Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Maisha yalivyo baada ya kufungwa kimakosa gerezani kwa miaka 48
- Author, Madeline Halpert
- Nafasi, BBC News New York
Glynn Simmons alitazama nje ya dirisha kwa muda mrefu, alipoketi kwenye upande wa abiria katika gari ambalo rafiki yake alikuwa akiliendesha, wawili hao wakiwa kwenye barabara kuu ya kuelekea mji wa Tulsa katika jimbo la Okahoma. Macho yake yalikuwa yanalenga anga iliyojaa mwanga wa nyota katika usiku huo.
Ilikuwa hali ambayo mwanamume huyo mwenye umri wa miaka 70 alikuwa hajashuhudia kwa takriban nuzu ya karne, kwani alikuwa gerezani akihudumu kifungo cha Maisha kwa kosa la mauaji ambalo hakulitekeza.
‘'Ni vitu kama hivi…kutazama misimu ikibadilika, majani ikiwa ardhini, mambo ya kawaida ambayo singeweza kuyafanya nikiwa gerezani. Hungeweza kuifurahia, hungeweza kuitizama, Simmons aliliambia BBC. ‘ Ni jambo la kusisimua sana.’'
Bwana Simmons aliachiliwa huru kutoka gerezani mwezi Julai mwaka jana {2023}. Mwezi Desemba, alipatikana bila hatia na kutangazwa asiyekuwa na makosa kwenye kesi ya mauaji ya Carolyn Sue Rogers iliyofanyika 1974.
Hukumu yake ambayo ilikuwa ya makosa, ndio iliyochukuwa muda mrefu zaidi katika historia ya taifa la Marekani.
Hukumu dhidi yake ilifutiliwa mbali, baada ya mahakama ya wilaya {jimbo} kupata ushahidi kwamba waendesha mashtaka kwenye kesi hiyo hawakuwa wamewasilisha ushahidi wote kwa mawakili wa upande wa utetezi, ikiwemo taarifa muhimu kwamba mmoj awa mashahidi alikuwa amewatambua washukiwa wengine.
Simmons alikuwa na umri wa miaka 22, wakati yeye na mshtakiwa mwenza Don Roberts walishtakiwa na kupewa adhabu ya hukumu ya kifo mnamo 1975, adhabu ambayo baadaye ilibadilishwa na kuwa kifungo cha maisha gerezani.
Simmons, alizungumza na BBC, wiki hii kuhusu maisha mapya akiwa huru, changamoto ya kiafya anayokabiliana nayo ya saratani iliyo katika kiwango cha nne, na imani na matumaini ambayo ilikuwa kiungo muhimu maishani mwake katika miaka 48 aliyokuwa gerezani.
'‘Ukiwa msafi bila hatia, imani hukupa nguvu ya kuendelea na maisha,’alisema.
‘Nitakuwa ninakudanganya nikisema kwamba sikuwahi kupoteza imani.. nilikumbana na hali hiyo kwa mara nyingi sana. Lakini kama ukanda wa mpira – una nyooshwa kisha unarudi hali ya kawaida,’
Ukosefu wa makusudi wa kuzingatia haki
Mnamo Januari 1995, Simmons alikuwa miongoni mwa watu kadhaa waliokamatwa katika eneo ambapo sherehe ilikuwa inafanyika.
Walikabiliwa na shtaka tofauti ambalo kulingana naye lilikuwa hafifu na lilikuwa la ‘wizi’, alisema.
Alifikishwa katika kituo cha polisi, ambapo maafisa wa polisi walimtaka kushiriki kwenye orodha ya utambulizi ya washukiwa kwenye kesi ya mauaji ya Rogers iliyofanyika mwezi mmoja kabla ya kukamatwa kwake.
Mauaji hayo yalifanyika kwenye duka la kuuza pombe katika mtaa mmoja ulio pembizoni mwa mji wa Oklahoma.
Mauaji ya Rogers – ambaye alikuwa akihudumu kwenye duka moja alipopigwa risasi kichwani – hadi sasa halijaweza kukamilika uchunguzi wake na mwenye kutekeleza mauaji hayo kukamatwa na kushtakiwa.
‘Nilikuwa tu ndio nimetimiza umri wa miaka 21. Sikuwahi kujipata tena katika hali ya makosa kisheria, na wala kuhusika pakubwa na idara ya haki,’ alisema Simmons. ‘Sikujuwa kwamba nilikuwa na haki ya kuwakilishwa na wakili, haki ya kukataa chochote. Sikuwa na ufahamu wowote.’
Glynn Simmons anataka kupigania mabadiliko kwenye mfumo wa haki.
Mteja ambaye pia alipigwa risasi kichwani kwenye tukio la mauaji ya Rogers, aliombwa kuangalia orodha ya utambulizi wa washukiwa na kuona ikiwa angemtambua aliyetekeleza uhalifu huo, siku chache baada ya kuondoka hospitalini, alisema Simmons.
Mwanamke huyo hakumtambua Simmons, alisema Simmons. Badala yake, aliwalenga washukiwa wengine watatu kwenye foleni hiyo, kulingana na wakili wa Simmons , Joe Norwood.
Hata hivyo, Simmons ambaye -kwa wakati huo wa mauaji alisema alikuwa mjini Louisiana- alishtakiwa, kupatikana na hatia na kuhukumiwa kifo.
‘Sitoitambua kama hukumu ya kimakosa au upotoshaji wa haki. Haikuwa makosa. Ilikuwa jambo la makusudi, ‘ alisema Simmons. ‘Ilikuwa hali ya kukusudia iliyokosa kuzingatia haki na sheria.’
Imetafsiriwa na Leillah Mohammed na kuhaririwa na Ambia Hirsi