Pakistan: Bushra Bibi, mke 'mcha Mungu' wa Imran Khan ni nani?

Chanzo cha picha, Reuters
Na Flora Drury
BBC News
Uvumi kuhusu mke wa tatu wa Imran Khan haukuchukua muda kuanza kuvuma.
Kwa mwanzo, Bushra Maneka - kama alivyojulikana kabla ya ndoa yake na nahodha wa zamani wa kriketi aliyegeuka kuwa mwanasiasa - ilikuwa tofauti kabisa na watangulizi wake wawili wazuri. Wakati sosholaiti Mwingereza Jemima Goldsmith na mwanahabari Reham Khan walipamba kurasa za majarida na skrini za televisheni, alijificha nyuma ya pazia.
Kwa kweli, Khan angeambia Mail on Sunday kwa fahari mnamo 2018 kwamba "hakuona sura ya mke wangu hadi baada ya kufunga ndoa" - kitu ambacho alisema "kisingekuwa sawa" miaka ya 1980, enzi yake ya maisha ya shamra shamra nyingi za klabu za usiku ya London.
Alisema, ni akili na tabia ya Bushra ndiyo iliyomvuta kwake. Lakini hiyo haikuwa kweli iliyofanya watu kuzungumza - ilikuwa, badala yake, nguvu za kiajabu alizopewa sifa.
Mwanamke ambaye sasa anajulikana kama Bushra Bibi alikuwa, kwa kweli, mponyaji wa imani na wafuasi wachache ambao walimheshimu kama mshauri wa kiroho.
Siku ya Jumatano wanandoa hao wote walihukumiwa kifungo jela na kutozwa faini ya zaidi ya $2m kila mmoja katika kesi ya ufisadi - habari ambazo ziliwafanya wasomaji kote ulimwenguni kutafuta jina lake kujua zaidi kumhusu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wengine wanasema Bushra Bibi anashikamana na mila ya Sufi, lakini hilo linapingwa na wengine. Mara nyingi hufafanuliwa kama mafumbo ya Kiislamu, Usufi - ambao mumewe anasema amekuwa akiupenda kwa zaidi ya miongo mitatu - unasisitiza utafutaji wa ndani wa Mungu na kukataa mambo ya kidunia.
Ni mbali sana na miaka yake ya kucheza kriketi alipositawisha sifa kama mvulana wa kupenda raha kabla ya kutulia kwenye ndoa ya jamii ambayo haikuwa mbali na kujulikana.
Mnamo 1995, akiwa na umri wa miaka 43, alimuoa mrithi wa Uingereza mwenye umri wa miaka 21, Jemima Goldsmith - binti wa mmoja wa watu matajiri zaidi duniani wakati huo. Ndoa hiyo ilidumu miaka tisa na ikazaa wana wawili.
Ndoa ya pili mnamo 2015, na mwandishi wa habari na mtangazaji wa zamani wa hali ya hewa wa BBC Reham Khan, ilidumu chini ya mwaka mmoja. Anadai alidhulumiwa na wafuasi wake na akaandika kitabu cha kusimulia yote.
Kinyume chake, ndoa ya Imran Khan 2018 na Bushra Bibi ilikuwa sherehe ya hali ya chini. Waangalizi wanasema hilo linamfaa vyema na maonyesho yake ya hadharani ya kujitolea kwa Uislamu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Inasemekana Khan alimgeukia mama wa watoto watano kwa ushauri baada ya kukutana kwenye kaburi la Wasufi la Karne ya 13. Wakati huo alikuwa bado ameolewa na mume wake wa kwanza.
Bushra Bibi, ilisemekana kisha akaona katika ndoto kwamba njia pekee ya Khan kuwa waziri mkuu ni ikiwa watafunga ndoa. Na hivyo, wanandoa hao walioana - na miezi sita baadaye Khan akawa waziri mkuu wa Pakistan.
Bushra Bibi, ambaye anaripotiwa kuwa sasa ana umri wa miaka 40, alikuwa mwepesi kutupilia mbali hadithi hiyo katika mahojiano yake pekee ya runinga hadi leo, Oktoba 2018.
Hata hivyo, alimhakikishia aliyekuwa akimhoji kwamba Pakistan itaimarika hivi karibuni chini ya uongozi wa Imran Khan.
Hilo halikutimia: wakati wa uongozi wake, uchumi uliporomoka, gharama ya maisha ilipanda, wapinzani wake wengi wa kisiasa walifungwa jela, uhuru wa vyombo vya habari ulizuiliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari yakaongezeka.
Kama mwanasiasa, Imran Khan alijenga mafanikio yake kwa kuunga mkono uliberali hadharani, wakati huo huo akivutia maadili ya Kiislamu na hisia za kupinga Magharibi. Pia alisemekana kuwa karibu na jeshi la Pakistani, ambalo baadaye aliachana nalo.
Ndani ya miaka minne ya kuwa Waziri Mkuu, maisha ya kisiasa ya Khan yalikuwa yameanza kuyumba. Mwaka wa 2022 aliangushwa kwa kura ya kutokuwa na imani na bunge na mwaka uliofuata alikamatwa na kufungwa huku kesi mahakamani zikiwa zimerundikana dhidi yake.
Sasa, mke wa waziri mkuu zamani wa Pakistan pia amefungwa, akitumikia kifungo cha miaka 14 baada ya wote kukutwa na hatia ya kujinufaisha kinyume cha sheria na zawadi za serikali alipokuwa ofisini.
Ana matatizo mengine ya kisheria pia.
Mume wake wa zamani, ambaye alikuwa naye kwa miaka 28 kabla ya talaka yao mnamo 2017, anamfuatilia kupitia korti.
Khawar Maneka - mtumishi wa umma na mwana wa mwanasiasa mashuhuri - aliwasilisha malalamiko akidai "ndoa ya ulaghai na uasherati" mnamo Novemba, kulingana na gazeti la Dawn la Pakistan. Siku zilizopita, aliiambia GeoNews ya Pakistan kwamba alijitokeza kwa sababu "amechoka kuyaficha ndani".
Mahakama ilitupilia mbali shtaka la uasherati lakini kesi ya ndoa ya ulaghai imeruhusiwa kuendelea.
Chini ya sheria ya familia ya Kiislamu, wanawake ni marufuku kuolewa tena kwa miezi michache baada ya mume wao kufariki au kuachwa. Inadaiwa kuwa Bushra Bibi aliolewa na Imran Khan kabla ya kukamilika kwa muda uliopangwa kufuatia talaka yake kutoka kwa Khawar Maneka.
Nafasi halisi ya Bushra Bibi katika kesi ya zawadi za serikali - ambapo hukumu ilikuja zaidi ya wiki moja kabla ya uchaguzi wa kitaifa ambapo mumewe amepigwa marufuku kushiriki - haiko wazi.
Yeye na mumewe walishtakiwa kwa kuuza zawadi kinyume cha sheria - ikiwa ni pamoja na manukato, seti za chakula cha jioni na vito vya almasi - kupitia wasaidizi wao huko Dubai wakati Khan akiwa ofisini. Kulingana na shirika la habari la Reuters, zawadi hizi zilikuwa na thamani ya zaidi ya rupia milioni 140 ($501,000; £395,000).
Chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) kimetupilia mbali kesi dhidi yake - ambazo mawakili wa Khan wanasema idadi yao katika eneo la 170 - zilichochewa kisiasa.
Hukumu ya Bushra Bibi ilikuwa jaribio jingine la kuweka shinikizo kwa waziri mkuu wa zamani, kaimu mwenyekiti wa PTI na wakili Gohar Ali Khan alisema.
"Bushra Bibi hana uhusiano na kesi hii," aliuambia mtandao wa televisheni wa ndani, kulingana na Reuters.
Hiyo, bila shaka, haibadilishi ukweli kwamba Bushra Bibi - ambaye alijisalimisha muda mfupi baada ya hukumu kutolewa - sasa anakabiliwa na uwezekano wa kufungwa jela kwa miaka mingi.
Notisi ya serikali iliyochelewa siku ya Jumatano ilisema atazuiliwa katika kizuizi cha nyumbani katika makazi yake huko Islamabad hadi amri zaidi itolewe.
Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












