Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi Tanzania 2025: Familia tano za vigogo CCM zilizopenya mbio za Ubunge
Chama cha Mapinduzi (CCM), moja ya chama kikongwe barani Afrika kinajiandaa na uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, miongoni mwa maandalizi hayo ni kupata wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, huku wakiwa na uhakika kuwa Rais wa sasa wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ndiye mgombea wao katika nafasi ya urais.
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, ilipitisha majina ya watia nia wa nafasi mbalimbali, kwa ajili ya kwenda kupigiwa kura za maoni na wajumbe, kisha majina hayo yakarudi kwa halmashauri kuu ya chama kwa ajili ya kuchagua jina moja.
Mwishoni mwa wiki hii CCM ilitoa orodha ya majina ya watakaogombea Ubunge, wale wa viti maalum na nafasi za baraza la Wawakilishi kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar.
Katika orodha ya wagombea wa CCM, wapo ambao wametoka katika familia za vigogo wa chama hicho, kuanzia rais wa sasa na marais wastaafu, pia wanachama wengine wa ngazi ya juu katika chama hicho.
Rais mstaafu Kikwete
Katika Jimbo la Mchinga Mkoani Lindi, CCM itawakilishwa na Salma Kikwete, ambaye yupo katika nafasi ya Ubunge tangu mwaka 2017. Ikumbukwe Salma ndiye aliyekuwa Mgombea pekee aliyechukua fomu katika Jimbo la Mchinga.
Katika familia ya Rais mstaafu wa awamu ya nne Jakaya Kikwete kuna mwanasiasa mwingine, ambaye atagombea katika Jimbo la Chalinze, Ridhiwani Kikwete, naye alikuwa mgombea pekee kuchukua fomu.
Rais Samia
Mtoto wa Rais Samia Suluhu Hassan, Wanu Hafidh Ameir alipitishwa na CCM kama mtia nia wa Ubunge jimbo la Makunduchi, Zanzibar, na hatua iliyofuata ni kuchuana na wenzake katika kura za maoni.
Baada ya kura za maoni, Wanu alipata ushindi kwa kura 1356, akiwabwaga wapinzani wake, huku mpinzani wake wa pili akiambulia kura 3 pekee. Hatimaye CCM imepitisha jina lake kugombea ubunge jimbo hilo.
Hayati Rais Mwinyi
Familia ya Hayati Rais Ali Hassan Mwinyi na mtoto wake ambaye ni Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi, imejikita katika siasa za Tanzania kuanzia nafasi ya urais hadi katika Bunge la Tanzania.
Hussein Mwinyi atagombea urais Zanzibar. Huku Asma Ali Hassan Mwinyi aliibuka mshindi katika kura za maoni za CCM kwa nafasi ya Ubunge katika Jimbo la Welezo Zanzibar. Chama chake kimempitisha kugombea Ubunge jimbo hilo.
Hayati Rais Magufuli
Chama Cha Mapinduzi(CCM) kilimteua Mtoto wa Rais wa awamu ya tano Hayati John Pombe Magufuli, Jessica Magufuli na wagombea wengine 30 kugombea Ubunge Viti Maalum kupitia kundi la UVCCM.
Jesca alishika nafasi ya pili kwa kupata kura 361, akitanguliwa na Ng'wasi Kamani aliyepata kura 409, nafasi ya tatu ikichukuliwa na Halima Bulembo aliyepata kura 320.
CCM imemteua Jesca kuwa Mgombea Ubunge viti maalum Vijana (UVCCM).
Dk. Emmanuel Nchimbi
Aliyekua Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, John John Nchimbi aliongoza kura za maoni Jimbo la Nyasa baada ya kupata kura 9,157 kati ya kura 10,695 zilizopigwa. Jana CCM imemteua kupeperusha bendera katika kinyang’anyiro cha Ubunge katika jimbo hilo.
Huyu ni ndugu na Emmanuel John Nchimbi. Mpaka mwishoni mwa wiki alikuwa Katibu Mkuu wa CCM, kabla ya Jumamosi kutangazwa Asha-Rose Migiro kushika nafasi hiyo. Emmanuel Nchimbi ndiye mgombea mwenza katika nafasi ya Makamu wa Rais katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025 kupitia chama hicho.
Sio mara ya kwanza na wapo wengi waliotemwa
Hiki si kitu cha kushangaza, familia za vigogo kuwa katika sehemu ya uongozi wa nchi. Kama ilivyo wananchi wengine wana uhuru na haki ya kufanya hivyo. Sheria haiwazuii kugombea ni utashi, uwezo na matakwa ya wapiga kura.
Toka enzi za mwalimu Julius Nyerere, Rais wa kwanza mpaka sasa awamu ya sita, si jambo la ajabu kuona mtoto, ama ndugu yeyote kuwa sehemu ya uongozi uwe wa kuchaguliwa ama wa kuteuliwa.
Lakini kwenye mchakato wa mwaka huu wa CCM, pia wapo familia za vigogo walioachwa. Januari Makamba, mtoto wa Katibu wa zamani wa CCM, na mwanachama mwandamizi wa siku nyingi wa CCM, Mzee Yusuph Makamba jina lake halikurudi kabisa hata kupigiwa kura.
Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kambarage Wasira kutoka familia ya Makamu mwenyekiti wa CCM, Stephen Wassira, aliomba kuteuliwa na chama hicho kugombea ubunge Bunda Mjini.
Licha ya kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 2032 nyuma ya mbunge aliyemaliza muda wake Robert Chacha Maboto (kura 2545), lakini ni Ester Amos Bulaya, aliyeshika nafasi ya tatu kwa kura 625, jina lake limepitishwa kuwania jimbo hilo.
Katika Jimbo la Namtumbo, aliyekuwa Mbunge Vita Kawawa alishindwa kura za maoni mbele ya Dkt. Juma Zuberi Homera, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya. Homera alipata kura 11,836 asilimia 92 huku Kawawa akipata kura 852.
Kawawa ni mtoto wa Marehemu Rashidi Mfaume Kawawa, aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Tanzania kati ya mwaka 1972-1977, serikali ya awamu ya kwanza ya Julius Nyerere. Angeweza kurejeshwa kugombea kama imewezekana kufanya hivyo kwa Bulaya.
Panga pia limemkuta, Mtoto wa waziri Mkuu wa zamani, hayati Edward Lowassa, Fredrick Lowassa aliyeachwa katika jimbo mla Mondoli aliloliongoza katika kipindi kilichopita.
Ole Sabaya, Mkuu wa zamani wa Wilaya ya Hai, jina lake likiondolewa kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi, ni mtoto wa kigogo wa muda mrefu wa CCM, Loy Thomas Sabaya, ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa chama hicho Arusha.
William Malecela, mtoto wa waziri mkuu wa zamani, John Malecela, ambaye mama yake wa kambo, Anne Kilango Malecela amepitishwa jimbo la Same Mashariki, aliwahi kusema lilipoibuka suala la familia za vigogo kuingia kwenye utawala kwenye chaguzi zilizopita: "Ni lazima tukubaliane kwanza kwamba watoto wa viongozi wa Tanzania ambao wengi wameanza kuingia kwenye siasa na kushika nafasi mbalimbali wana haki kabisa ya kushika nafasi yoyote ya uongozi wa taifa kama Watanzania wengine.
Malecela aliongeza "Haki yao ya Kikatiba kuchaguliwa au kushiriki nafasi yoyote ya kisiasa kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo haifutwi au kuondolewa kwa sababu ya nafasi za baba zao kwa taifa letu, sasa au huko nyuma".