Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Nilimkataza ila walanguzi wa binadamu walimhadaa kwa kumpa maneno matamu'
Ni giza, kumetengwa na hali ya hewa ni baridi kali.
Fazal Ahmed (sio jina lake halisi) ana umri wa miaka 24 na hajaolewa.
Baada ya kuishi katika kambi za wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh kwa zaidi ya muongo mmoja, ameamua kuondoka kwa kupitia walanguzi wa binadamu.
Anasogea kwa tahadhari kuelekea mto unaogawanya Cox's Bazaar nchini Bangladesh kutoka jimbo la Rakhine la Myanmar.
"Ninajua watu wengi wamekufa njiani, lakini pia ninafahamu wengi ambao wamefika Malaysia. Siwezi kuendelea kuishi hivi," Ahmed anaiambia BBC.
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi linasema kuwa takriban Warohingya 348 walifariki au kutoweka baharini mwaka 2022, jambo ambalo linaufanya kuwa mmoja wa miaka ya vifo vingi zaidi tangu 2014.
Hata hivyo Umoja wa Mataifa unasema kumekuwa na ongezeko la idadi ya watu wanaofanya safari hatari ya baharini kuelekea Malaysia. Ni nini kinachowasukuma wakimbizi kupuuza hatari inayowakodolea macho?
Ahmed ana dada wadogo watatu na kaka wawili. Wazazi wake walifariki na sasa yeye ndiye kichwa cha familia. Anataka kuboresha matazamio ya familia yake.
"Nchini Bangladesh maisha yetu si salama. Hatuna fursa zozote za kufanya kazi," anasema.
Ahmed anatumai maisha yake yatabadilika na kuwa mazuri mara tu atakapofika Malaysia.
Wakimbizi Waislamu wa Rohingya wamekuwa wakikimbilia Bangladesh kwa miongo kadhaa. Nchi yao ya Myanmar inakataa kuwatambua kama raia.
Jeshi la Myanmar lilianzisha operesheni kubwa katika jimbo la Rakhine mnamo 2017 ambayo UN inaelezea kama "mfano wa kitabu cha kiada kuhusu mauaji ya halaiki".
Takriban Warohingya milioni moja walikimbilia Bangladesh.
Ahmed na familia yake walikuwa tayari wanaishi katika kambi za wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh kabla ya hapo.
"Tulipoteza matumaini kwamba Myanmar itaturudisha nyuma," anasema.
Ahmed aliwasiliana na wakala ambaye aliahidi kumpeleka Malaysia kwa takriban $4,400. Tayari amelipa $950 kama malipo ya kwanza. Familia yake itafanya malipo hayo kulingana na maendeleo yake.
Dada zake ambao wanafanya kazi kama kina dada wa kazi walichangisha sehemu ya pesa hizo. Mengine yanatokana na kuuza vito vya dhahabu vya familia.
Watu wasijulikana walipo
UNHCR inasema wakimbizi 3,500 wa Rohingya walijaribu kuvuka baharini mwaka jana, ikilinganishwa na 700 mwaka 2021.
Baadhi ya boti huzama na hazipatikani tena. Umoja wa Mataifa unasema boti moja, inayodhaniwa kuondoka Cox's Bazar tarehe 2 Disemba 2022 ikiwa na takriban wakimbizi 180 wa Rohingya, ilizama katika Bahari ya Andaman.
Kwa kuwa Warohingya wanasalia bila utaifa na wanafanya safari hiyo kupitia mitandao ya uhalifu, ni juhudi kidogo tu jamaa wanaweza kufanya kuwatafuta wale wanaopotea.
Sharifa Khatun ni mjane mwenye umri wa miaka 33 ambaye ameishi katika kambi hiyo ya wakimbizi tangu 2016.
Watu wanne wa familia yake wametoweka baharini. "Dada yangu alikwenda Malaysia na watoto wake watatu - binti wawili na wa kiume," anasema.
Shemeji yake alikuwa tayari ametorokea Malaysia kutoka Myanmar nyuma mwaka wa 2013 kwa kusafiri kwa mashua hatari.
Dadake Khatun na watoto wao kisha walikimbia hadi Bangladesh mwaka wa 2016 ili kuepuka vurugu. Tangu wakati huo, ametaka kujiunga na mume wake huko Malaysia.
"Walanguzi hao wa binadamu walimpa matumaini. Dada yangu alilipa takriban dola 2,500 kama awamu ya kwanza na akanipa maagizo nilipe kiasi kilichobaki pindi atakapofika anakoenda," anasema Khatun.
"Aliondoka tarehe 22 Novemba na baada ya takriban wiki mbili alinipigia simu kutoka kitongoji cha Rathedaung, kilicho kando ya pwani katika jimbo la Rakhine nchini Myanmar."
Tangu wakati huo, Khatun hajasikia chochote kutoka kwa dada yake.
"Nilimkataza dada yangu asiende, ila walanguzi wa binadamu walimhadaa kwa kumpa maneno matamu."
Kuongezeka kwa ulanguzi wa binadamu
Kambi ya wakimbizi ya Kutupalong katika eneo la Cox's Bazar - ambayo mara nyingi hubainika kama kubwa zaidi duniani - inapokea watu wengi kama Khatun ambao hawajui nini kimewapata wapendwa wao.
"Usafirishaji haramu wa binadamu unaongezeka siku baada ya siku. Sijui jinsi ya kukomesha," anasema Mohammed Aziz, mwanaharakati wa Rohingya kutoka Cox's Bazar.
"Katika nusu ya pili ya Januari takriban boti tatu zilikwenda Malaysia. Moja tarehe 16 Januari, mashua ya pili tarehe 20 na ya mwisho tarehe 27."
Anasema zaidi ya watu 350 walikuwa kwenye boti hizi, na huenda kuna wengine.
Vyanzo vya habari ndani ya kambi za Rohingya vimeiambia BBC kwamba mashua iliyokuwa na watu 200 iliondoka kutoka Tankaf nchini Bangladesh tarehe 17 Februari.
Kwa kuwa wakimbizi wa Rohingya hawaruhusiwi kufanya kazi, Aziz anasema wengi wa wakimbizi hao hupokea pesa kutoka kwa jamaa zao nje ya nchi ili kufadhili safari hiyo.
"Wengi wa wahamiaji ni vijana wa kiume na wa kike. Baadhi ya watu huondo watoto wao pamoja nao."
Wasafirishaji haramu binadamukwa kawaida hutumia boti za uvuvi kwa safari ambazo hazitakiwi kubeba watu wengi kwa umbali mrefu.
Pia wanatia chumvi kile kinachowangoja wasafiri hao wanakwenda ukutana nao"
"Mawakala wanawaambia wakimbizi kwamba baada ya kufika Malaysia wanaweza kupata hifadhi nchini Marekani, Canada na Ulaya," anasema Aziz.
"Yote ni uwongo."
Kutokuwa na matumaini na kukata tamaa
Lakini kwa Warohingya wengi, kukaa Bangladesh, mojawapo ya nchi zenye watu wengi zaidi duniani, pia hakuvutii.
"Kambi haziwezi kuwa kama nyumbani kamwe. Wanazidi kukosa matumaini na kukata tamaa. Ndiyo maana wanajaribu kufanya safari ya hatari," anasema Mohammad Mizanur Rahman, mratibu wa NGO katika Cox's Bazar.
"Tumefungua kesi 12 za usafirishaji binadamu kwa njia haramu mwaka uliopita. Pia tumekamata watu wanaohusika na hili na kukamata baadhi ya boti zilizokuwa zikitumika kusafirisha watu," anasema Rahman.
Mamlaka ya Bangladesh na Umoja wa Mataifa wote wanasema kuwa wanachukua hatua za kuonya dhidi ya uhamiaji usio wa kawaida, lakini, kwa kuwa safari nyingi hufanyika kwa usiri, Umoja wa Mataifa unasema inakuwa na wakati mgumu kufuatilia watu wanaoondoka.
"UNHCR haina uwezo wa kutafuta watu baharini. Ikiwa tutafahamishwa kuhusu meli iliyozama tunaweza kutahadharisha UN au mashirika mengine ya kibinadamu yaliyo karibu," anasema Regina De La Portilla, afisa wa Mawasiliano wa UNHCR katika Cox's Bazar.
Katika siku za nyuma, Umoja wa Mataifa umefanikiwa kutoa msaada kwa boti zenye shida baharini. Boti moja ya aina hiyo ikiwa na zaidi ya wakimbizi 100 wa Rohingya hatimaye ilifika Sri Lanka mwezi Desemba.
Matumaini
Kurudi kambini, Khatun bado yuko katika hali ya sintofahamu.
Hafurahishwi na hali yake ya maisha lakini mjane huyo mwenye watoto watatu ameazimia kusalia.
Hana uhakika ni nani atamsaidia kupata habari kuhusu dada yake aliyepotea.
"Nina huzuni sana. Sina habari zozote kuwahusu. Mara ya mwisho nilizungumza nao ilikuwa tarehe 14 Desemba," anasema Khatun.
"Natumai kumuona dada yangu na watoto wake siku moja."
Kuondoka kwa hisia
Saa moja baada ya kuzungumza nasi, Fazal Ahmed anapokea simu kutoka kwa wafanyabiashara hao.
Yeye hatasubiri.
Ahmed anavua viatu vyake na kukunja saruale yake. Anapofika ukingo wa maji, kuna msukumo wa hisia.
“Dada zangu na kaka zangu waliniambia nisiende, sina kazi yoyote hapa,” anasema huku akianza kulia.
Anatarajia kufanya kazi kama kibarua kwani hajui kusoma wala kuandika.
"Naenda Malaysia kutafuta pesa kwa ajili ya ndugu zangu. Itasaidia kaka na dada zangu kusoma."
Ahmed anajua itakuwa safari ya kubadilisha maisha, kwa njia moja au nyingine.
Anapita kwenye maji gizani kuelekea kwenye mashua anayotarajia itamsafirisha hadi kwenye maisha yenye matumaini.