Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Juhudi za usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas zaendelea Saudia
Juhudi za kufikiwa usitishaji mapigano kati ya Israel na Hamas ambao unaweza kuchelewesha mashambulizi ya Israel huko Rafah kusini mwa Gaza zinaendelea.
Saudi Arabia siku ya Jumapili ilitoa wito wa "utulivu" wa kikanda huku ikionya juu ya athari za vita vinavyoendelea kati ya Israel na Hamas kwa uchumi wa dunia.
Mkutano maalumu wa siku mbili wa Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF) unafanyika mjini Riyadh, ambao pia unajumuisha wapatanishi wanaofanya mazungumzo ya kumaliza mzozo wa Gaza.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken, ambaye alisafiri kwa ndege kuelekea Saudi Arabia kwa awamu inayofuata ya mazungumzo na viongozi wa nchi za Kiarabu, pia anashiriki katika mkutano huo.
Wizara ya Mambo ya Nje ilisema itasisitiza haja ya kuzuia mzozo huo kuenea.
Pia walioalikwa ni viongozi wa Palestina na maafisa wakuu kutoka nchi nyingine wanaojaribu kusuluhisha usitishaji vita kati ya Israel na Hamas.
Vita huko Gaza, pamoja na mizozo ya Ukraine na kwingineko, vinaweka "shinikizo kubwa" kwa "hisia za kiuchumi," Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia Mohammed al-Jadaan alisema katika moja ya mijadala ya kwanza ya kongamano hilo.
"Nadhani nchi, viongozi na wengine wanapaswa kutawala na kuhakikisha kuwa hali inapungua," Jadaan alisema. "ukanda unahitaji utulivu."
"Ulimwengu wa leo unapita katika njia ngumu, ukijaribu kupata uwiano kati ya usalama na ustawi," Waziri wa Mipango wa Saudi Faisal al-Ibrahim alisema katika mkutano na waandishi wa habari Jumamosi.
"Tunakutana wakati ambapo uamuzi mmoja usiofaa, hesabu moja mbaya au kutokuelewana kutafanya matatizo yetu kuwa mabaya zaidi."
Rais wa WEF Borge Brende alisema katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Jumamosi kwamba "kuna kasi mpya katika mazungumzo ya mateka, na vile vile ... njia inayowezekana ya kutoka kwenye mzozo ambao tunajikuta huko Gaza."
Hata hivyo, Israel haitashiriki katika mkutano huo, na Brende alibainisha kuwa upatanishi unaohusisha Qatar na Misri haujajadiliwa rasmi katika mkutano huo.
Bila shaka, hali ya kibinadamu huko Gaza itajadiliwa, pamoja na Iran inayounga mkono Hamas na kundi la Lebanon la Hezbollah, aliongeza.
Siku ya Jumamosi, Hamas ilitoa video ya mateka wawili kuonesha kuwa bado walikuwa hai, na kulikuwa na maandamano makubwa nchini Israel kudai makubaliano.
Siku ya Jumamosi, Hamas ilisema inachunguza pendekezo la hivi punde la Israel la kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, na Jumapili msemaji wa kundi hilo, ambaye aliomba kutotajwa jina, aliiambia Reuters kwamba ujumbe wa Hamas utawasili Cairo siku ya Jumatatu kujadili mapendekezo ya hivi karibuni.
Siku moja kabla, ripoti za vyombo vya habari zilisema kuwa wajumbe wa Misri walikuwa wamewasili Israel katika jaribio la kufufua mazungumzo yaliyokwama.
Shambulio dhidi ya Rafah
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas alisema ni Marekani pekee inayoweza kuizuia Israel kushambulia Rafah, akiongeza kuwa anatazamia shambulio katika siku zijazo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Israel Katz alisema mashambulizi yaliyopangwa kufanyika katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah yanaweza kusitishwa ikiwa Hamas itakubali kuwaachilia mateka ambao bado wanawashikilia.
Jeshi la Israel lilisema mapema wiki hii kwamba kama IDF itaanzisha uvamizi katika mji wa Rafah, ambapo takribani Wapalestina milioni moja waliokimbia makazi yao wanajihifadhi, "eneo la kibinadamu" katika pwani litapanuliwa ili kuchukua raia zaidi.
Kauli hiyo iliibua hofu kwamba shambulio dhidi ya Rafah, hitaji ambalo Israel imekuwa ikilizungumzia kwa miezi kadhaa, linaweza kuanza katika siku za usoni, licha ya shinikizo kutoka kwa jumuiya ya kimataifa.
Israel inasema lazima isonge mbele hadi Rafah, kando ya mpaka wa Gaza na Misri, ili kupunguza tishio la kijeshi linaloletwa na Hamas.
Wanajeshi wa Israel wanadai kuwa ni lazima wawaondoe wanamgambo waliosalia kwa sasa Rafah.
Mbali na kuwaua wanamgambo wa Hamas na viongozi wakuu wa kijeshi, Waisrael wanataka kuwapata mateka 129 ambao kundi hilo limewashikilia tangu shambulio la Oktoba 7, wengi wao wanaaminika kuwa huko Rafah.
Utawala wa Biden umeitaka Israel mara kadhaa kujiepusha na operesheni kubwa ya kijeshi huko Rafah.
"Rais Biden amekuwa wazi sana: Hatuwezi kuunga mkono operesheni kubwa ya kijeshi huko Rafah," Antony Blinken alisema wiki iliyopita.
Hatua kama hiyo, alisema, "itakuwa na matokeo mabaya" kwa raia waliosalia katika jiji hilo, na Israel, kwa maoni yake, inaweza kufikia malengo yake ya kijeshi kupitia njia nyingine.
Sehemu kubwa ya misaada inaingia Ukanda wa Gaza kupitia vituo viwili vya ukaguzi katika eneo la Rafah. Pia ni mahali ambapo mashirika ya Umoja wa Mataifa na makundi mengine ya misaada yanapatikana kwa sasa, pamoja na hospitali na zahanati nyingi zinazofanya kazi.
Ukatishaji wowote wa vifaa vya msaada, haswa chakula, unaweza kuwa na matokeo mabaya. Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa ya kibinadamu yanaonya kwamba njaa iko karibu kuikumba Gaza.
Israel ilianzisha mashambulizi huko Gaza kufuatia shambulio la Oktoba 7 la Hamas kusini mwa Israel ambalo, kulingana na takwimu za Israel, liliua watu 1,200 na kuwateka watu 253.
Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 34,000 wamekufa na idadi kubwa ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao, kulingana na wizara ya afya ya Gaza inayodhibitiwa na Hamas.