Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mfahamu Jenerali Aharon Haliva, ambaye alijiuzulu baada ya kushindwa kuilinda Israel kutokana na shambulio la Oktoba 7
Jeshi la Israeli limetangaza kujiuzulu kwa mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Kijeshi baada ya kukiri kushindwa kuzuia shambulio la Hamas kusini mwa Israeli mnamo Oktoba 7.
Jeshi la Israel lilisema katika taarifa kwamba Jenerali Aharon Haliva atastaafu "mara tu mrithi wake atakapoteuliwa kwa utaratibu uliopangwa na wa kitaalamu."
Jenerali Halifa aliyejiuzulu, ametumikia jeshi kwa miaka 38, ni afisa wa kwanza wa ngazi ya juu kujiuzulu wadhifa wake kwa kushindwa kuzuia shambulio lililoanzishwa na Hamas.
Katika barua yake ya kujiuzulu, ambayo ilisambazwa kwa vyombo vya habari, jenerali huyo alithibitisha kwamba anawajibikia kushindwa kuzuia shambulio ambalo halijawahi kutokea dhidi ya Israel.
Barua ya Haliva ilisema: "Siku ya Jumamosi, Oktoba 7, Hamas ilianzisha shambulio baya la kushtukiza dhidi ya taifa la Israel... Idara ya upelelezi chini ya uongozi wangu haikutimiza majukumu tuliyokabidhiwa.
Haliva aliongeza: "Nimeibeba siku hiyo nyeusi tangu wakati huo. Kila mchana na usiku, nitabeba pamoja nami milele maumivu makali ya vita."
Jenerali Aharon Haliva alitoa wito wa "uchunguzi wa kina kuhusu mambo na mazingira" yaliyoruhusu shambulio hilo kutokea.
Aharon Haliva ni nani?
Haliva alizaliwa mnamo 1967 huko Haifa kwa wazazi wa asili ya Morocco na alijiunga na jeshi la Israeli mnamo 1985.
Alipata shahada ya kwanza katika sayansi ya kijamii kutoka Chuo Kikuu cha Bar-Ilan na shahada ya uzamili katika fani hiyo hiyo kutoka Chuo Kikuu cha Haifa.
Hapo awali alijitolea kama askari wa miavuli katika Brigedia ya Jeshi la Israeli, kisha akawa afisa wa mwanajeshi wa kupigana vitani. Alipigana kama kiongozi wa kikosi katika Kikosi cha 202 cha miavuli katika Operesheni ya Law and Order kusini mwa Lebanon mnamo 1988.
Kabla ya kuwa Mkuu wa Ujasusi wa Kijeshi, Haliva aliwahi kuwa Mkuu wa Kurugenzi ya Operesheni, Mkuu wa Kurugenzi ya Teknolojia na Usafiri, Mkuu wa Sehemu ya Operesheni Kurugenzi ya Operesheni, Kamanda wa Kitengo cha 98 cha Miavuli, Kamanda wa Brigedia ya Miavuli na Kamanda wa Shule ya IDF.
Mnamo Novemba 2017, alipiga marufuku masomo ya Torah ambayo yalifanyika nje ya kambi ya Ariel Sharon, hatua ambayo ilizua maandamano kutoka kwa mamia ya wanajeshi waliotafuta msaada kutoka kwa Mkuu wa Majeshi, Gadi Eisenkot.
Mnamo Oktoba 2021, aliteuliwa kuwa mkuu wa Idara ya Ujasusi wa Kijeshi.
Katika msimamo wake mpya, alizingatia kwamba Mkataba wa Abraham "unatokana na hitaji la wakaazi wa nchi za Mashariki ya Kati kuboresha kiwango chao cha maisha na kukabiliana na shida ya hali ya hewa."
Mnamo Oktoba 7, alikuwa likizoni huko Eilat. Ripoti zilisema alifahamishwa takriban saa 3 asubuhi siku hiyo kuhusu "ishara fulani kutoka Gaza" kuhusu shambulio lililokaribia, lakini ripoti zilisema hakushiriki katika mashauriano katika ngazi za juu za IDF kuhusu viashiria hivyo na hakupatikana kwa njia ya simu.
Baadaye Haliva alinukuliwa akiwaambia waliokuwa karibu yake kwamba hata kama angeshiriki katika mashauriano hayo, angehitimisha kuwa Hamas wanaonekana kufanya mafunzo na kwamba kushughulikia suala hilo lingeweza kusubiri hadi asubuhi. "Isingebadilisha matokeo ya mwisho kwa njia yoyote," alisema.
Mnamo Oktoba 17, aliandika barua kwa askari wake ambapo alisema: "Tumeshindwa katika kazi yetu muhimu zaidi, na kama mkuu wa Kurugenzi ya Ujasusi ya Israeli, ninawajibika kikamilifu kwa kushindwa."
Pia katika mwezi huo huo, alisema: "Katika ziara zangu zote kwenye vitengo vya Kurugenzi ya Ujasusi wa Kijeshi katika siku 11 zilizopita, niliketi na kusisitiza kwamba mwanzo wa vita ulikuwa kushindwa kwa ujasusi," akiongeza kuwa Idara ya Ujasusi ya Kijeshi, Kurugenzi, chini ya uongozi wake, "ilishindwa kuonya juu ya shambulio la kigaidi."
Kwa sasa anashiriki katika uchunguzi wa ndani wa jeshi kuhusu kushindwa kwake katika kipindi cha kabla ya shambulio la Oktoba 7.
Uchunguzi umepangwa kuwasilishwa kwa Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Israeli, Jenerali Herzi Halevy, mwanzoni mwa mwezi Juni.
Kulingana na ripoti ya kituo cha Channel 12 cha Israeli mnamo Desemba, Kurugenzi ya Ujasusi ya Kijeshi ya Israeli ilifanya majadiliano miezi mitatu kabla ya shambulio hilo, ambapo afisa - aliyetambuliwa tu kwa cheo chake na herufi ya kwanza ya jina lake, Brigedia Jenerali Bey - alihitimisha: "Tulijaribu lakini hatukuweza.” Hatuwezi kusema ni vipi (kiongozi wa Hamas huko Gaza Yahya Sinwar) atachukua hatua, na kwa hivyo makamanda kwenye uwanja lazima wachukue tahadhari zinazohitajika."
Alisema matokeo ya mjadala huo yalitolewa kwa Haliva ambaye aliamuru kuongezwa kwa uchunguzi wa kiintelijensia na kuongeza kuwa hilo tayari limefanyika.