"Sikujua kuwa nina uja uzito hadi nilipojifungua"

Chanzo cha picha, Bryony Mills-Evans
Mwanamke huyo hakujua kwamba alikuwa na mimba hadi baada ya kujifungua.
Alisimulia jinsi alivyojifungua peke yake katika saluni aliyofanyia kazi na kukata kitovu cha mtoto wake kwa mkasi.
Bryony Mills-Evans alisema hata hakujua kama alitaka watoto, lakini alijifungua akiwa na miaka 23 bila dalili zozote za ujauzito.
Mimba zisizoeleweka, ambapo mwanamke hajui hali yake hadi mwishoni mwa ujauzito au, kama ilivyo kwa Briony, hadi wakati wa uchungu, zimeelezewa na profesa mmoja wa masuala ya uzazi kuwa "nadra lakini si ya kipekee."
Baada ya kujua kwamba kuna mambo machache sana yanayojulikana kuhusu mimba hizo, Briony aliamua kusimulia hadithi yake ili wengine waliowahi kupata mimba hiyo wajue kwamba hawako peke yao.
Takwimu zinasema kwamba karibu watoto 325 wanaozaliwa bila kutarajiwa hutokea nchini Uingereza kila mwaka.
Mwanamke huyo alikuwa akifanya kazi Newtown, Wales, siku aliyojifungua. Baada ya kummalizia mteja wake wa mwisho, alihisi kile alichofikiri ni maumivu ya hedhi tu.
"Nilikuwa nimevaa sokisi zinazonibana, hivyo nilijilaza kwenye kochi ili nizivue kwa sababu nilifikiri zinaweza kupunguza maumivu," alisema.
"Baada ya dakika 10, kichwa chake kilionekana."
"Nilidhani nilihitaji tu kwenda bafuni, nikatazama chini na nikaona kichwa chake."
Briony alianza kusukuma kwa nguvu na akajifungua mtoto wa kike, Willow, mwenye uzito wa kilo 3.1.
"Sikujua la kufanya. Simu yangu ilikuwa imekufa na ilikuwa katika chumba kingine, hivyo nilijilaza kitandani kidogo," alisema.
"Baada ya muda niliona kitovu chake kimegeuka kuwa cheupe. Nilikuwa na mkasi karibu yangu, sijui chochote kuhusu watoto, lakini nilikata kamba na kumfunga mtoto kwenye rundo la taulo."

Chanzo cha picha, Bryony Mills-Evans
Briony alienda kuchaji simu yake, lakini alihisi hamu ya kwenda chooni tena.
"Sikujua kuna kondo lingine linatoka. Nadhani niliogopa sana kuwa ni mtoto mwingine," alikumbuka.
Baada ya kupiga simu 999, Briony alipelekwa hospitalini.
Akiwa njiani akiulizwa maswali na madaktari alimtumia mama yake meseji kama "nimejifungua tu, usijali, wote tuko sawa," kisha akamuuliza kama anaweza kukutana nao.
"Nadhani nilithubutu tu kuichukua asubuhi iliyofuata," mwanamke huyo alisema.
"Niliogopa sana kwa sababu nilikuwa na umri wa miaka 23 tu na sikuwa na uhakika kuwa nilitaka watoto hata kidogo."

Chanzo cha picha, Bryony Mills-Evans
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Briony anasema alianza kutulia kidogo tu mamake alipomwambia ampe mtoto huyo jina.
"Ilikuwa mshtuko. Kila mtu huniambia kila mara, 'Lazima umepooza kwa hofu.'
"Sikumbuki kama nilipooza, niliendelea kufanya kila kitu kwa sababu sikuwa na chaguo jingine."
Briony alisema hakuwa na dalili zozote ambazo ungetarajia wakati wa ujauzito, pamoja na tumbo.
"Watu wanapouliza, 'Inakuwaje usijue?' Huwa nasema, 'Ikiwa una hedhi... unaangalia kama una mimba?'" mwanamke huyo anasema.
Wakati wa ujauzito wake, Briony alitembelea uwanja wa Alton Towers, ambapo alipanda safari zote, alihudhuria sherehe za muziki na alisafiri kwenda Poland, ambayo anaamini ilikuwa wakati alikuwa tayari kujifungua.
Kutokana na mwonekano wa mtoto huyo mwenye mikunjo baada ya kuzaliwa, Briony aliambiwa kwamba huenda binti yake alizaliwa akiwa amechelewa kwa takriban wiki mbili.
"Nilikuwa na maumivu ya mgongo, lakini imekuwa hivyo kila wakati kwa sababu nina urefu wa 180cm na mimi hulala kila siku kwenye kazi yangu, kwa hivyo sikuhisi kama kitu kisicho cha kawaida," anasema.
Tangu wakati huo amejifungua mtoto mwingine.

Chanzo cha picha, Bryony Mills-Evans
Briony hakuwa amemwona babake Willow, Robert Evans, kwa miezi kadhaa kabla ya kuzaliwa kwa msichana huyo.
Kwa sababu hakuwepo wikendi alipojifungua, hakumwambia habari hizo hadi siku chache baada ya binti yao kuwasili bila kutarajia.
"Alifurahi sana - alinipigia simu mara moja na akaja asubuhi iliyofuata," alisema.
"Tulikaa nyumbani siku nzima na kujaribu tu kujua yote ... ilikuwa muhimu kabla ya kuwa tayari kuingia katika ulimwengu wa kweli."

Chanzo cha picha, Wooden Door Photography Photo caption,
Miezi sita baada ya kuwa wazazi, mapenzi ya wenzi hao yalianza upya.
Miaka minne baada ya kuzaliwa kwa Willow, walipata mtoto wao wa pili, Parker Mills-Evans.
Briony anasema ujauzito wake wa pili ulihisi tofauti kabisa.
"Kila kitu nilichokuwa nacho wakati wa ujauzito wangu wa pili, sikuwa na Willow."
Willow sasa ana miaka mitano, na Briony anasema hawezi kufikiria maisha bila mtoto ambaye hakuwahi hata kujua kuwa alikuwa naye.
Imetafsiriwa na Seif Abdalla












