Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Uchaguzi wa Marekani 2024: Kipi kitatokea kwa Trump na kesi zake mahakamani?
- Author, Madeline Halpert
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Donald Trump atakuwa rais wa kwanza kuchukua madaraka huku akiwa na kesi kadhaa za uhalifu dhidi yake mahakamani.
Lakini matatizo yake mengi ya kisheria yataisha atakapoingia Ikulu. Majadiliano tayari yameanza kati ya timu ya Trump na ofisi inayosimamia kesi za shirikisho kuhusu namna ya kumaliza kesi hizo, kulingana na CBS.
Kijue kile kinachoweza kutokea kwa kila moja, kati ya kesi nne za zinazomkabili.
Hukumu ya New York
Donald Trump alipatikana na hatia kwa makosa 34 ya kughushi rekodi za biashara yake mwezi Mei huko New York.
Mahakama ya New York ilimpata na hatia ya makosa yote yanayohusiana na malipo ya pesa zilizotolewa kwa nyota wa filamu za utupu ili kumziba mdomo.
Jaji Juan Merchan aliipeleka mbele hukumu ya Trump kutoka Septemba hadi 26 Novemba, baada ya uchaguzi.
Bado anaweza kuendelea na hukumu kama ilivyopangwa licha ya ushindi wa Trump, anasema mwendesha mashtaka wa zamani wa Brooklyn, Julie Rendelman.
Lakini wataalamu wa sheria wanasema hakuna uwezekano wa Trump kuhukumiwa kifungo kama mzee, na kwa vile ni kosa lake la kwanza.
Ikiwa atahukumiwa kifungo gerezani, mawakili wake wataka rufaa dhidi ya hukumu hiyo mara moja, na kusema kifungo hicho kitamzuia kutekeleza majukumu yake rasmi na anapaswa kusalia huru akisubiri rufaa hiyo, anasema Bi Rendelman.
"Mchakato wa kukata rufaa katika kesi hiyo unaweza kuendelea kwa miaka," anasema.
Kesi ya Januari 6
Wakili maalumu Jack Smith alifungua mashtaka ya jinai dhidi ya Trump mwaka jana kutokana na tuhuma za kutaka kupindua ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa 2020.
Trump anakana kufanya kosa hilo.
Kesi hiyo imekuwa na mtafaruku wa kisheria tangu Mahakama ya Juu ilipotoa uamuzi msimu huu wa joto kwamba Trump kwa namna fulani ana kinga ya kutofunguliwa mashitaka ya jinai kwa vitendo alivyofanya akiwa madarakani.
Smith amewasilisha tena kesi yake, akisema jaribio la Trump la kubatilisha uchaguzi halikuhusiana na majukumu yake rasmi.
Hii ni moja ya kesi ambayo inaweza kuondoshwa kwa majadiliano ya sasa.
Akiwa rais mteule, kesi ya jinai kwake inaweza kuondoshwa, kulingana na mwendesha mashtaka wa zamani wa shirikisho Neama Rahmani.
“Iko wazi kuwa rais aliye madarakani hawezi kushitakiwa, hivyo kesi juu ya uchaguzi katika Mahakama ya Wilaya ya DC itaondoshwa,” anasema.
Bw Rahmani anasema iwapo Smith atakataa kutupilia mbali kesi hiyo, Trump anaweza kumuondoa, kama alivyoahidi kufanya.
"Nitamfuta kazi ndani ya sekunde mbili," Trump alisema wakati wa mahojiano ya redio mwezi Oktoba.
Kesi ya hati za siri
Smith pia anaongoza kesi dhidi ya Trump juu ya tuhuma za kuzishughulikia vibaya hati za siri baada ya kuondoka Ikulu ya White House, mashtaka hayo Trump anayakanusha pia.
Inaelezwa alizihifadhi hati nyeti nyumbani kwake Mar-a-Lago na kutatiza juhudi za Idara ya Haki kuzipata hati hizo.
Jaji aliyepewa kesi hiyo, aliyeteuliwa na Trump, Aileen Cannon, alitupilia mbali mashtaka mwezi Julai, akisema Smith aliteuliwa isivyofaa na Idara ya Haki kuongoza kesi hiyo.
Smith alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, lakini kwa vile Trump anarudi kuchukua madaraka, mazungumzo sasa yanaendelea kuhusu kuimaliza kesi hiyo.
Rahmani anasema, anatarajia kesi ya hati za siri itafikia hatima sawa na kesi ya uchaguzi.
Kesi ya uchaguzi ya Georgia
Trump pia anakabiliwa na mashtaka ya jinai huko Georgia kuhusu juhudi zake za kupindua matokeo ya uchaguzi wa 2020 katika jimbo hilo.
Kesi hiyo imekumbwa na vikwazo vingi, ikiwa ni pamoja na jitihada za kumwondolea sifa Mwanasheria wa Wilaya, Fani Willis juu ya uhusiano wake na wakili aliyemwajiri kufanyia kazi kesi hiyo.
Mahakama ya rufaa iko mbioni kutathmini iwapo Willis aruhusiwe kuendelea na kesi hiyo au la.
Lakini kwa vile Trump ndiye rais ajaye, kesi hiyo inaweza kukabiliwa na ucheleweshaji zaidi, au ikiwezekana kufutwa.
Inatarajiwa kusitishwa wakati Trump akiwa madarakani, kulingana na wataalamu wa sheria.
Wakili wa Trump, Steve Sadow alisema hayo alipoulizwa na jaji ikiwa Trump bado anaweza kushtakiwa iwapo atachaguliwa.
“Jibu la hilo, naamini chini ya kifungu cha ukuu na majukumu yake kama rais wa Marekani, kesi hii haitoendelea hadi baada ya kumaliza muda wake wa uongozi,” alisema.