WARIDI WA BBC : Kutoka kuwa mchuuzi mpaka kutambulika kimataifa

Chanzo cha picha, Irene Kendi
Irene Kendi kutoka nchini Kenya akiwa na miaka 36 sasa amekabiliana na changamoto nyingi lakini ametafuta mbinu za kukabiliana na hali yake.
Kwanza kabisa maisha ya utotoni mwake yaliharibiwa mno hasa na kukataliwa na baba yake mzazi baada ya mama yake kushindwa kujaaliwa mtoto wa kiume baada ya kujifungua watoto wa kike wanne.
Vilevile hali ya umasikini mwingi ulioghubika jamii yake ulimfanya aamue kuwa mchuuzi katika umri mdogo wa miaka 10 pekee kama njia ya kusaidiana na mama kutoa riziki kwa familia yake wakiishi Kaunti ya Meru .
Kama anavyosema Irene, “Kungekuwa na siku ngumu zaidi mbeleni, lakini nilikataa kuruhusu hali ya wakati huo itawale hatima yangu ya baadaye ”.
Ugumu wa Maisha ya Utotoni
Mwanadada huyu anasimulia kuwa kipindi akiwa binti mdogo kilikuwa kipindi kigumu mno, huku mitazamo mingi alionayo katika maisha ya sasa ikitengenezwa wakati huo.
Irene pamoja na ndugu zake wengine walilelewa na mama, baada ya baba kuwatelekeza na kwa hiyo anasema kuwa kulelewa na mama asiye na mwenzi (na watoto sita) kulimaanisha maisha yalikuwa ni panda shuka za kila siku hasa jinsi ya kuwasomesha na pia kupata lishe ya kila siku.
“Kodi yetu ilikuwa ikichelewa kila mara na inarundikana, chakula kilikuwa haba, karo ya shule ilikuwa changamoto kubwa kiasi kwamba dada zangu waliacha shule. Mara nyingi tulidhihakiwa kwa unyonge na umasikini ”anasema Irene.
Sababu kubwa ya Mwanamke huyu kuanza kazi za uchuuzi akiwa na umri wa miaka 9 ilikuwa ili kuchangia mapato ya familia , anasema kuwa ni mama yake ambaye alimfunza mbinu za kuwa mchuuzi ngangari kwani hawakuwa na wakati wa kucheza au kufurahia utoto wao kama watoto wengine .
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Alipohitimisha shule ya sekondari ilikua bayana kuwa hangejiunga na chuo kikuu wakati huo na badala yake aliamini kuwa akitoroka na kuingia kwa ndoa labda shida zake zingefika kikomo asijue kuwa kwenye ndoa ndiko angekumbana na dhuluma nyingi .
“Kwa kweli, ndoa yangu nikiwa na umri wa miaka 20 iliongozwa na hitaji la kupata uthabiti maishani, na hata kule sikuwa na amani na niliamua njia ya kuishi pekee yangu pamoja na mwanangu ”anasema Irene
Ugumu huu wa maisha ya kuhangaika kila uchao uliendelea kumsukuma mama huyu kutathmini changamoto ambazo watu maskini wanakabiliana nazo na kumtia moyo daima kujitahidi zaidi maishani ili kuhakikisha kuwa maisha kama hayo hayajirudii tena kama yalivyokuwa ya mama yake.
Kwa sababu ya matatizo aliyokabiliana nayo , alijifunza kupigana kwa ajili yake na watu wengine walioathiriwa kam yeye.
“ Kama mama na mwanamke nilikataa kuwekwa kwenye makundi ya kuwa wanawake ni wadhaifu na kadhalika. Niliamini kuwa hakuna kitu nisichoweza kuafikia - nilifanya kufanya kazi kwa bidii ili kuzuia utoto wangu kujirudia katika maisha ya mwanangu,” aliongezea.
Maisha ya Chuo Kikuu

Chanzo cha picha, Irene Kendi
Akiwa na umri wa miaka 24 alikua ameweka akiba ya takribani pesa za Kenya shilingi milioni moja , hizi zilitokana na biashara ya uchuuzi pamoja na vibarua vidogo vidogo ambavyo alikuwa anavifanya wakati huo .
Fedha hizi aliamua kujilipia Karo ya chuo kikuu kwani aliamini kuwa ni kupitia elimu ambapo angefanikisha ndoto ya kuwa kiongozi, ila uamuzi huo uliweka uhusiano wake na mama yake mzazi pabaya.
Huku mama akiwa na maoni kuwa busara ingekuwa ajenge nyumba na pesa hizo Irene alikataa .
“Baadaye nilijiunga na chuo kikuu wakati mwanangu alikuwa na umri wa miaka miwili tu. Nilihudhuria masomo naye huko Nairobi , huku wanafunzi wakinishangaa na wengine kunisimanga ila nilijikaza”anasema Irene .
Akiwa chuo kikuu Irene alijitosa kwenye siasa za wanafunzi na upigaji picha - njia ambazo pia zilimuingizia mapato. Mwanadada huyu anasema kuwa aliweka historia kama naibu rais wa kwanza mwanamke wa Shirika la Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi (SONU).
Ni wakati huo pia ambao , alipata nguvu za kutetea haki za wanawake nchini Kenya , na kupata kazi kama mratibu wa mipango katika Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU).
Wakati wa uchaguzi wa 2017, tabia yake ya kujieleza waziwazi ilimfungulia mwanya mwingine kutambuliwa na aliye kuwa Rais kuongoza kampeni zake za vijana nchini Kenya. Kupitia hili, alikutana na watu wengi mashuhuri ambao walimfungulia milango zaidi katika ngazi za kimataifa
Kwa bahati mbaya, mwanadada huyu anasema kuwa alimpoteza mama mzazi katika ajali ya barabarani mwaka wa 2017. Ikiwa jambo moja kwa maisha yake lililompa huzuni, iliogeuka na kuwa sonana ambayo alipigana nayo kwa miaka mitatu na baadaye kutoka kwenye lindi hilo .

Chanzo cha picha, Irene Kendi
Kupitia hayo yote Irene Kendi aliandika kitabu cha simulizi ya maisha yake na changamoto nyingi ambazo alikumbana nazo
‘Carving of a firebrand’ kama njia ya kuhakikisha ulimwengu unafahamu umuhimu wa kuwa mstahimilivu hasa kwa vijana na kutokata tamaa maishani
Mwanadada huyu ambaye amekutana na watu mashuhuri duniani kupitia ukakamavu wake wa kutoa hotuba katika majukwaa ya kimatifa kuhusu nguvu za vijana anasema kuwa mafanikio sio tukio, ila ni safari .
Anaamini kuwa kila siku lazima mtu aongeze thamani hatua kwa hatua kwa ujuzi wake, maadili, kanuni, mitandao ya watu anaowafahamu na kimsingi zaidi ni kujijenga katika maisha.












