Sokwe huonesha 'ishara' kupitia midundo yao ya ngoma

ggg

Chanzo cha picha, A SOLDATI

Sokwe mwitu wana "mtindo wao wa kupiga ngoma " kwa mujibu wa wanasayansi.

Watafiti waliofuatilia na kuchunguza sokwe katika msitu wa Uganda waligundua kuwa wanyama hao hutumiana ujumbe wao kwa wao kwenye mizizi ya miti.

Wanasayansi hao wanasema kwamba ishara ya midundo huwaruhusu kutuma taarifa kwa umbali mrefu, kufichua ni nani yuko wapi na anafanya nini.

Matokeo ya utafiti huo yamechapishwa katika jarida la wanyama la Animal Behaviour.

Dkt Catherine Hobaiter kutoka Chuo Kikuu cha St Andrews alieleza kuwa nyani hao wa porini hutumia mizizi mikubwa ya miti kama ubao ili kupiga ngoma kwa mikono na miguu.

"Ukigonga mizizi kwa nguvu sana, inasikika na kutoa sauti kubwa ya kina, inayovuma ambayo husafiri msituni," aliambia kipindi cha Sayansi ya BBC Radio 4.

"Mara nyingi tuliweza kutambua ni nani aliyekuwa akipiga ngoma tulipowasikia; ilikuwa ni njia nzuri sana ya kuwapata sokwe mbalimbali tuliokuwa tukiwatafuta. Kwa hiyo kama tumeweza kufanya hivyo, tulikuwa na uhakika wangeweza pia."

Kila sokwe dume, wanasayansi waligundua, hutumia muundo tofauti wa mapigo. Wanaichanganya na sauti za masafa marefu, zinazoitwa pant-hoots. Na wanyama tofauti hupiga ngoma katika sehemu tofauti.

Mtafiti mkuu juu ya utafiti huu, mwanafunzi wa PhD Vesta Eleuteri kutoka Chuo Kikuu cha Vienna, alielezea jinsi baadhi ya viumbe kuwa na mdundo wa mara kwa mara, kama wapiga ngoma za rock na blues, ilhali wengine wana midundo tofauti zaidi, kama jazz.

"Nilishangaa kwamba niliweza kutambua ni nani aliyekuwa akipiga ngoma baada ya wiki chache tu msituni," alisema. "Lakini midundo yao ya ngoma ni ya kipekee sana kwamba ni rahisi kuipokea."

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Bi Eleuteri alielezea sokwe mmoja mchanga wa kiume, ambaye watafiti walimpa jina la Tristan, kama "John Bonham (marehemu Led Zeppelin mpiga ngoma) wa msituni".

"Anafanya onesho hili refu la ngoma zenye midundo mingi na unaweza kuwaambia kutoka mbali, kwa hivyo unaweza kusema ni Tristan anapiga ngoma."

Wanyama hao pia walionekana kutumia tu mdundo wao waishara walipokuwa wakisafiri. Watafiti wanakisia kuwa sokwe huchagua kutoa au kutotoa utambulisho wake.

Dk Hobaiter aliongeza kuwa kuelewa upigaji wa sokwe kwa njia hii kunaweza kutatua fumbo la muda mrefu la mawasiliano: sokwe-mwitu husalimiana wanapokutana, lakini hawaonekani "kuaga" wanapogawanyika msituni.

"Huenda sokwe wasihitaji kusema kwaheri, kwa sababu wanaweza kuwasiliana wanapokuwa mbali," Dk Hobaiter alieleza.

"Ishara hizi za umbali mrefu huwapa sokwe njia ya kuwasiliana wao kwa wao. Hilo linaweza kutusaidia kuelewa mojawapo ya mambo haya ambayo tulifikiri yalikuwa tofauti ya kweli kati ya sokwe na binadamu na kutusaidia kuelewa kwa nini tofauti hiyo inaweza kutokea".