Vita Gaza: Geti 96, kivuko kipya ambapo misaada inatatizika kuingia

    • Author, Lucy Williamson
    • Nafasi, BBC

Geti namba 96 ni sehemu ya wazi kwenye uzio wa mpaka wa Gaza. Magari ya mizigo yanaongoza kuelekea jiji la Gaza , ili kuokoa maisha, katika giza nene la jioni.

Wakati Umoja wa Mataifa unaishutumu Israel kwa kutatiza uingizwaji wa misaada kimakusudi, Israel imefungua lango 96 - mojawapo ya njia mpya za misaada ambayo imeidhinisha.

Kando ya uzio wa mpaka, malori saba yakiwa yamepakia chakula cha msaada yamejipanga kusubiri kuvuka.

Kivuko hiki kipya kinawapeleka moja kwa moja katika maeneo ya kaskazini ya Gaza yenye hali ngumu, ili kuepusha safari ndefu, ngumu kupitia eneo la migogoro.

Onyo la Umoja wa Mataifa ni kwamba kaskazini mwa Gaza kumesalia wiki kadhaa kabla ya baa la njaa, shinikizo la kimataifa la kuongeza kiwango cha misaada linazidi kuongezeka.

Israel inasema imewezesha zaidi ya malori 350 ya misaada kuelekea kaskazini mwa Gaza katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita. Mashirika ya misaada yanasema eneo hilo kwa ujumla linahitaji malori 500 kwa siku.

"Kusuasua misaada kuingia hakusababishwi na IDF [Vikosi vya Ulinzi vya Israel]," Kanali Moshe Tetro, anaeshughulikia idhini ya misafara ya misaada kuingia anasema.

Pia unaweza kusoma

Aliiambia BBC, kazi ya jeshi ni "kuwezesha kuingia misaada ya kibinadamu Gaza" na misaada kutoingia kunatokana na uratibu wa mashirika ya misaada katika kuisambaza.

Amenyooshea kidole malori yanayosubiri kuvuka, akisema ushahidi uko mbele yetu. Malori 20 yalikuwa yameidhinishwa kuvuka usiku huo, alisema, lakini saba pekee ndiyo yalijitokeza.

"Tumechukua hatua nyingi kuongeza kiwango cha misaada ya kibinadamu," anasema.

"Lakini Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa yana changamoto kuhusu kiasi cha malori, kiasi cha madereva wa lori, wafanyakazi, saa za kazi..."

Matthew Hollingworth, mkurugenzi wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), alikuwa kwenye moja ya lori lililokuwa limesimama kwenye uzio wa mpaka usiku huo. Aliambia BBC kuna sababu maalumu kwa nini WFP haikuweza kupeleka magari yote 20.

"Kwenye msafara huu, tulipewa kikomo cha madereva 15 waliohakikiwa na IDF ambao waliruhusiwa kutumia njia hii, lakini ni saba tu ndio tuliowapata", alisema.

Baadhi ya madereva walioidhinishwa walikuwa wamekwenda katika Jiji la Gaza siku iliyotangulia, na walikuwa wamekwama huko, alisema. Hata kuendesha lori tupu kurudi Gaza kunahitaji idhini ya jeshi la Israel.

"Tunahitaji madereva wa malori 50, 60, 70, 80 kutumia njia hizi kila siku," alisema. "Tunahitaji maeneo zaidi ya kuingia kaskazini mwa Gaza na katika jiji la Gaza, na tunahitaji idhini ya mapema ili tuweze kuendesha misafara mingi kila siku."

Israel ina nia ya kuuonyesha ulimwengu kuwa inaruhusu misaada zaidi kuingia Gaza - lakini inasema haihusiki na kiasi cha misaada inayoingia, au uwezo wa mashirika kusambaza misaada.

Sheria ya kimataifa inasema tofauti; Israel ina wajibu, si tu kufungua milango, lakini kutumia njia zote zinazowezekana kupeleka chakula na dawa kwa watu walio chini ya udhibiti wake.

Kanali Tetro ananiambia hakuna uhaba wa chakula huko Gaza, na kama Hamas wanataka kubadilisha hali ya huko, wanapaswa kumaliza vita.

Alipoulizwa juu ya maonyo ya baa la njaa, na picha za watoto walio na utapiamlo katika hospitali za Gaza, alirudia maneno yale yale, tena na tena.

"Hakuna njaa Gaza," alisema. "Hakuna uhaba wa chakula."

Siku ya Jumapili, shirika kuu la misaada la Gaza, Unrwa, lilisema Israel imepiga marufuku kupeleka chakula zaidi kaskazini mwa Gaza.

Israel inasema shirika hilo lina uhusiano na Hamas, na itaendelea tu kufanya kazi na mashirika ambayo "hayahusiki na ugaidi."

Mkurugenzi wa Unrwa, Philippe Lazzarini, alisema marufuku hiyo inasikitisha na kuishutumu Israel kwa kuzuia misaada kimakusudi.

Shirika hilo hivi karibuni lilijaribu kuanzisha tena misafara baada ya kusimama kwa miezi miwili, baada ya lori lake moja kushambuliwa na kombora mwezi Januari.

Katika lango namba 96, magari ya jeshi yanapiga kelele kuzunguka msafara huo, kabla ya kivuko kufunguliwa na lori kuondoka wakati wa usiku.