Je, Elon Musk anaweza kuwa Rais wa Marekani?

Muda wa kusoma: Dakika 7

Wanasema kwamba huko Marekani, ndoto hutimia, hata ikiwa inaonekana kuwa haiwezekani. Lakini vipi ikiwa ndoto hiyo inaingia Ikulu?

Kabla ya 2009, Waamerika wengi weusi hawakuamini kwamba mmoja wao angeweza kufikia nafasi hiyo. Imani hii iliendelea hadi Barack Obama akawa rais wa kwanza mwenye asili ya Kiafrika, na hivyo kusambaratisha imani hiyo.

Katika hotuba yake ya ushindi, Obama alisema, "Mistari mirefu mbele ya shule na makanisa ni uthibitisho kwamba hadithi yako huko Marekani bado haijaandikwa na kwamba ndoto bado iko hai."

Hii ilikuwa ndoto sawa na ambayo Martin Luther King, Jr., alielezea miaka mingi iliyopita katika hotuba yake maarufu ya "I have a dream"

Je, hii ndiyo ndoto ambayo Elon Musk, mtu tajiri zaidi duniani, anayo?

Chama kichanga dhidi ya kikwazo cha zamani

Bilionea huyo wa Canada na Marekani hivi karibuni alitangaza kuundwa kwa "Chama cha Marekani," hatua ambayo alisema ilikuwa kujibu "hitaji pana la umma" kati ya wafuasi wake kwenye jukwaa la mtandao wa kijamii X. Hatua hiyo inaashiria kujitenga kwake rasmi na mshirika wake wa zamani na mpinzani wa sasa, Donald Trump.

Tangazo la kuanzishwa kwa chama hicho mara moja lilizua wimbi la upinzani wa kisiasa na kisheria. Trump aliita hatua hiyo "ya kipuuzi" na kusema haina maana ndani ya mfumo ulioanzishwa wa Marekani wa vyama viwili.

Kwa mtazamo wa wachambuzi, chama kipya cha Musk ni jaribio la kunyonya mamilioni ya wafuasi wake kwenye mitandao ya kijamii na kujaza pengo lililotokana na watu huru kutoridhika na vyama hivyo viwili vya jadi.

Lakini je, mwanamume aliyezaliwa Afrika Kusini na baadaye akawa raia wa Marekani anaweza kupanda hadi cheo cha juu zaidi cha kisiasa nchini Marekani?

Jared Martin, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mhariri wa tovuti ya American Politics, aliiambia BBC: "Watu wamekuwa wakisubiri mabadiliko ya kimsingi katika nyanja ya kisiasa ya Marekani kwa miaka mingi.

Wakati wagombea huru au wa chama cha tatu wamejitokeza kwa nyakati tofauti, ni nadra kupata nafasi ya kufaulu katika muundo wa sasa wa vyama viwili."

Anaonyesha kuibuka kwa watu maarufu kama Andrew Yang na Chama cha Forwad party na sasa Elon Musk, ambao wanajaribu kupinga muundo wa jadi.

Kulingana naye, hata Trump, licha ya uanachama wake rasmi katika Chama cha Republican, ameunda aina ya utambulisho huru wa kisiasa wenye kauli mbiu "Make America Great Again," ambayo ni mbali na itikadi ya jadi ya chama.

Tariq Shami, mtaalamu wa masuala ya Marekani pia anasema: "Elon Musk anapenda kuonekana na wakati huo huo anatafuta ushawishi wa kisiasa.

Anaweza kuwa na udanganyifu kuhusu umaarufu wake wa kweli katika ulimwengu wa kweli, lakini kuundwa kwa chama kipya kunaonyesha kwamba ana nia ya kumaliza umaarufu wa Trump."

Kulingana na Shami, jukumu la Musk linaweza kuwa tu katika ufadhili na mwongozo wa kiakili kwa chama, na ikiwa atafanikiwa kwa kiasi, atakuwa na jukumu kama la 'godfather' katika chama.

Kikwazo cha kikatiba

Hata iwapo Musk atafanikiwa kuanzisha chama na kupata msingi mpana wa kitaifa, kuna kikwazo kimoja cha msingi ambacho si chama wala wafanyabiashara wakubwa wanaweza kukishinda: Katiba ya Marekani.

Kifungu cha II, Kifungu cha 5 cha Katiba kinasema kwamba ni "raia mzaliwa wa asili" ya Marekani ambaye ana umri wa angalau miaka 35 na ameishi Marekani kwa angalau miaka 14 anaweza kuwa rais. Musk, ambaye alikua raia mnamo 2002, hafikii mahitaji ya kwanza.

Jared Martin anasema umaarufu wa Musk unaweza kuibua mjadala wa kitaifa kuhusu "uraia wa kuzaliwa" na kuchunguza tena maana ya kuwa Mmarekani, hasa kwa vile anaweza kutumia fursa hiyo kukabiliana na jitihada za Trump za kuzuia uraia wake.

Hata hivyo, Martin anaamini kwamba Musk hawezi kupata uungwaji mkono wa kutosha kurekebisha sehemu hii ya Katiba; ingawa inaweza kuchukua jukumu la Trump la kuzuia haki za wahamiaji.

Njia ya kuelekea kwenye mageuzi ya sheria

Kuna njia mbili za kurekebisha Katiba: kura ya theluthi mbili katika mabunge yote mawili ya Congress ikifuatiwa na kuidhinishwa na robo tatu ya majimbo; au mkutano rasmi wa theluthi mbili ya majimbo ili kuandaa marekebisho, ambayo hayajawahi kutekelezwa.

"Kubadilisha katiba ni kazi ngumu sana na inayotumia muda mwingi. Kutokana na mgawanyiko wa kisiasa uliokithiri nchini Marekani, ni jambo lisilowezekana," anasema Tariq Shami.

Anaongeza kuwa itahitaji idhini ya thuluthi mbili katika Seneti na Baraza la Wawakilishi, na kisha robo tatu ya mabunge ya majimbo kuidhinisha. "Pamoja na upinzani mkubwa kutoka kwa pande zote mbili kuu, nadhani haiwezekani kutokea."

Jared Martin pia alisema, akizungumzia utata wa muhula wa pili wa Trump, "Nimejifunza kusema haiwezekani, lakini sidhani kama kuna msaada wa kutosha kuondoa kikwazo hiki cha kisheria.

Juhudi zilizopita

Kumekuwa na mapendekezo huko nyuma kuruhusu raia wa asili kugombea urais.

Maarufu zaidi kati ya haya ni mswada wa Seneta Orrin Hatch wa "Fursa Sawa ya Kutawala" mwaka wa 2003, ambao ungeruhusu raia ambao walikuwa wametawaliwa kwa angalau miaka 20 kugombea urais.

Mpango huu ulipendekezwa wakati wa umaarufu wa Arnold Schwarzenegger, gavana mzaliwa wa Austria wa California, na kwa sababu hii uliitwa jina la utani "Arnold Amendment."

Lakini mpango huo hata haukufanya mswada huo kupita kamati ya bunge kwa sababu ya upinzani mkubwa wa umma.

Kura ya maoni ya Gallup mwaka huo huo iligundua kuwa ni asilimia 28 tu ya watu walioidhinisha wazo hilo, huku asilimia 70 wakilipinga.

Marekani ya leo na ya Jana

Hali ya kisiasa nchini Marekani leo ni tofauti sana na mwaka 2003. Migogoro ya vyama imeongezeka, na kuna mijadala iliyoenea kwa pande zote mbili kuhusu kurekebisha Katiba, kuweka mipaka katika Mahakama ya Juu zaidi, na kuondoa mfumo wa uchaguzi wa wajumbe.

Hali hii imeongeza uwezekano wa msaada wa kuondoa mahitaji ya "kuzaliwa Marekani ", hasa kati ya wahamiaji.

"Vyama vipya vinaweza kuunda tofauti za kiakili na kuweka njia ya makubaliano na ushirikiano, badala ya chama kimoja kuharibu mara kwa mara mafanikio ya mwingine," anasema Martin.

Anaongeza kuwa kuwepo kwa mfumo wa vyama vingi kunawalazimu wabunge na serikali kushirikiana katika pande zote, jambo ambalo linaweza kufanya utawala kuwa rahisi na wenye nguvu.

Kwa wengine, nguvu kuu ya Musk ni umaarufu wake; akiwa na wafuasi milioni 222 kwenye X, rekodi nzuri ya uvumbuzi wa viwanda, na ushawishi mkubwa wa vyombo vya habari, anaweza kuanzisha kampeni ya kitaifa ya mageuzi ya sheria.

Lakini Al-Shami anaonya kwamba umaarufu pekee hautoshi: "Hata kama Musk atatumia mamia ya mamilioni ya dola, itakuwa vigumu kuleta shinikizo inayohitajika miongoni mwa umma au wanasiasa kubadilisha katiba.

Chaguo mbele yake

Kisheria, Musk hawezi kuwa rais mradi tu kifungu cha "mzaliwa wa Marekani" katika Kifungu cha II cha Katiba kinasalia.

Kisiasa, kuanzisha chama kunaweza kumpa madaraka mengi ya kujadiliana, lakini hakuwezi kumfungulia njia ya urais.

Kinadharia, ingawa katiba imefanyiwa marekebisho mara 27, kifungu kinachohusiana na "uraia wa kuzaliwa" ni mojawapo ya magumu zaidi kubadilika kutokana na uhusiano wake na dhana ya uhuru wa taifa na uaminifu wa pande mbili.

"Marekani bado inajitahidi kufafanua utambulisho wake wa kitaifa," Martin anasema. Masuala kama vile uraia na uhamiaji ni sehemu ya mapambano haya ya utambulisho.

"Leo tuna fursa ya kufafanua upya maana ya kuwa Mmarekani, ikiwezekana kwa kukataa mielekeo ya utaifa ya utawala wa sasa na kuleta maono jumuishi zaidi ya uraia kwa kuzingatia usawa wa haki na fursa."

Alisema kuundwa kwa vyama vipya na endelevu vya kisiasa kunaweza kuimarisha hali ya kujihusisha kisiasa. Waamerika wengi wana imani ambazo haziendani na mfumo wa vyama viwili vya Democratic-Republican.

"Vyama vingi vinaongoza kwa demokrasia yenye afya na uwakilishi bora wa watu. Watu hawahitaji tena kujitolea kwa maadili na imani zao ili kushiriki katika siasa."

Hatimaye, Elon Musk anaweza kutuma roketi kwa sayari ya Mars na kupeleka mtandao wa satelaiti wa Starlink katika mzunguko wa Dunia, lakini kasi yake ya roketi haitamfikisha Ikulu ya Marekani hadi kufanyike marekebisho ya katiba.

Kichwa cha "rais wa kwanza asiye mzawa wa Marekani" ni dhana ya kisiasa zaidi kuliko ukweli unaoweza kufikiwa kwa sasa, isipokuwa Musk anaweza kushawishi majimbo 38 kubadili sheria iliyoanzia karne ya 19.

Lakini kwa kuzingatia mienendo yenye utata ya Trump katika siasa za Marekani, hata walio na matumaini zaidi wanauliza: iwapo Musk ni "mwendawazimu" zaidi kuliko Trump?

Imetafasiriwa na Seif Abdalla