za kivita za F-35 za Israel.
Pia alionya kwamba Israel inaweza kuanzisha 'mashambulizi mapema' mara tu baada ya uwasilishaji wa ndege za kivita za hali ya juu kwa Iran kuanza, kwa sababu, kulingana na yeye, Israeli haitavumilia hata UAE au Saudi Arabia kuwa na toleo dhaifu la F-35.
Gazeti la Taiwan la China Times, ambalo linaunga mkono misimamo ya Beijing, liliandika katika toleo lake la tarehe 27 Juni, likimnukuu Brigedia Jenerali mstaafu Li Chengchi, kwamba huenda China haina nia ya kuiuzia Iran ndege za kivita, kwani hatua hiyo inaweza kuhatarisha uhusiano wa kiuchumi wa Beijing na Israel.
Mwanablogu wa Kichina Songlin Kan Shijie pia alidokeza kwamba kama Uchina ingeuza silaha kama HQ-9 kwa Iran, itakabiliwa na hatari za kimkakati.
Kulingana naye, hatua hii itazidisha mzozo wa Iran na Israel na Marekani; itasababisha wimbi jipya la vikwazo, kuvuruga usawa wa kijeshi katika Mashariki ya Kati, na kuibua hisia kutoka kwa nchi kama vile Saudia.
Vile vile ameongeza kuwa, udhaifu katika mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran unaweza pia kuharibu uaminifu wa zana za kijeshi za China, suala ambalo halina maslahi kwa Beijing wala Tehran.
Imetafafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi