Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Vita vya Ukraine: Kwa nini ni muhimu kuudhibiti mji wa Kherson?
Vikosi vya Ukraine hatimaye vimeuteka mji wa Kherson, baada ya vikosi vya Urusi Kuondoka siku ya Alhamisi.
Pande zote mbili zinaona mji huo, kusini mwa nchi, ni muhimu kuudhibiti. Hata hivyo, wataalam wa kijeshi wanasema vita kwa ajili yake vinaweza kuwa ghali sana.
Kherson iko wapi na kwa nini eneo hili ni muhimu?
Kabla ya vita, Kherson ilikuwa na idadi ya watu wapatao 380,000. Iko kwenye ukingo wa mto Dnipro, karibu na pwani ya Bahari Nyeusi. Pia iko karibu na peninsula ya Crimea - sehemu ya Ukraine ambayo Urusi iliiteka mwaka 2014 na ambayo ina kambi zake kadhaa za kijeshi.
"Kherson ni lango la Crimea," anasema Marina Miron, mtafiti katika masomo ya ulinzi katika Chuo cha Kings London. "Kuidhibiti tena kungefungua njia ya kuitwaa tena Crimea, ambayo Ukraine inalenga kufanya hivyo katika vita hivi."
Mahali iliipo Kherson pia ni muhimu, anasema Forbes Mackenzie, afisa wa zamani wa ujasusi wa Jeshi la Uingereza na mtendaji mkuu wa Huduma za Ujasusi za Mackenzie. "Kupata udhibiti wa mto Dnipro ni muhimu kwa sababu unapita katikati mwa Ukraine," anasema.
Umuhimu wa Kherson ni upi hasa?
Vikosi vya Ukraine vimeshambulia madaraja katika eneo la Dnipro kwa makombora, ili kujaribu kukata njia za usambazaji za Urusi kuelekea mji huo kutoka mashariki na kusini.
Vikosi vyake pia vimekuwa vikisonga mbele polepole kwenye mji huo kutoka kaskazini magharibi na kaskazini mashariki.
"Lengo kuu linalofuata la Ukraine ni mji wa Beryslav," anasema Bi Miron. "Mara tu wanapouchukua mji huo, basi wanaweza kushambulia Kherson yenyewe. Inaweza kuwa ni suala la wiki chache tu."
Hata hivyo, Ben Barry, Mshirika Mwandamizi wa Vita vya Ardhi katika Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati, anasema vikosi vya Ukraine vimekuwa vikipiga hatua polepole kuelekea mji wa Kherson.
"Bado wanapaswa kuzuia vikosi vya mstari wa mbele vya Urusi kaskazini mwa Kherson," anasema. "Wanaweza kupunguzwa kasi kutokana na ardhi ya eneo hilo lenye matope. Huenda wasiweze kupenya ili kufika mjini."
Je, Urusi inajiondoa kutoka Kherson?
Urusi imewahamisha raia 70,000 kutoka mji huo, mbali na wanajeshi wake
Naibu msimamizi wa kiraia aliyewekwa na Urusi katika eneo la Kherson, Kirill Stremousov, alisema vikosi vya Urusi vitaondoka kurudi sehemu za Kherson upande wa magharibi wa Dnipro. "Uwezekano mkubwa wa vikosi vyetu, askari wetu, wataondoka kuelekea mashariki," alisema.
Hata hivyo, jeshi la Ukraine limesema mazungumzo ya Urusi ya kusema itawaondoa wanajeshi wake yanaweza kuwa ni ujanja. Mackenzie Intelligence inakadiria kuwa Urusi ina wanajeshi kati ya 5,000 na 10,000 wanaoulinda mji huo.
Taasisi ya Uchunguzi wa masuala ya Vita inasema kuwa wanajiandaa kwa ulinzi zaidi ndani ya Kherson na kaskazini magharibi mwa mji huo. "Kuna taarifa zinazokinzana," anasema Ben Barry.
"Urusi inawaondoa wasimamizi wake, lakini wakati huo huo imekuwa ikiwaweka askari wa miamvuli na wanajeshi wa majini."
Vita vya Kherson vinaweza kuwa na gharama gani?
Shambulio la kuikomboa tena Kherson linagharimu sana vikosi vya Ukraine, linasema Forbes Mackenzie. "Mapigano yanaweza kuwa ya nyumba kwa nyumba na kiwango cha majeruhi kinaweza kuwa kikubwa sana," anasema.
"Kwa mtazao itakuwa ya kutisha."
Hata hivyo, vita kwa ajili ya jiji hilo haviepukiki, anasema Ben Barry. "Kila upande una uchaguzi," anasema. "Vikosi vya Urusi vinaweza kupigana ili kuwachelewesha Waukraine na kisha kuondoka. Waukraine wanaweza kujaribu kuzunguka mji na kukata njia za usambazaji badala ya kuingia.
"Ni ngumu kukisia mikakati yao."