Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Marekani 2024: Elon Musk anawapa baadhi ya wapiga kura dola milioni 1. Je, ni halali?
- Author, Sam Cabral, James FitzGerald & Jake Horton
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Maswali yameibuka kuhusu uhalali wa pesa za bilionea wa teknolojia Elon Musk kwa wapiga kura wa majimbo mbalimbali wanaotia saini ombi lake, kabla ya uchaguzi wa Marekani tarehe 5 Novemba.
Ombi hilo liliundwa na kundi la kampeni la Musk la America PAC, ambalo lilianzishwa ili kumuunga mkono Donald Trump katika kinyang'anyiro cha urais.
Lakini wataalam wa sheria wanasema huenda hilo linavunja sheria ya Marekani - kutoa pesa kwa mtu aliyesajiliwa kama mpiga kura.
Musk anatoa nini?
Ombi lililoundwa na Amerika PAC linawahimiza wapiga kura katika majimbo sita - Georgia, Nevada, Arizona, Michigan, Wisconsin na North Carolina - kutia saini ya "kuunga mkono uhuru wa kujieleza na haki ya kubeba silaha."
Wale wanaoleta mpiga kura mwingine atakayetia saini hupewa kiasi cha dola za kimarekani 47. Kiasi cha juu cha dola 100 kwa kusaini au kumleta mtu wa kusaini hutolewa huko Pennsylvania, jimbo ambalo ni uwanja wa vita kati ya Trump na Harris na kura zao huko zinaaminiwa zinaweza kuamua mshindi wa mwisho.
Amerika PAC inasema wale wanaotia saini ombi hilo wanaashiria kuunga mkono kifungu cha kwanza na cha pili cha katiba ya Marekani.
Kila siku hadi siku ya kupiga kura tarehe 5 Novemba, zawadi ya dola milioni 1 itatolewa katika mfumo wa bahati nasibu kwa mtu yeyote aliyetia saini katika mojawapo ya majimbo saba.
Je, ni halali?
"Naamini pesa ya [Elon] Musk inaweza kuwa ni kinyume cha sheria," anasema Paul Schiff Berman, profesa wa sheria wa Chuo Kikuu cha George Washington.
Kanuni za Marekani kuhusu sheria ya uchaguzi, inasema mtu yeyote "anayelipa au kujitolea kulipa au kukubali malipo - kwa ajili ya kujiandikisha kupiga kura au kupiga kura" anaweza kutozwa faini ya dola 10,000 au kifungo cha miaka mitano jela.
"Pesa zake ziko kwa ajili ya wapiga kura waliojiandikisha tu, kwa hivyo nadhani anakwenda kinyume na sheria hii," anasema Berman.
Idara ya Sheria ya Marekani ilikataa kutoa maoni. Tume ya Shirikisho ya Uchaguzi (FEC) imefuatwa ili kutoa kauli.
“Hoja ya kuvunja kanuni inaweza kuwa dhaifu, kwa sababu hakuna anayelipwa moja kwa moja ili kujiandikisha au kupiga kura,” anasema mwenyekiti wa zamani wa FEC, Brad Smith.
"Hawalipi watu kujiandikisha kupiga kura. Anawalipa ili kutia saini ombi lake - na anataka watu waliojiandikisha tu kupiga kura kutia saini ombi hilo. Kwa hiyo nadhani yuko sawa hapa,” anasema.
Lakini profesa wa sheria za uchaguzi katika Chuo Kikuu cha Northwestern aliambia BBC lengo la pesa hiyo kutolewa ni muhimu.
"Naelewa kwa baadhi ya wachambuzi kuwa sio kinyume cha sheria, lakini lengo moja liko wazi, kushawishi watu kujiandikisha kupiga kura kwa njia ambayo ina shida kisheria," anasema Michael Kang.
Adav Noti kutoka kituo cha Campaign Legal Center, anasema mpango wa Musk "unakiuka sheria ya shirikisho na uko chini ya kosa la kiraia au jinai kwa mujibu wa Idara ya Haki."
"Ni kinyume cha sheria kutoa pesa kwa masharti kwamba wapokeaji wawe wamejisajili kama wapiga kura," anasema Noti.
Profesa wa sheria za katiba Jeremy Paul, kutoka Chuo Kikuu cha Northeastern anasema katika barua pepe kwa BBC kwamba Musk anatumia mwanya wa kisheria.
Ingawa kuna hoja kwamba pesa hizo zinaweza kuwa kinyume cha sheria, “lakini zinatolewa kwa mtindo wa kuizunguka sheria" na anaamini kesi hiyo itakuwa ngumu mahakamani.
Hoja za Kisheria
Gavana wa Pennsylvania Josh Shapiro, anasema jambo hilo, linatia mashaka na kutoa wito kwa vyombo cha sheria kuchunguza.
Mwekezaji bilionea Mark Cuban, ambaye amefanya kampeni katika wiki za hivi karibuni kwa Kamala Harris, anasema:
"Ikiwa mpango huo utafanya kazi au la ni jambo jingine. Na mpango huo unaweza hata kukupa matokeo tofauti na uyatakayo," aliiambia CNBC.
Musk amejibu ukosoaji huo, akisema Democratic na wafadhili wao wamefadhili mipango kama hiyo hapo awali.
Kwenye X, aliweka chapisho linalosema bosi wa Meta, Mark Zuckerburg "alifanya vivyo hivyo mwaka 2020."
Zuckerburg alichangia dola milioni 400 katika uchaguzi wa 2020 - lakini pesa hiyo ilitolewa kwa mashirika mawili yasiyoegemea upande wowote ili kusaidia vifaa katika upigaji kura kwa njia ya posta. Haikutolewa moja kwa moja kwa wapiga kura.
Huko nyuma Chama cha Democratic, kiliwahi kuwekeza katika mipango ya kuongeza wafuasi, kwa kampeni ya usajili wa wapiga kura ya dola milioni 25 katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani wa 2022.
Lakini pesa hizi hazikutolewa moja kwa moja kwa wapiga kura. Pesa hizo zilikuwa ni za mipango ya kuwahimiza wapiga kura kujiandikisha, na zilitolewa kwa wale walioajiriwa kubisha hodi nyumba hadi nyumba, na kwa matangazo ya televisheni na mtandaoni.
"Ni halali kuwalipa watu kwenda kusajili wapiga kura, lakini huwezi kuwalipa watu moja kwa moja kujiandikisha," anasema Prof Kang.
Musk na siasa za Marekani
Tajiri huyo mkubwa zaidi duniani alikuwa na uhusiano mbaya na Trump wakati Trump alipokuwa rais, lakini Musk ameelezea kutofurahishwa kwake na Democratic katika miaka ya hivi karibuni.
Kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa 2022, alitangaza amekihama chama hicho na kuwahimiza wafuasi wake kupiga kura Republican.
Mwaka huu, amejihusisha na siasa za Marekani, akitoa michango na machapisho ya mitandaoni kwa niaba ya Warepublican kadhaa.
Katika maoni yake wiki iliyopita, alieleza kuwa sehemu kubwa ya mpaka wa Marekani na Mexico ni kama filamu ya World War Z.
Musk alizindua America PAC, Julai kwa lengo la kuunga mkono kampeni za Trump za kuwa rais. Hadi sasa amechangia takribani dola milioni 75 katika kikundi hicho.
Tovuti ya Amerika PAC inasema inataka "udhibiti wa mipaka", "miji salama", "uhuru wa kujieleza", "matumizi mazuri ya pesa", "mfumo sawa wa haki" na "kujilinda".
Katika wiki za hivi karibuni, Musk ameonekana kwenye kampeni kwa mara ya kwanza, akiwa na Trump na katika ukumbi mwingine akiwa mwenyewe.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Yusuf Jumah