Afrika itakuwa mwenyeji wa Michezo ya Jumuiya ya Madola 'siku moja'

Afrika ina uwezo wa kuandaa Michezo yake ya kwanza kabisa ya Jumuiya ya Madola katika siku zijazo, kulingana na afisa mmoja anayehusika katika kuandaa tukio hilo la kila baada ya miaka minne.

Michezo ya mwaka huu -makala ya 22 - itaanza mjini Birmingham, Uingereza, siku ya Alhamisi, lakini awali ilipangwa kufanyika nchini Afrika Kusini.

Durban ilitajwa kuwa mwenyeji wa michezo hiyo kwa mwaka 2022 mnamo Septemba 2015 lakini ilibidi ajiuzulu mwezi Machi 2017 kwa sababu ya shida za kifedha.

Makamu wa rais wa kanda ya Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGF) Miriam Moyo ana imani kuwa Afrika ina uwezo wa kupiga hatua. "Hakika, Afrika itakuwa mwenyeji wa Michezo hii moja ya siku hizi," aliiambia BBC Sport Africa.

"Afrika Kusini ilijaribu kuwa mwenyeji lakini mambo hayakwenda sawa. Hiyo ndiyo ishara namba moja ya kuonesha kwamba Afrika ingetaka kuwa mwenyeji ninauhakika siku moja, labda Afrika Kusini inaweza kujitokeza."

Michezo hiyo, ambayo ilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Canada mwaka 1930, inashirikisha wanariadha kutoka nchi 72 - wengi wao wakiwa makoloni ya zamani ya Uingereza.

Hata hivyo, nchi nne za mwisho kujiunga na Jumuiya ya Madola - Rwanda, Msumbiji, Gabon, na Togo - hazina uhusiano wa kihistoria na Dola ya Uingereza.

Mataifa yote wanachama yamesaini vipengele vya maadili ikiwa ni pamoja na demokrasia, usawa wa kijinsia na amani na usalama wa kimataifa.

Kama bara lenye mataifa wanachama wa juu zaidi (21), Afrika haijawahi kuandaa michezo hiyo, na mji mkuu wa Nigeria wa Abuja ulitoa ombi ambalo halikufanikiwa la kuandaa Michezo ya 2014, ambayo ilifanyika Glasgow.

Kupunguza gharama na waandaaji wenza

Afrika iliwahi kuandaa michuano mikuu, huku Afrika Kusini ikiandaa Raga za wanaume na Kombe la Dunia la Fifa (mpira wa miguu) mnamo 1995 na 2010 mtawalia.

Hata hivyo, gharama ya kuandaa Michezo ya Jumuiya ya Madola ni sababu ya wazabuni wanaotarajiwa, huku bajeti ya jumla ya Birmingham 2022 ikitarajiwa kuwa £778m ($935m).

Tangu 2002, mji mkuu wa India Delhi ndio mji pekee nje ya Uingereza au Australia kuwakaribisha wanariadha kutoka Jumuiya ya Madola, huku tukio la 2026 likiwekwa kwa jimbo la Australia la Victoria.

Moyo, rais wa zamani wa Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki ya Zambia, alisema ni nchi chache tu za Afŕika ndizo zenye vifaa vya kuandaa Michezo hiyo - ambayo itashirikisha michezo 26 tofauti mjini Birmingham.

"Gharama zitakuwepo kila wakati. Hayo ni mambo ambayo yanajadiliwa na Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola, tunaweza kufanya nini kupunguza gharama," aliongeza.

"Kama; Afrika itawasilisha nini, tunaweza kutoa nini, nini kifanyike kwetu kuandaa michezo hii? Na nina uhakika, Afrika bila shaka itaikubali.

"CGF inaangalia maeneo haya yote kwa sababu, kama vyombo vingine vyote, tunatafuta kupunguza baadhi ya maeneo ambayo yanafanya michezo kuwa ghali. Unajua, kama kujenga vijiji (vya wanariadha) na mambo yote. Kuna mambo tunaweza kutumia kupunguza gharama hii na kuweza kuandaa Michezo."

Moyo, ambaye yuko katika bodi ya utendaji ya CGF, anapendekeza kuwa nchi mbili za Afrika zinaweza kuwasilisha zabuni ya pamoja ya kuandaa hafla hiyo katika siku zijazo.

"Kumekuwa na mijadala mingi ya uandaaji pamoja barani Afrika, ili mzigo usiwe tu kwa nchi moja kufanya matukio yote au taaluma, lakini kushiriki," alisema.

"Hili limejitokeza mara kadhaa kwenye mkutano wetu wa kanda, na ni jambo ambalo tunaliangalia kwa umakini. Na najua kwamba, kuzungumza kutoka kwa maoni ya bodi ya CGF, ni jambo ambalo hakika watalihimiza, na hii inaweza kusaidia Afrika kuingia kwenye meli.

"Nchi kama Nigeria na Botswana zina shauku kubwa ya kuandaa Michezo hii. Ziko tayari lakini kwa kuwa mwenyeji wa pamoja, ni bora kuwa na nchi karibu ambapo serikali zinaweza kukubaliana na kuendesha Michezo hii kwa wakati mmoja."

Afrika itakuwa ikituma timu kutoka mataifa 19 kwenda Birmingham, na bondia wa zamani wa Botswana Lechedzani Luza, mshindi wa medali ya fedha katika Michezo ya 2002 mjini Manchester, anaamini kuwa michezo hiyo inatoa jukwaa la ushindani kwa wanariadha wa bara hilo.

"Michezo ya Jumuiya ya Madola ni muhimu sana kwa wanariadha wa Afrika kwa maana hiyo ni fursa kwao kuonyesha vipaji vyao katika michezo tofauti," aliambia BBC Sport Africa.

"Labda Jumuiya ya Madola (Michezo) haina umuhimu sana, lakini najua nchi nyingi zinazotumia Jumuiya ya Madola kama kigezo cha Olimpiki, wanajua wakifanya vizuri katika michezo hii, bila shaka katika miaka miwili ijayo, watafanya vizuri sana.

"Kila mtu anataka kupata medali hiyo, ili kumaliza jukwaa. Kwa sababu inaweza kuwa wakati mzuri wa kazi, kupata medali katika Michezo ya Jumuiya ya Madola.

"Kila mtu anatazamia Michezo - msisimko na yote ambayo hujenga, na baada ya Covid kila mtu ana njaa ya mafanikio."

Aliyekuwa kocha mkuu wa Chama cha Ndondi cha Botswana (BOBA), Luza, kama Moyo, pia anatumai michezo hiyo hatimaye itaandaliwa barani Afrika.

"Tulifikiri kwamba Durban, Afrika Kusini, ingefaulu," aliongeza.

"Ni ndoto kwa kila mwanariadha kuwa na Michezo ya Jumuiya ya Madola kuja karibu na nyumbani, ambapo watu wako wanaweza kuja kukutazama na kuona kile unachofanya kila wakati kwenye michezo hii mikubwa.

"Kwa hivyo, siku moja, ninaamini katika maisha yetu, Mungu akiruhusu, tutaona Michezo hii barani Afrika. Na tutafurahi sana."