"Nina maumivu ya kichwa sana kiasi kwamba huwa ninapiga kichwa changu ukutani"

Na Angie Brown

BBC Edinburgh

Kwa miaka 17, Daren Frankish amekuwa akisumbuliwa na maumivu ya kichwa kiasi kwamba yanamfanya apige kelele na kupiga kichwa chake ukutani.

Mwanaume huyu mwenye umri wa miaka 53 kutoka Edinburgh, Uskochi anasema anapokuwa na maumivu hayo anahisi kana kwamba anapigwa kwa fimbo ngumu ya mchezo wa besiboli kichwani mwake huku akichomwa kisu jichoni.

Ugonjwa wake ujulikana rasmi kama “cluster headaches," na huchukuliwa kuwa moja ya hali mbaya zaidi kiafya kwa wanadamu.

"Wakati wa karantini ya janga la Covid, ilibidi nitembee hospitali na ninakumbuka nikifikiria kwamba ikiwa basi litapita ningejitupa mbele yake, kwa hivyo ninaelewa kwa nini yanaitwa maumivu ya kichwa ya kujiua," anaelezea mhandisi huyo wa mimea katika mazungumzo na BBC Scotland News.

"Ninaishi kwa hofu ya shambulio lijalo la maumivu, linanitisha sana. Ni mateso ya kisaikolojia kujua kwamba yanaweza kutokea wakati wowote, ninaogopa sana.

Hadi masaa 12

Kwa kawaida, maumivu haya huchukua kati ya dakika 15 na saa tatu na yanaweza kutokea katika awamu saba au nane kwa siku moja. Lakini pia Daren anasema wakati mwingine maumivu haya huyapata kwa vipindi vya saa 12.

Anasema huanza kwa maumivu makali upande wa kushoto wa kichwa, juu ya jicho. "Jicho langu la kushoto linaanza kugeuka rangu na kuwa jekundu, na kutoa machozi kwa wingi, kisha ninahisi pua limeziba na kuanza kuhisi maumivu makali kichwani mwangu.

"Naweza tu kuelezea shambulio hilo kuwa la kutisha. Ninahisi kana kwamba mtu ananigonga kwa fimbo ya besiboli. Pia wakati mwingine huhisi kama kisu kimepita kwenye jicho langu kushoto kabla ya maumivu makali.

"Huwa maumivu haya yakianza ninapiga kelele kitandani , nikipiga kichwa changu ukutani au kitu chochote chenye kelele. Kwa kawaida huwa ninatembea kuzunguka sebule yangu katika giza kabisa kwa sababu siwezi kuvumia mwangaza wowote."

Wakati mwingine Daren anatembea na kitambaa juu ya jicho lake la kushoto, ambalo hutokwa machozi mengi.

Hutembea hadi sehemu tupu na hubeba kadi (na ujumbe ulioandikwa) maelezo ikiwa mtu anajaribu kuzungumza naye.

"Siwezi kuwasiliana na mtu yeyote wakati ninapoumwa kichwa hiki," anaelezea.

Daren na kuongeza kuwa hivi karibuni maumivu yake yamekuwa ya mara kwa mara na zaidi.

Mwezi Mei mwaka jana, alilazwa siku mbili katika kitengo cha dharura katika hospitali ya Royal Infirmary mjini Edinburgh, baada ya kupata awamu mbili za maumivu hayo ambayo kila awamu ilidumu kwa saa 12.

"Mashambulizi haya yalikuwa yasiyovumilika na mabaya zaidi niliyowahi kuyapata," anasema.

Maumivu ya kichwa ya cluster headaches ni nini

Maumivu haya ya kichwa ni ya nadra, na huathiri mtu mmoja kati ya watu 1,000.

Lakini hii ni hali mbaya kwa hali ambayo ni "zaidi ya maumivu ya kichwa", anasema Katie Martin, mkuu wa utafiti katika taasisi ya Utafiti wa Ubongo Uingereza.

"Kama Daren anavyoelezea, maumivu makali ya cluster headaches yanaongezeka, na kusababisha watu kupiga kelele kutokana na maumivu na kupiga vichwa vyao ukutani wakijaribu kumaliza uchungu.

Watu wanaosumbuliwa na hali hii kwa kawaida huwa na umri wa zaidi ya miaka 30, na maumivu haya ya kichwa ni ya kawaida kwa wanaume kuliko wanawake.

Mzunguko wa maumivu unaweza kutofautiana kuanzia maumivu ya mara moja kila saa hadi maumivu kadhaa kwa siku. Kila kipindi kinaweza kudumu kutoka dakika 15 hadi masaa kadhaa.

Maumivu haya humfanya mgonjwa kulazwa hospitalini mara kwa mara , na hivyo huathiri maisha ya wale walioathirika na mara nyingi husababisha wengi wao kupoteza kazi zao.

Pia huhusishwa na hatari ya mara tatu ya msongo wa mawazo na mara ngingi wenye ugonjwa huu huripotiwa kuwa na mienendo ya kutaka kujiua.

Hakuna matibabu.

Matibabu

Daren alipata maumivu ya kwanza mwaka 2007, akiwa na umri wa miaka 37.

"Nilikuwa likizo na familia yangu huko Prague wakati nilipopatwa na maumivu makali sana kiasi kwamba nilifikiri kitu kibaya sana kilikuwa kinatokea, kama uvimbe wa ubongo," anasema baba huyu wa watoto wawili.

Tangu wakati huo, ameagizwa awe anatumia dawa ikiwa ni pamoja na steroids, lithiamu, dawa za moyo na vidonge vya kifafa.

"Mimi sina kifafa, wanajaribu kila kitu, lakini hakuna kitu kinachofanya kazi.

"Pia nina sindano ambayo ninaweza kutumia mara tu shambulio linapotokea na wakati mwingine huwa inapoza maumivu’’, anasema.

Daren ana mirija ya oksijeni nyumbani, ambayo hutumia kujaribu kutuliza maumivu Amejaribu milo tofauti na kuacha kuvuta sigara na unywaji wa pombe, lakini bado anasumbuliwa na maumivu ya kichwa.

"Hatua inayofuata itakuwa kuingiza kizuizi cha neva kichwani mwangu," anaelezea.

Atawekewa sindano ya ndani inayotia ganzi mishipa kwa muda mfupi - Steroidi ambayo hupunguza kuvimba na inaweza kupunguza maumivu hayo katika kipindi cha hadi mwaka mmoja.

"Niko tayari kujitia hatarini kwasababu maumivu haya ya kichwa cha kujiua yanaathiri sana maisha yangu," anaelezea. "Yanaharibu kila kitu na siwezi kufanya chochote.

"Yameniletea matatizo katika yangu na kuchangia katika talaka yangu. Ninajisikia vibaya sana kwasababu watoto wangu walikua wakisikia kelele zangu.

Daren anasema alisoma kwamba kuna ushahidi kwamba maumivu ya kichwa yanaweza kusababishwa na ugonjwa wa uti wa mgongo, ugonjwa ambao alikuwa nao alipokuwa na umri wa miaka miwili na pia alipokuwa na umri wa miaka 12.

Kwa sasa, anapaswa kuishi nayo.

"[Maumivu] yanakuja wakati wowote, sina mamlaka juu nayo. yanapokuja kwa ajili yako, yanakupata."