Uchaguzi Tanzania 2025: ACT ina 'ubavu' gani wa kukabiliana na CCM?

    • Author, Rashid Abdallah
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

"CCM ijiandae kufunga virago kwa sababu wakati wao wakuongza Tanzania umepita", kauli ya Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo Ado Shaibu kwenye Mkutano mkuu wa chama hicho Agosti 06, 2025 jijini Dar es Salaam.

Kauli hii inajenga hisia za kuhoji nguvu za chama hicho katika kuitoa CCM madarakani, chama kilichokaa madarakani kwa miaka zaidi ya 60 tangu nchi hiyo ipate uhuru.

Katika uchaguzi wa Mwaka 2020, kupitia kwa mgombe wake Bernard Membe, ambaye alitoka CCM na kujiunga na ACT Wazalendo, chama hicho kilipata kura 81,129 za urais kikishika nafasi ya tatu nyuma ya CHADEMA na CCM walioongoza kupitia kwa mgombe wake Hayati John Magufuli kwa kuzoa kura 12,516,252.

Kura hizo zilishuka kutoka 98,763 alizopata mgombea wake Anna Mghwira katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 huku Magufuli alishinda kwa kura 8,882,935. Chadema kupitia kwa mgombea wake Hayati Edward Lowassa kilizoa kura 6,072,848, kura nyingi zaidi kuwahi kupata mgombea wa upinzani tangu uchaguzi wa vyama vingi uanze kwenye uchaguzi wa mwaka 1995.

Vyama vingine vilivyokuwa na nguvu kwa nyakati tofauti kama CUF, NCCR-Mageuzi, kikaja chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, vimekuwa vikijaribu mara kadhaa, ikiwemo hata kuungana kupitia UKAWA katika uchaguzi wa mwaka 2015, lakini haikuwa rahisi kukabiliana na CCM, yenye mizizi mikubwa. Hapa ndipo panapoibuka swali: Je, ACT Wazalendo ina nguvu za kupambana na CCM?

Wagombea wake

Ukiacha kuwa na wanachama na wafuasi wa kutosha, wagombea wenye sifa na nguvu ni eneo muhimu la kisiasa unapotaka kupata ushindi kwenye uchaguzi kama chama cha siasa.

Mkutano Mkuu Maalumu wa ACT-Wazalendo umeidhinisha majina ya Luhaga Mpina na Othman Masoud kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar.

Mpina akitokea CCM wiki hii na kukabidhiwa bendera ya chama hicho kuwania Urais wa Tanzania, Masoud ambaye ni makamu wa kwanza wa rais wa Znazibar atagombea urais wa visiwa hivyo. ACT inasema viongozi hao wanatosha kabisa kuonyesha nguvu ya chama hicho kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.

Kiongozi mstaafu wa chama hicho, Zitto Kabwe alisema kuhusu wagombea urais hao "hii ni vita ya kizazi, hiki kizazi kinakwenda kufanya kazi (kuiondoa CCM) ambayo nyinyi (wazee) mmeshindwa kufanya".

Katibu Mkuu wa chama hicho Ado Shaibu amethibitisha pia chama hicho kimepata wagombea wengi zaidi katika uchaguzi huu, kuonyesha nguvu yake na namna kilivyojipanga kukabiliana na CCM.

Kwa mujibu wa Katibu huyo, chama hicho kina wagombea udiwani kwenye kata zote nchi nzima, kimekamilisha kupata wawakilishi na wagombea ubunge katika majimbo yote 50 kule Zanzibar na majimbo 222 kwa upande wa Tanzania bara

"Ukicha kila jimbo tuna mgombea, tuna wimbi kubwa sana, kuna vuguvugu sana la watu wanaogonga hodi ACT wazalendo tuunganishe nguvu, tufanye kazi pamoja, tuunganishe nguvu ili tuiongoe CCM madarakani, wako wengi wanatoka CCM, na wako wengine wanatoka vyama vingine vya upinzani, ikiwemo ndugu zetu CHADEMA, tuunganishe nguvu tuitoe CCM madarakani", alisema Shaibu.

Pia unaweza kusoma

Upande wa Bara

Ukitaka kuyataja mafanikio ya ACT kwa upande wa bara, kwa hakika aya moja inatosha: Kilianzishwa mwaka 2014. Kilisimamisha mgombea wake wa kwanza wa urais katika uchaguzi mkuu wa 2015 na kilishinda kiti kimoja katika Bunge na viti kadhaa vya udiwani. Kwa upande wa Zanzibar? Tutafika huko pia.

Wakati Chama kikuu cha upinzani Tanzania bara, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kikionesha kila dalili kwamba huenda kisishiriki uchaguzi wa mwaka huu, bila shaka bongo za watunga sera wa ACT wameona hii ni nafasi kwao, angalau kuzitawala siasa za upinzani, ikiwa watashindwa kuingia Ikulu.

Ni ukweli ulio wazi kuwa si kila mtu amejiandaa kuipigia kura CCM au kukaa nyumbani kisa Chadema haitoshiriki. Kuna ambao wanatamani kuiona CCM ikiondoka, kuna ambao wanatamani kuiona CCM haitawali pekee Bungeni, watu hawa bila shaka wataona bora kwenda kumpigia kura mpinzani yoyote kuliko kutopiga kabisa.

Na hapo ndipo nguvu za ACT katika siasa za upinzani bara zinaweza kuibuka na kumea. Kutoka kuwa na Mbunge mmoja kati ya mwaka 2015 hadi 2020, na kukosa Mbunge kabisa katika ya 2020 hadi 2025, na kujipatia Wabunge kadhaa baada ya uchaguzi wa 2025.

Kuna nyakati siasa haitoi chaguo kati ya jambo ‘baya na zuri.’ Yapo mazingira ambapo unalazimika uchague tu kati ya ‘baya na baya zaidi.’ Udogo wa ACT katika siasa za bara, unaweza kuwa ni sababu pia inayowasukuma kushiriki uchaguzi. Kushiriki uchaguzi katika mazingira yenye mashaka, ni jambo baya lakini kutoshiriki huenda likawa baya zaidi.

Chama kidogo kinachokuwa kama ACT, kisiposhiriki uchaguzi, uamuzi huo haukifanyi chama hicho kuwa kikubwa, kupendwa na kuongeza ushawishi. Bali hukifanya kuwa kidogo zaidi, kiduchu, kidigi na hatimaye hupotea kabisa.

Upande wa Zanzibar

Baada ya Chama cha Wananchi (CUF), ambacho kilikuwa chama kikuu cha upinzani Zanzibar, kuporomoka, kutokana na mgogoro wa vigogo wawili hayati Maalim Seif na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, na Maalim kujiondoa chamani 2029 na kuhamia ACT Wazalendo, chama hicho kimeibuka kama mrithi wa siasa za upinzani visiwani humo.

Kimetoa Wabunge kadhaa katika Uchaguzi wa 2020 na Mawaziri katika serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, kubwa zaidi Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud ni kiongozi katika serikali ya sasa.

Kwa upande wa Zanzibar, ACT itaendelea kuimarika, itaimarika zaidi katika uchaguzi wa mwaka huu ikiwa uchaguzi huo utakwenda vyema bila ya sarakasi za kisiasa kama zile za 2020, ambavyo vyama vya upinzani vilipoteza kila jimbo.

ACT itakuwa na uwezo mzuri zaidi Zanzibar kupambana na CCM. Na huko, ndiko lolote linaweza kutokea ikiwa karatasi za kura zitaheshimiwa.

Changamoto kubwa ni ipi?

Lakini ushiriki wa ACT Wazalendo katika uchaguzi, haufuti hoja za muda mrefu za Chadema. Vuta nikuvute ya Chadema dhidi ya utawala, inatokana na madai yao ya kutaka mabadiliko hasa katika vyombo vinavyosimamia uchaguzi. Chadema haiamini kwamba mifumo ya sasa inaweza kutoa haki kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi.

Kwa kuzingatia kilichotokea katika uchaguzi wa 2020, kulikuwa na walakini mkubwa (pale upinzani ulipokosa viti bungeni hata katika majimbo ambayo ni ngome zao za miaka yote). Kwa kuzingatia hilo, hoja ya Chadema inabaki kuwa yenye mashiko. Ingawa uamuzi wao wa kutoshiriki, hatujui utasaidia vipi kupata mabadiliko wayatakayo.

Tukirudi kwa ACT, swali litabaki kwao; wamejipangaje kuhakikisha uchaguzi huu hauwi mchafukoge kama ule uliopita? Na hiyo ndio changamoto kubwa ilio mbele yao wakati huu wakijiandaa na kujipanga kutafuta wagombea wao.

"Tunakwenda kwenye miezi mitatu migumu sana, lakini ni miezi mitatu ya kurejesha heshima ya kura ya Tanzania", anasema Zitto bila kufafanua zaidi namna watakavyoirejesha heshima hiyo, ambayo watu wa Chadema wamekuwa wakipigia kelele kwa muda mrefu.

Nguvu za ACT kupambana na CCM, zitategemea pakubwa ikiwa uchaguzi utakuwa huru na haki. Kwa hakika kuna uhusiano ulio wazi kati ya mafanikio ya vyama vya upinzani barani Afrika na utayari wa wale wanaosimamia uchaguzi katika kutenda haki.