Ijue meli 'shujaa' inayoshughulika na matatizo ya mtandao Afrika

...
Muda wa kusoma: Dakika 6

Meli yenye ukubwa kama uwanja wa soka, ikiwa na wahandisi na wataalamu zaidi ya 50, inazunguka baharini karibu na Afrika ili kuendelea kuweka bara hili kwenye mtandao.

Inatoa huduma muhimu, kama ilivyoshuhudiwa kuzimika kwa mtandao mwaka jana wakati nyaya za mtandao zilizofungwa chini ya bahari zilipopata hitilafu.

Mamilioni kutoka Lagos hadi Nairobi yalizama katika giza la kidijitali: programu za ujumbe zilishindwa kufanya kazi na miamala ya benki ikikwama. Iliwafanya wafanyabiashara na watu binafsi kutatizika pakubwa.

Ni Léon Thévenin iliyoleta suluhisho la matatizo ya nyaya hizo nyingi. Meli hii, ambayo kikosi kazi cha BBC kilisafiri nayo kwa wiki moja katika mwambao wa Ghana, imekuwa ikifanya kazi hii maalum ya kutengeneza nyaya kwa zaidi ya miaka 13.

"Kwa sababu yangu, nchi zinaendelea kunufaika na utumiaji wa mtandao," anasema Shuru Arendse, mtaalamu msaidizi wa kuunganisha nyaya kutoka Afrika Kusini ambaye amekuwa akifanya kazi kwenye meli hii kwa zaidi ya muongo mmoja, akizungumza na BBC.

Wataalamu wa IT nyumbani wana kazi kwa sababu mimi naleta chanzo kikuu cha mtandao," anasema.

"Unaweza kuwa na mashujaa wanaookoa maisha - mimi ni shujaa kwa sababu ninaokoa mawasiliano."

Fahari na shauku yake inaonyesha hisia za wafanyakazi wenye ujuzi kwenye meli ya Léon Thévenin, ambayo ina ghorofa nane juu ya ardhi na ikibeba vifaa mbalimbali.

Mtandao wa intaneti ni mtandao wa kompyuta na seva - ili kusoma makala hii, kuna uwezekano kuwa takriban moja ya nyaya 600 mahsusi duniani zilikusanya data ili kukuwezesha kuona kwenye skrini yako.

Seva nyingi hizi zipo kwenye vituo vya data nje ya Afrika na nyaya hizo hutandazwa chini ya bahari kuunganisha mtandao na miji ya pwani barani Afrika.

Data husafiri kupitia nyaya nyembamba za fibreglass, mara nyingi zimeunganishwa kwa jozi na kulindwa kwa tabaka tofauti za plastiki na shaba kulingana na umbali wa nyaya kutoka pwani.

"Mradi tu seva hazipo nchini mwako, unahitaji kuunganishwa. Nyaya hufuata kutoka nchi moja hadi nyingine, kuunganisha watumiaji na seva zinazohifadhi data zao - iwe ni kufikia Facebook au huduma nyingine yoyote ya mtandao," anasema Benjamin Smith, kaimu mkuu wa wataalam wa Léon Thévenin.

...
Maelezo ya picha, Léon Thévenin imekuwa ikizunguka bahari za Afrika kwa zaidi ya miaka 13 ikihudumia nyaya za chini ya bahari.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Nyaya maalum za mtandao ambazo hutandikwa chini ya bahari zimeundwa kufanya kazi kwa miaka 25 kwa matengenezo madogo, lakini zinapoharibika, mara nyingi hutokana na shughuli za binadamu.

"Kwa kawaida, nyaya hazikatiki kwa asili isipokuwa zikiwa katika eneo lenye mizunguko mikali ya maji na mawe makali," anasema Charles Heald, ambaye anasimamia kifaa hicho cha meli (ROV).

"Lakini mara nyingi ni watu wanaoegesha meli mahali wasipopaswa na meli za uvuvi wa samaki zinaweza kugusa chini ya bahari, hivyo kwa kawaida tungeweza kuona alama za uvuvi."

Bwana Smith pia anasema majanga ya asili husababisha uharibifu wa nyaya, hasa katika sehemu za bara lenye hali mbaya ya hewa. Anatoa mfano wa bahari za pwani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ambapo Mto Congo unamwagamaji katika Bahari ya Atlantiki.

"Katika eneo la Congo, ambapo kuna mvua nyingi na joto la chini, inaweza kuunda mizunguko ambayo huweza kuharibu nyaya," anasema.

Ni vigumu kutambua uharibifu wa makusudi - lakini wafanyakazi wa meli ya Léon Thévenin wanasema hawajashuhudia ushahidi wazi wa hili wenyewe.

Mwaka mmoja uliopita, nyaya tatu muhimu katika Bahari ya Shamu - Seacom, AAE-1 na EIG - zilikatika, kwa mujibu wa taarifa kutokana na nanga ya meli, na kusababisha kukatika kwa mtandao kwa mamilioni ya watu kote Mashariki ya Afrika, ikiwemo Kenya, Tanzania, Uganda na Msumbiji.

Mwezi mmoja baadaye, mnamo Machi 2024, seti nyingine za nyaya zilizopata hitilafu katika nyaya za Wacs, Ace, Sat-3, na MainOne kwenye pwani ya Afrika Magharibi zilisababisha kuzimika kwa intaneti kubwa kote Nigeria, Ghana, Ivory Coast na Liberia.

Kila kitu kilichohitaji mtandao kufanya kazi kiliathirika huku matengenezo yakichukua wiki kadhaa.

Kisha mnamo Mei, changamoto nyingine: nyaya za Seacom na Eassy ziliharibika kwenye pwani ya Afrika Kusini, na kuathiri tena muunganisho katika mataifa mengi ya Afrika Mashariki.

Makosa haya hugunduliwa kwa kupima nguvu za umeme na alama zinazopita kwenye nyaya.

"Kunaweza kuwa na volts 3,000 kwenye nyaya na ghafla inashuka hadi 50 volts, hii inamaanisha kuna tatizo," anafafanua Loic Wallerand, mkuu wa wataalamu wa meli hiyo.

Unaweza pia kusoma
..
Maelezo ya picha, Ndani ya kebo ya intaneti kuna nyaya kadhaa za fibreglass.

Kuna wataalamu wa eneo husika wenye uwezo wa kushughulikia hitilafu kwenye maeneo ya maji ya kina kifupi, lakini ikiwa hitilafu itagundulika zaidi ya urefu wa mita 50 (ft 164), meli hii huitwa kuchukua hatua.

Wafanyakazi wake wanaweza kutengeneza nyaya zilizozama zaidi ya mita 5,000 chini ya kiwango cha bahari.

Matengenezo yaliyoshuhudiwa na BBC katika mwambao wa Ghana yalichukua zaidi ya wiki moja kukamilika, lakini watumiaji wengi wa intaneti hawakugundua kwa sababu kebo nyingine ilitumika.

Kila aina ya matengenezo hutegemea sehemu ya kebo iliyoathirika.

Ikiwa nyuzi za fibreglass kwenye chanzo zimekatika, inamaanisha kuwa data haiwezi kusafiri kwenye mtandao na inapaswa kutumwa kwenye kebo nyingine.

Lakini baadhi ya nchi za Afrika zina kebo moja pekee inayohudumia. Hii inamaanisha kuwa kebo iliyoathirika kwa njia hii inaliacha eneo lililoathirika bila intaneti.

Wakati mwingine, tabaka linalokinga fibreglass linaweza kuharibika, ambapo humaanisha usafirishaji wa data bado unafanyika, lakini kwa ufanisi mdogo. Katika hali zote, wafanyakazi lazima wapate mahali halisi palipoharibika.

Katika suala la nyaya za fibreglass zilizokatika, ishara ya mwanga inatumiwa kupitia kebo na kupitia sehemu yake ya kurudishia, wafanyakazi wanaweza kubaini mahali ambapo hitilafu imetokea.

Wakati tatizo likiwa ni uharibifu wa ufungaji wa kebo - inayojulikana kama "shunt fault" - inakuwa ngumu zaidi na ishara ya umeme lazima itumwe kupitia kebo ili kufuatilia wapi ilipopotea.

.
Maelezo ya picha, Kifaa kinachotumika kwa mbali (ROV) kinashushwa hadi kwenye sakafu ya bahari ili kutafuta sehemu ya kebo iliyo na hitilafu.

Baada ya kubaini eneo linaloweza kuwa na hitilafu, operesheni inahamia kwa timu ya ROV.

Imetengenezwa kama buldoza, ROV, ikiwa na uzito wa kilo 9.5, inashushwa chini ya maji kutoka kwenye meli ambapo inalekezwa hadi chini ya bahari.

Wafanyakazi watano wanashirikiana na muendesha mtambo huo crane kuizindua - mara tu inapochomolewa kutoka kwa kamba yake, inayoitwa umbilical cord, inapaa kwa ustadi.

"Haiwezi kuzama," anasema Bwana Heald, akielezea jinsi inavyotumia mashine nne za kusukuma mwelekeo wa usawa na wima kuhamia katika mwelekeo wowote.

Kamera tatu za ROV huwezesha timu iliyokuwa kwenye meli kutafuta mahali sahihi penye hitilafu inaposogea hadi kwenye salafu ya bahari.

Mara tu eneo lililoathirika linapotambuliwa, ROV hukata sehemu hiyo ikitumia mikono yake miwili, kisha inaiunganisha na kamba ambayo inavutwa kurudi kwenye meli.

Hapa, sehemu iliyo na hitilafu inatengwa na kubadilishwa kwa njia ya kuunganishwa na kebo mpya - mchakato unaoonekana kama ambao ulichukua saa 24 katika operesheni iliyoshuhudiwa na BBC.

Baada ya hapo, kebo inashushwa kwa uangalifu kurudi kwenye sakafu ya bahari na kisha ROV inafanya safari moja ya mwisho kukagua kama imetiwa mahali sahihi na kuchukua vipimo ili ramani ziweze kuhuishwa.

..
Maelezo ya picha, Ilichukua saa 24 kwa wataalamu wa teknolojia kutengeneza kebo iliyo na hitilafu katika mwambao wa Ghana.

Wakati tahadhari inapotolewa kuhusu kebo iliyo na hitilafu, wafanyakazi wa Léon Thévenin huwa tayari kuondoka ndani ya saa 24.

Hata hivyo, hatua hiyo hutegemea mambo kadhaa: mahali meli ilipo, upatikanaji wa nyaya za akiba na changamoto za kimamlaka.

"Vibali vinaweza kuchukua wiki. Wakati mwingine tunasafiri hadi nchi iliyoathirika na kusubiri pwani hadi hati zitakapokuwa zimekamilika," anasema Bwana Wallerand.

Kwa wastani, wafanyakazi hutumia zaidi ya miezi sita baharini kila mwaka.

"Ni sehemu ya kazi," anasema Kapteni Thomas Quehec.

Lakini wanapozungumza na wafanyakazi, ni vigumu kupuuza namna walivyojitolea binafsi.

Wanatokea kwenye asili na utaifa tofauti: Ufaransa, Kusini mwa Afrika, Filipino, Malagasy na wengine.

Adrian Morgan, mhudumu mkuu wa meli kutoka Afrika Kusini, amekosa sherehe za maadhimisho ya ndoa yake kwa miaka mitano mfululizo.

"Nilitaka kuacha. Ilikuwa vigumu kukaa mbali na familia yangu, lakini mke wangu alinipa moyo. Nafanya hivyo kwa ajili yao," anasema.

Unaweza pia kusoma

Imetafsiriwa na Martha Saranga na kuhaririwa na Ambia Hirsi