Mimea 7 yenye sumu kali zaidi duniani

Chanzo cha picha, Getty Images
Ingawa mimea mingi duniani ina faida kubwa kiafya na kiikolojia, kuna baadhi ambazo ni hatari sana kwa maisha ya binadamu na wanyama. Mimea hii huonekana ya kawaida, mara nyingine hata kuvutia, lakini ndani yake imebeba sumu kali sana.
Katika kuadhimisha Siku ya afya ya mimea (Mei 12), tunakumbushwa kwamba afya ya mimea si tu ulinzi dhidi ya magonjwa, bali pia uelewa wa hatari zinazoweza kujificha kwenye mazingira yetu.
Hii hapa ni orodha ya mimea 7 inayojulikana na wanasayansi kuwa na sumu kali zaidi duniani, kwa mujibu wa taasisi kubwa za masuala ya afya na magonjwa duniani kama Royal Botanic Gardens Kew, Centers for Disease Control (CDC) na National Institutes of Health (NIH).
1. Oleander (Nerium oleander)
Ingawa maua yake mekundu au meupe yana mvuto mkubwa, Oleander ni mojawapo ya mimea yenye sumu kali zaidi duniani.
Kwa mujibu wa Taasisi inayoshughulika na kukinga na kudhibiti magonjwa (CDC), majani, maua, na hata mti wake una kemikali zinazojulikana kama cardiac glycosides, ambazo zinaathiri moyo. Hata kiasi kidogo cha majani kilicholiwa na mtoto au mnyama mdogo kinaweza kusababisha kifo.
Mmea huu hupatikana maeneo ya Mediterania lakini hulimwa pia kama mmea wa mapambo katika sehemu nyingi duniani, ikiwemo Afrika Mashariki.
2.Castor Bean (Ricinus communis)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mbegu za mmea huu hutoa mafuta ya castor yenye faida kwa ngozi na mfumo wa chakula, lakini pia zina ricin, moja ya sumu kali zaidi duniani.
Shirika la Ulinzi wa Mazingira la Marekani (EPA) linaeleza kuwa hata kiasi kidogo sana cha ricin kinaweza kuua mtu mzima ndani ya siku chache, kwa kuvuruga utendaji kazi wa seli mwilini.
Kwa bahati mbaya, mmea huu hustawi vizuri maeneo ya joto, ikiwemo Tanzania, na wakati mwingine huonekana kwenye barabara au mashamba kama magugu.
3.Water Hemlock (Cicuta spp)

Chanzo cha picha, Getty Images
Kwa mujibu wa USDA (U.S. Department of Agriculture), Water Hemlock ni mmea wa porini unaopatikana karibu na vyanzo vya maji na ni mojawapo ya mimea yenye sumu kali zaidi Amerika Kaskazini. Inayo sumu inayoitwa cicutoxin, ambayo hushambulia mfumo wa neva na kusababisha degedege, kupoteza fahamu, na hata kifo ndani ya saa chache.
Mmea huu ni hatari kwa binadamu na mifugo, na unapotafunwa au kumezwa kwa bahati mbaya, huweza kuwa na madhara ya haraka na yasiyotibika.
4.Belladonna (Atropa belladonna)

Chanzo cha picha, Getty Images
Inajulikana pia kama Deadly Nightshade, mmea huu uliotumika kihistoria kama dawa ya macho na sumu ya kivita, una kemikali aina ya atropine na scopolamine. Kemikali hizi hupooza mfumo wa neva na kupandisha mapigo ya moyo hadi kiwango hatari.
Kwa mujibu wa Kew Science, hata matunda yake madogo ambayo yanaweza kuonekana kama zabibu kwa mtoto yanaweza kusababisha kifo.
Mmea huu hupatikana zaidi Ulaya, lakini umeenea sehemu nyingine kupitia bustani za mimea adimu.
5. Aconite (Aconitum napellus)

Chanzo cha picha, Getty Images
Mmea huu pia hujulikana kama monkshood au wolf's bane, na umetumika kihistoria kama sumu ya mishale ya kupambana na wanyama wakali.
Kwa mujibu wa jarida la British Medical Journal (BMJ), kemikali ya aconitine huathiri mishipa ya fahamu na moyo, na inaweza kuua kwa haraka baada ya kuingia mwilini.
Hupatikana zaidi maeneo ya baridi ya Ulaya na Asia, lakini mara nyingine hupandwa kama maua kwenye bustani za mapambo.
6.Rosary Pea (Abrus precatorius)
Mbegu zake nyekundu na nyeusi hutumika kutengenezea shanga, lakini zina abrin, sumu kali zaidi ya ricin. Kwa mujibu wa NIH (National Institutes of Health), abrini inaweza kuharibu seli za mwili haraka sana, hata ikiwa kwenye kiasi kidogo.
Mmea huu huota tropiki kote duniani, ikiwemo Afrika Mashariki, na mara nyingine hukusanywa na watoto kwa ajili ya michezo au mapambo jambo ambalo ni hatari sana.
7.Gympie-Gympie (Dendrocnide moroides)

Chanzo cha picha, Getty Images
Huu ni mmea wa porini kutoka Australia, lakini umaarufu wake umeenea duniani kutokana na athari zake kali. Majani yake yana nywele ndogo ndogo zenye sumu kali sana, ambazo zikigusa ngozi huleta maumivu yanayoelezewa kama "kuchomwa na moto wa umeme" yanayoweza kudumu kwa wiki au miezi.
Kwa mujibu wa Queensland Herbarium, watu waliowahi kuuguswa hueleza kuwa ni moja ya maumivu mabaya zaidi wanayowahi kupitia.















