Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iran inataka kufanya mazungumzo, lakini sina haraka - Trump
Katika matamshi yake ya hivi punde kuhusu suala la nyuklia la Iran na mazungumzo na nchi hiyo, Rais wa Marekani Donald Trump amesema "hana haraka na mazungumzo hayo" kwa sasa.
"(Iran) inataka kujadiliana, sina haraka ya kujadiliana kwa sababu tuliharibu vituo vyao vyote," Trump aliwaambia waandishi wa habari jijini Washington.
Matamshi ya hivi karibuni ya Rais wa Marekani kuhusu mazungumzo na Iran yanakuja wakati Ufaransa ikitangaza jana kuwa itaanzisha mchakato wa Iran kuchukuliwa hatua kuanzia mwishoni mwa Agosti.
Tovuti ya habari ya Axios ilitangaza mchakato huo pia unaungwa mkono na Marekani. Kupitia Waziri wake wa Mambo ya Nje, Marekani imeunga mkono hilo katika majadiliano na viongozi wenzake wa Ulaya huko Ufaransa, Uingereza na Ujerumani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Jean-Noël Barrow amesema iwapo hakuna maendeleo madhubuti yatakayopatikana katika makubaliano ya nyuklia na Iran, nchi tatu za Ufaransa, Uingereza, na Ujerumani zitaanzisha mchakato wa kuchukua hatua, ikiwemo kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran ifikapo mwishoni mwa Agosti.
"Ufaransa na washirika wake wana haki ya kuweka tena vikwazo vya kimataifa [dhidi ya Iran] kwa silaha, benki na vifaa vya nyuklia, vikwazo ambavyo viliondolewa miaka 10 iliyopita," aliwaambia waandishi wa habari.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa alisema: "Bila ya dhamira thabiti, inayoonekana na inayoweza kuthibitishwa na Iran, tutachukua hatua hii mwishoni mwa Agosti."
Barrow alitangaza hayo, kabla ya mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.
Kambi mbili zinazokinzana
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi, ambaye alikuwa China kuhudhuria Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai, alikutana na mawaziri wenzake wa China na Urusi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov alisema alizungumza na Araghchi kuhusu "kutafuta suluhu la amani kwa mgogoro wa Iran."
"Hakuna mtu, ikiwa ni pamoja na wakaguzi wa IAEA, ambaye amewahi kutoa ushahidi kwamba Iran inatafuta kutengeneza bomu la nyuklia]," alisema Lavrov.
"Kanuni muhimu sana ni kutokiuka haki halali ya Iran, sawa na haki ya mataifa mengine yasiyo ya nyuklia ambayo ni wanachama wa IAEA na waliotia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Nyuklia (NPT), kuwa na haki ya kurutubisha uranium kwa madhumuni ya nishati."
China na Urusi, zikiwa wanachama wawili wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zinapinga kurejeshwa kwa vikwazo dhidi ya Iran.
Makubaliano ya JCPOA
Baada ya kufikiwa makubaliano ya JCPOA mwezi Julai 2015, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliidhinisha makubaliano hayo na kufuta maazimio yote ya hapo awali, vikiwemo vikwazo dhidi ya Iran.
Katika utaratibu wa utatuzi wa mizozo katika makubaliano ya JCPOA, inawezekana kwa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kurejesha vikwazo vilivyoondolewa iwapo hawataridhika na utekelezaji wa Iran wa wajibu yake.
Kwa mujibu wa JCPOA, mara tu hatua zitakapo anza kuchukuliwa, hakuna mwanachama yeyote wa kudumu wa Baraza la Usalama atakayeweza kupinga rasimu ya azimio hilo na kuzuia vikwazo dhidi ya Iran.
Fursa ya kutumia utaratibu huu na kufufua maazimio ya Baraza la Usalama dhidi ya Iran inamalizika tarehe 18 Oktoba mwaka huu.
Iran imetangaza kuwa itachukua hatua dhidi ya maazimio hayo iwapo yatafufuliwa.
Marekani iliwahi kuanzisha juhudi za kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran kuelekea mwisho wa muhula wa kwanza wa Donald Trump, lakini wakati huo, Ufaransa na Uingereza, pamoja na China na Urusi, zilipinga uamuzi huo na hivyo kutoungwa mkono.
Vikwazo vipya vya EU
Baraza la Ulaya limesema jana Jumanne (Julai 14), limeweka vikwazo kwa watu wanane wa Iran na taasisi moja kwa "ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu" na "ukandamizaji wa serikali."
Taarifa ya Baraza la Ulaya inaeleza waliowekewa vikwanzo wanahusika na ukiukaji wa haki za binadamu kama vile unyongaji na mauaji ya kiholela, na pia kutoweka kwa wapinzani au wakosoaji.
" Mtandao wa Zaindashti , kikundi kinachohusishwa na Wizara ya Ujasusi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," kimewekwa kwenye orodha ya vikwazo vya Umoja wa Ulaya. Kulingana na taarifa ya Baraza la Ulaya, mtandao huo “umefanya vitendo vingi vya ukandamizaji, yakiwemo mauaji ya wapinzani.”
Mkuu wa mtandao huo, Naji Ebrahim Sharifi Zeindashti, "mlanguzi wa dawa za kulevya," na washirika wake Abdolvahab Kochak, Ali Esfanjani, Ali Kochak, Akram Oztunc, na Nihat Asan, pia wameidhinishwa. Wanadaiwa kuhusika katika mauaji ya Masoud Vardanjani na Saeed Karimian (mmiliki wa Jam TV).
Marekani iliwawekea vikwazo watu hao mwaka jana.
Baraza la Ulaya pia limemuidhinisha Mohammad Ansari, kamanda wa Kikosi cha 840 cha Jeshi la Quds la IRGC, "aliyeamuru kuuawa kwa waandishi wa habari.
Mali zao zimezuiliwa na wamepigwa marufuku kuingia Umoja wa Ulaya.