Kwa nini kesi ya Lissu inavutia macho ya kimataifa?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Kesi ya uhaini na ya kuchapisha taarifa za uongo - zinazomkabili mwanasiasa wa Tanzania, kutoka chama kikuu cha upinzani Chadema, Tundu Lissu, ambazo zimesikilizwa katika mahakama jijini Dar es Salaam siku ya jana, zimegonga vichwa habari kitaifa na kimataifa.

Uhaini ni kesi ambayo ukipatikana na hatia hukumu yake inaweza kuhusisha kunyongwa hadi kufa, na kesi ya kuchapisha taarifa za uongo, inaweza kukuingiza katika faini au kufungwa gerezani si chini ya miaka mitatu ama yote mawili.

Hivi karibuni Tundu Lissu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema, akirithi nafasi hiyo kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa muda mrefu Freeman Mbowe. Miongoni mwa nyadhifa nyingine, Lissu amepata kuwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chadema, Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Rais wa chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), kazi ambazo zimelea na kukuza jina lake katika siasa za Tanzania.

Wanaharakati kutoka nchi jirani ya Kenya wamefanya juhudi zao kuingia Tanzania, kuonyesha uungaji mkono kwa Lissu. Fauka ya hilo, Bunge la Umoja wa Ulaya limekaa kikao wiki mbili zilizopita kujadili kesi ya Lissu. Haya ni mambo ambayo yanaonesha kesi zake zimevutia watu hadi nje ya mipaka ya Tanzania. Je, kwa nini?

Pia unaweza kusoma

Wanaharakati wa Kenya

Wanaharakati kadhaa wa Kenya wamezuiliwa kuingia nchini Tanzania; alianza Wakili wa Kenya na aliyekuwa Waziri wa Sheria na Masuala ya Kikatiba wa nchi hiyo Martha Karua na wenzake wawili ambao walirudishwa Kenya baada ya kuzuiliwa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Wengine waliorudishwa ni aliyekuwa Jaji Mkuu wa Kenya, Willy Mutunga na wanaharakati Hussein Khalid na Hanifa Farsafi, ambao wote waliingia nchini Tanzania kwa ajili ya kufuatilia kesi ya Tundu Lissu.

Vyombo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa, mwanaharakati Boniface Mwangi kutoka Kenya na Mwanasheria Agather Atuhaire kutoka Uganda wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Tanzania, kwa mujibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Serikali ya Kenya imesema kuzuiliwa na kufukuzwa kwa raia wake nchini Tanzania hakutaathiri uhusiano wa nchi hizo mbili. Msemaji wa Serikali ya nchi hiyo, Isaac Mwaura amesema, “sidhani kama kuna mzozo wowote wa kidiplomasia kati ya Kenya na Tanzania. Kila nchi ina njia yake ya kushughulikia mambo yake.”

Kukazia msimamo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema, "tumeanza kuona mtiririko au mwenedo wa wanaharakati wa kanda hii, kuanza kuingilia mambo yetu huku, sasa kama kwao wameshadhibitiwa wasije kwetu huku, tusitoe nafasi.”

Nimemuuliza Mtafiti katika Taasisi ya Mafunzo ya Uslalama (ISS) nchini Kenya, Dr. Nicodemus Minde, kuhusu kipi kinachowasukuma wanaharakati wa Kenya kumiminika Tanzania, kufuatilia kesi hii:

“Ni kwa lengo la kujenga mshikamano, kama walivyokwenda nchini Uganda kusikiliza kesi ya Kizza Besigye," amesema Dr. Minde, na kuongeza kuwa, "kuna taarifa kwamba wanataka kutengeneza mshikamano katika nchi za Afrika Mashariki na Kati, ukizingatia nchi hizi zinapitia wakati mgumu kwenye suala zima la demokrasia.”

Bunge la Ulaya

Wiki mbili zilizopita Bunge la Ulaya limelaani hatua ya kukamatwa Tundu Lissu na kueleza wasiwasi kuhusu kesi ya uhaini dhidi yake ambayo ina hukumu kifo. Bunge hilo pia, limeitaka Tanzania kurejesha ushiriki kamili wa Chadema katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, kufanya mazungumzo na vyama vyote vya siasa kuhusu mageuzi ya uchaguzi, kuheshimu haki za vyama vya siasa na kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki.

Kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Tanzania ilijibu kwa kueleza kuwa imesikitishwa na azimio la Bunge la Umoja wa Ulaya na kusema uamuzi uliofikiwa na Bunge hilo ni kutokana na taarifa zisizo kamili au za upande mmoja bila kuwasiliana na Serikali kwa njia za kidiplomasia.

Lakini hiyo si mara ya kwanza kwa Tanzania kujadiliwa katika Bunge la Ulaya, juu ya mwenendo wa siasa zake: Disemba 2018 Bunge hilo, lilitoa kauli ya kukosoa hali ya kisiasa nchini Tanzania kutokana na kile ilichokiita ni ukandamizaji wa uhuru wa wananchi kupitia sheria kali dhidi ya asasi za kiraia, watetezi wa haki za binadamu, vyombo vya habari na vyama vya siasa.

Umaarufu wa Tundu Lissu nje ya mipaka ya Tanzania, ulizidi kuongezeka baada ya kunusurika shambulio la mauaji Septemba 2017. Watu wasiojuulikana walimshambulia akiwa katika gari lake katika jiji la Dodoma na kumpiga dazeni ya risasi katika mwili wake.

Katika juhudi za kuokoa maisha yake, matibabu yake ya kwanza yalianzia nchini Tanzania, kisha Nairobi, Kenya na baada ya hapo akasafiri kwenda kuishi uhamishoni Ulaya katika nchi ya Ubelgiji ambako pia aliendelea na matibabu.

Katika nyakati hizo na wakati wa kushiriki uchaguzi Mkuu wa 2020 kama mgombea wa urais wa Chadema, jina lake lilizidi kuvuma nje ya Tanzania – hivyo haishangazi kusikia sauti kutoka Kenya na Ulaya zikiwa mstari wa mbele kuzungumzia kesi yake.