Je, mtoto aliyeua kwa risasi wenzake 8 shuleni alipataje bunduki?

A man holds his head in his hands in front of the school where a 13-year-old shot dead eight classmates and a school guard

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Ni tukio la kwanza la kipekee kutokea Serbia

Tukio la mauaji ambalo halijawahi kushuhudiwa katika shule ya msingi huko Serbia katika mji mkuu wa Belgrade, wakati mvulana mwenye umri wa miaka 13 alipowaua wanafunzi wenzake wanane na mlinzi wa shule, linatoa kengele juu ya idadi ya silaha zilizokuwa mikononi mwa watu binafsi katika nchi hiyo ambayo bado ina hali tete.

Polisi walimkamata mwanafunzi huyo katika shule ya msingi ya Vladislav Ribnikar katikati mwa Belgrade kufuatia shambulio la Jumatano asubuhi.

Wanafunzi wenzake walisema aliingia katika darasa la Historia, kwanza alimpiga risasi mwalimu na kisha akawageuzia silaha wanafunzi wenzake na kuanza kuwashambulia.

Ni mara ya kwanza kwa tukio la aina hiyo kutokea nchini Serbia, waziri wa elimu alisema.

Nchi hiyo imeshtushwa sana na tukio hilo, huku wengi wakihoji ni kwa namna gani shambulio hilo linaweza kutokea, huku kipindi cha maombolezo cha kitaifa cha siku tatu kuanzia Ijumaa hii kimetangazwa.

Silaha mbili za moto zilifikaje mikononi mwa mtoto?

Police arrested a 13-year-old student at the Vladislav Ribnikar primary school in central Belgrade over Wednesday morning's attack.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Kwa mujibu wa Polisi, mtuhumiwa alichukua bunduki kutoka kwa baba yake aliyehifadhi kwenye kasiki ama sanduku maalumu na salama nyumbani.

Kwa mujibu wa Polisi, mshukiwa alikuwa amechukua bunduki za babake kutoka kwenye kasiki iliyokuwa nyumbani kwao. Bunduki mbili zilisajiliwa kwa jina la baba yake na alikuwa na leseni halali za umiliki.

Nchini Serbia, silaha ndogo ndogo, silaha za kuwinda na risasi zinaweza kununuliwa na watu binafsi wenye umri wa zaidi ya miaka 18, ikiwa mamlaka itaaamua kutoa leseni husika.

Kwa mujibu wa sheria iliyopo, ni muhimu kueleza sababu za kina na halali za kumiliki bunduki, pamoja na ripoti ya afya. Hata kama leseni itatolewa, daktari atapaswa kuendelea kufuatilia afya ya mmiliki wa bunduki na kutoa ripoti juu ya mabadiliko yoyote.

Mnamo 2022, Serbia ilifanya mabadiliko ya sheria katika jitihada za kuvutia watu zaidi kusajili silaha na kumiliki kihalali, lakini hakuna data rasmi kuhusu hilo.

Predrag Petrovic wa kituo cha kujitegemea cha utafiti cha kutoka Kituo cha Polisi cha Usalama cha Belgrade aliiambia BBC Serbian mwaka 2022 kwamba bado kuna mianya na ukosefu wa ushirikiano kati ya maafisa wa afya na polisi.

Je Serbia inakabiliwa na tatizo la watu kumiliki silaha?

Mourning parents and relatives in front of the school in central Belgrade

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Nchi imeshtushwa sana na tukio hilo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mamilioni ya silaha ndogo ndogo na wingi wa risasi bado hazijulikani ziliko tangu kuvunjika kwa nchi ya Yugoslavia ya zamani, kuanguka kwa jeshi lake na muongo wa vita katika miaka ya 1990.

Inakadiriwa kuwa raia katika eneo hilo wana silaha ndogo ndogo na silaha zingine mara tisa zaidi kuliko wanajeshi na polisi, kwa mujibu wa Utafiti wa Silaha Ndogo Ndogo Ulimwenguni wa 2018.

Huko Serbia, kuna bunduki 40 kwa kila raia 100.

Ripoti nyingine ya hivi majuzi zaidi inaonyesha umiliki wa bunduki nchini Serbia na nchi jirani ya Montenegro ndio wa juu zaidi barani Ulaya. Hata hivyo si kila mtu anakubali kwamba silaha zenyewe ni tatizo.

"Singesema kuwa umiliki wa bunduki ndio hoja hapa," Bojan Elek, naibu mkurugenzi wa Kituo cha Sera za Usalama cha Belgrade aliambia BBC News.

"Serikali imefanya mengi sana kuchukua bunduki zote hizi haramu. Kuna kampeni za mara kwa mara za msamaha na misaada mingi ya kimataifa," aliongeza.

Hata hivyo, hakuna nayepinga kwamba kunabunduki nyingi kwenye mikono ya watu nchini Serbia.

"Kukosekana kwa utulivu wa kisiasa na kijamii na kiuchumi katika miaka 30 iliyopita, na vitisho vya mara kwa mara vya matusi [kutoka kwa wanasiasa] vya migogoro na vita vipya, vimewafanya watu wengi kusita kusalimisha silaha zao - wangependelea kuziweka "ndani tu'," Predrag Petrovic wa Kituo cha Polisi cha Usalama cha Belgrade aliiambia BBC Serbian mnamo 2022.

Makadirio ya idadi ya silaha haramu nchini Serbia ni kati ya 200,000 hadi zaidi ya milioni moja.

"Hizi ni silaha zilizosalia sio tu kutoka kwenye vita vya miaka ya 1990, lakini kutoka kwenye migogoro mbalimbali katika kanda katika Karne ya 20," Petrovic alisema.

Licha ya kampeni nyingi kwa raia binafsi kukabidhi silaha zao, Petrovic alisema data kutoka kwa tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa "idadi kubwa ya raia hawataki kusalimisha silaha". "Mbali na kukosekana kwa utulivu wa kisiasa, tamaduni inachangia, kwa sababu kumiliki silaha inachukuliwa kuwa ni ishara ya hadhi," alisema.

Silaha ndogondogo katika nchi za Balkans

Serbia - Bunduki 40 kwa kila raia 100

Montenegro - Bunduki 40 kwa kila raia 100

Bosnia and Herzegovina - Bunduki 31 kwa kila raia 100

Northern Macedonia - Bunduki 30 kwa kila raia 100

Kosovo - Bunduki 24 kwa kila raia 100

Croatia - Bunduki 2 kwa kila raia100

Albania - Bunduki 1.5 kwa kila raia 100

Chanzo:Global Small Arms Survey, World Population Review