Je wajua desemba sio ya Krismasi pekee?

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Mwezi Disemba ukishika kasi tunajikuta tukikaribisha msimu wa sherehe, nyimbo za krismasi huanika kila pembe ulimwenguni, mapambo ya rangi na watu wakimiminika sokoni na madukani kununua mahanjumati ya Krismasi.

Lakini pilka pilka hizi za sherehe zikinoga, wengi hutafakari ni nini maana ya wakati huu wa mwaka kwa watu wa imani, dini na asili tofauti.

Mwezi Disemba ni muhimu sio tu kwa watu wanaosherehekea Krismasi tarehe 25, bali pia kwa watu wengi na tamaduni nyingine.

Mwezi wa mwisho wa mwaka huleta sherehe mbalimbali za kidini na kwa kuwa na ufahamu kuhusu sherehe hizi za Disemba, tunaweza kuongeza uelewa na kuthamini imani na tamaduni nyingine.

Hivyo basi, tutaangazia baadhi ya sherehe nyingi za Disemba kando na Krismasi!

Sherehe za Hanukkah kuanzia 18-26 disemba

Sherehe ya Kiyahudi inayokumbuka kurejeshwa kwa Yerusalemu na kuunguzwa tena kwa Hekalu la Pili mwanzoni mwa Uasi wa Makkabei dhidi ya Dola ya Seleusid katika karne ya pili KK.

Makkabei walifanikiwa kupigana dhidi ya Mfalme Antiochus IV Epiphanes.

Kulingana na Talmudi, Hekalu lilitakaswa na taa za menorah ziliungua kwa miujiza kwa siku nane, ingawa mafuta ya mafuta yaliyokuwa yanaweza kuwaka kwa siku moja pekee.

Sherehe zinazopamba siku hii ni kama vile:

  • Kuwasha mishumaa kila usiku.
  • Kuimba nyimbo maalum, kama Ma’oz Tzur.
  • Kusoma sala ya Hallel.
  • Kula vyakula vilivyopikwa kwa mafuta, kama latkes na sufganiyot, pamoja na vyakula vya maziwa.
  • Kucheza mchezo wa dreidel.
  • Kutolewa zawadi za fedha za Hanukkah (Hanukkah gelt).

Sherehe ya Kiyahudi ya Hanukkah inayodumu kwa siku nane inaanza tarehe 18 Desemba.

Sehemu kuu ya Sherehe hii ya Nuru za Kiyahudi ni kuwasha menorah yenye matawi tisa kila usiku.

(Taa ya tisa hutumika kuwasha nyingine.) Desturi hii inaashiria jinsi mafuta ya siku moja yalivyodumu kwa miujiza kwa siku nane wakati wa vita kati ya kundi dogo la Wayahudi na jeshi lenye nguvu la Kigiriki-Syria mnamo mwaka 165 KK.

Kulingana na desturi ya Kiyahudi, inasemekana walishinda na kurejesha Hekalu Takatifu la Yerusalemu.

Kwanzaa (Desemba 26 - Januari 1)

Sherehe ya Kwanzaa inayodumu kwa wiki moja inaheshimu urithi wa Waafrika-Amerika; ni sherehe ya kitamaduni, si ya kidini.

Karenga, mtaalamu wa taifa la Waafrika, alianzisha Kwanzaa mwaka 1966 kama njia ya kuunganisha jamii ya Waafrika-Amerika baada ya Uasi wa Watts katika jiji la Los Angeles.

Uasi huu ulianza baada ya afisa wa polisi kumkamata kijana mweusi kwa kosa la ulevi.

Uasi huo ulisababisha vifo 34, huku wengi wakiwa wamepigwa risasi na polisi au walinda amani, na majeruhi zaidi ya 1,000.

Karenga aliweka kanuni saba kuu za Kwanzaa: umoja; kujitegemea; uwajibikaji wa pamoja; uchumi wa ushirikiano; lengo; ubunifu; na imani. Jina la Kwanzaa linatoka katika methali ya Kiswahili “matunda ya kwanza,” inayomaanisha “matunda ya kwanza.”

Sherehe za Kwanzaa hutumia tamaduni za muziki na hadithi za Kiafrika.

Zarathosht Diso (Desemba 26)

Zoroastrianism, dini ya monotheistic iliyoanzishwa na Nabii Zoroaster zaidi ya miaka 3,000 iliyopita, ni moja ya dini za kale zaidi duniani. Waumini wa Zoroastrian heshimu kifo cha nabii wao siku hii kwa kutembelea hekalu la moto na kutoa sala.

Yule (Desemba 21 - Januari 1)

Wiccans na Neo-Pagans husherehekea solstisi ya majira ya baridi (siku ya giza zaidi ya mwaka, Desemba 21) kupitia sherehe ya Yule.

Solstisi ya majira ya baridi inasherehekea siku fupi zaidi na usiku mrefu zaidi wa mwaka; Yule inadhimisha kurudi kwa jua na kuanza kwa siku kuwa ndefu tena.

Sherehe hii ilianza kusherehekewa katika Skandinavia kama sherehe ya Kinnor.

Desturi maarufu ni kuteketeza mti wa Yule, ambao awali ulifanywa kusherehekea kurudi kwa jua.

Tangu wakati huo, desturi hii imeunganishwa na Krismasi.

Hata hivyo, Yule ilihusishwa na Krismasi katika karne ya 9, ingawa baadhi bado husherehekea Yule kama ilivyokuwa awali.

Los Posades, Latin

Los Posades ni jina la Kilatino, maana yake kuongeza maombi.

Sherehe hii huadhimishwa sana katika mataifa yaliyo na watu wa asili ya Kilatino: Mexico, Guatamala, Cuba, Uhispania na Amerika.

Sikukuu hii inayosherehekewa kati ya tarehe 16 na 24 huwa ukumbusho wa Maria mama yake Yesu Kristo. Watu huimba na kula pamoja kuonyesha upendo.

Sherehe ya Siku Tatu za Mfalme, Uhispania

Baada ya siku kumi na mbili za Krismasi, inakuja siku inayoitwa Epiphany au Siku Tatu za Mfalme inayoadhimishwa Uhispania.

Siku hii inasherehekewa baada ya watu ‘kuona Kristo’ na ‘kumpa zawadi’.

Watoto wengi hupewa zawadi jijini Peurto Rico.

Kabla ya mtoto kuenda kulala mnamo Januari 5, watu huacha kateni ya nyasi kitandani pake, kuashiria kuwa Mfalme atapata zawadi nono.

Madhehebu yasiyosherehekea Krismasi

Madhehebu mengine maarufu ni Waadventista Wasabato – wafuasi wake huabudu siku ya Jumamosi, siku ya Sabato ya Kiyahudi. Waadventista Wasabato hawaitambui Disemba 25 kama siku rasmi ya kusherehekea kuzaliwa Yesu.

Mashahidi wa Yehova Jehova Witness) ni mojawapo ya kundi kubwa la Wakristo ambao hawasherehekei Krismasi. Hapo zamani Mashahidi wa Yehova walikuwa wakisherehekea Krismasi hadi 1928, baada ya utafiti wao.

Waliacha kusherehekea Krisimas walipogundua inatokana na sherehe ya kipagani na Bibilia haijasema kuhusu kusherehekea kuzaliwa Yesu. Hata hivyo, hawawazuii wengine kuheshimu siku hiyo.