Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kwanini kichwa huuma ukinywa mvinyo?
- Author, Michelle Roberts
- Nafasi, BBC
Watafiti wa Marekani wanasema huenda wamegundua ni kwa nini baadhi ya watu hupata maumivu ya kichwa baada ya kunywa glasi moja ndogo tu ya mvinyo mwekundu.
Timu ya Chuo Kikuu cha California inasema ni kutokana na mchanganyiko wa zabibu nyekundu ambazo zinaweza kuharibu jinsi mwili unavyoibadilisha pombe.
Zabibu nyekundu hutengeneza quercetin kwa wingi zaidi wakati zinapopigwa na jua.
“Na hiyo inamaanisha kuwa mvinyo mwekundu wa bei ghali, unaweza kuleta maumivu ya kichwa kwa watu wenye historia ya kuwa na maumivu ya kichwa,” mmoja wa watafiti, Prof Andrew Waterhouse, aliambia BBC.
"Aina za zabibu za bei nafuu hupandwa kwenye mashamba yenye dari kubwa na majani mengi, kwa hivyo hazipati jua sana," alisema. "Wakati zabibu za ubora wa hali ya juu hupandwa katika majani kidogo. Kiasi cha jua kinasimamiwa kwa uangalifu ili kuboresha ubora wa mvinyo."
Lakini wengine wana mashaka na utafiti huo.
Prof Roger Corder, mtafiti wa dawa kutoka Chuo Kikuu cha Queen Mary cha London, aliiambia BBC – ''ushahidi unaonyesha mvinyo wa bei nafuu ni mbaya zaidi kwa maumivu ya kichwa, kwa hivyo kuelewa viungo vinavyotumiwa kutengeneza mvinyo mwekundu linaweza kuwa jambo bora zaidi.”
Nadharia Nyingine
Nadharia kadhaa zimeelezwa kujaribu kutegua kitendawili cha maumivu ya kichwa baada ya kunywa mvinyo mwekundu, ambayo yanaweza kutokea ndani ya dakika 30 baada ya kunywa hata kiasi kidogo.
Wengine wanasema sababu inaweza kuwa salfa – kemikali zinazotumiwa kuifanya isiharibike na iendelee kuwa nzuri.
Lakini salfa ipo nyingi zaidi katika mvinyo mweupe kuliko mvinyo mwekundu.
Ingawa baadhi ya watu wanaweza kuwa na mzio na salfa na wanapaswa kuiepuka, lakini kuna ushahidi mdogo kwamba salfa inasababisha maumivu ya kichwa.
Kitu chingine kinachotajwa ni kemikali ya histamine – kiungo kinachowekwa zaidi katika mvinyo mwekundu kuliko mweupe.
Histamini inaweza kupanua mishipa ya damu katika mwili, na inaweza kusababisha maumivu ya kichwa. Lakini uthibitisho kamili bado haupo.
Sababu nyingine inaelezwa ni kwamba; pombe huvunjwa ndani ya mwili kwa hatua mbili - inabadilishwa kuwa kemikali ya sumu iitwayo asetaldehyde, na kisha hubadilika kuwa siki isiyo na madhara.
Ikiwa hatu ya pili haifanyiki, acetaldehyde yenye sumu hujijenga na kuleta athari. Watafiti wanasema acetaldehyde inaweza kuhusika katika maumivu ya kichwa ya mvinyo mwekundu.
Unga wa Quercetin huleta matatizo pindi tu unapochanganywa na pombe, kulingana na watafiti, ambao wamechapisha matokeo ya utafiti wao katika jarida la Scientific Reports.
Quercetin pia hupatikana katika matunda na mboga nyingine nyingi - na ina faida kiafya kwa uwezo wake wa kupambana na maambukizi - na haionekani kusababisha maumivu ya kichwa.
Watafiti bado wanahitaji kuthibitisha nadharia yao kwa watu.
Mtafiti mwenza Prof Morris Levin, mtaalamu wa magonjwa ya mfumo wa neva na mkurugenzi wa Kituo cha Maumivu ya Kichwa katika Chuo Kikuu cha California, San Francisco, alisema: "Hatimaye tuko kwenye njia sahihi ya kuelezea fumbo hili la muda mrefu. Hatua inayofuata ni kupima watu wanaopata maumivu haya ya kichwa, kwa hivyo endelea kutufuatilia."
Wanatumai kuanza tafiti zao baada ya miezi michache.
Athari ya Unywaji Pombe
Lakini Prof Corder, ambaye amechunguza uwezekano wa faida za kiafya za mvinyo, anashuku kuwa viungo vingine vinafaa kuchunguzwa kama vichochezi vya maumivu ya kichwa:
Kemikali ya Dimethyl dicarbonate inatumika kuhifadhi mvinyo wa bei nafuu, kemikali hizo huvunjika na kuunda kemikali za methanoli.
Kunywa sana, kunywa haraka haraka, au kunywa ili ulewe kunaweza kuwa na madhara makubwa ya muda mfupi na muda mrefu kwa afya.
Kunywa mara kwa mara bia kali au kunywa glasi 10 ndogo aina yoyote ya pombe - kunaweza kuharibu ini na kusababisha matatizo mengine ya afya, ikiwa ni pamoja na kiharusi na ugonjwa wa moyo.
Pombe husababisha aina saba tofauti za saratani - hatari ya kupata saratani huongezeka kadiri unavyokunywa.
Takribani kesi moja kati ya 10 ya saratani ya matiti husababishwa na unywaji pombe – kuna kesi 4,400 kwa mwaka nchini Uingereza.
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Munira Hussein