Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ethiopia: 'Jinsi densi katika Tiktok ilivyo hatarisha maisha yangu'
Wakati klipu ya wanaume wawili wakicheza densi kwenye tafrija nchini Ethiopia ilipowekwa kwenye mtandao wa TikTok, iliibua wimbi la chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na hatimaye kumlazimisha mmoja wao kutoraka nchini humo.
Wawili hao hawakujua kwamba walikuwa wakirekodiwa. Hapo awali video hizo zilitumwa kwa Instagram ambapo mtu alichukua picha ya skrini ili kutengeneza chapisho la TikTok ambalo lilisabmbaa kwa kasi.
"Sikutaka kujionyesha [kama mpenzi wa jinsia moja], lakini mitandao ya kijamii iliniondoa," Arnold, ambaye jina lake limebadilishwa ili kulinda utambulisho wake, anaiambia BBC.
"Sasa kila mtu anajua mimi ni nani, na utambulisho wangu wa kijinsia," mwanafunzi huyo wa miaka 20 kutoka Ethiopia anasema.
Mapenzi ya jinsia moja ni kinyume cha sheria nchini Ethiopia na adhabu yake ni kifungo cha kuanzia siku 10 hadi miaka mitatu jela, kulingana na UN.
Arnold anasema kufuchua kuhusu uhusiano wako mapenzi ya jinsia moja kunaweza kuhatarisha maisha yako, ikizingatiwa mwenendo wa majirani
Kisa cha densi iliyobadili maisha kilifanyika Mei katika mji mkuu, Addis Ababa, kwenye hafla ya kijamii, ambapo tamasha la kitamaduni, mashairi na muziki liliandaliwa ili kuwatumbuiza watu wafurahie.
"Tulikuwa tukinywa pombe, tukiwa na furaha. Tulikuwa sisi wenyewe," Arnold anasema.
Siku mbili baadaye ndipo alipogundua kuwa video za hafla hiyo zilikuwa zimeshirikiwa mtandaoni bila idhini yake, mwanzoni na mtu asiyejua hatari zinazoweza kutokea.
"Watu wengi walifanikiwa kuiona kwenye TikTok," anasema.
"Niliogopa sana na nilihisi kutishiwa."
Hakika, siku chache baadaye, Arnold alishambuliwa wakati wa mapumziko yake ya chakula cha mchana: "Nilipotoka kwenye mgahawa kikundi cha wanaume walikuja kwangu na kusema kwamba wameniona kwenye video hiyo na kuniambia nikubali kwamba nilikuwa nikidanganya kuhusu muelekeo wangu wa kijinsia.
"Watu 12 walikuwa wamenizunguka. Kisha wawili kati yao wakaanza kunipiga, nilifanikiwa kukimbia lakini walinikamata tena na kunikanyaga usoni na kunivunja shavu."
Alitumai kuwa hali ingetulia baada ya muda, lakini mnamo Julai, video nyingine ya TikTok ilichapishwa, na ilipata maelfu ya maoni.
Ilikuwa na onyesho lenye picha za watu kutoka kwenye sherehe hiyo, akiwemo Arnold, pamoja na maelezo: "Hawa ni wapenzi wa jinsia moja wanaoishi kwa uhuru nchini Ethiopia."
Ilionekana kama moto usioweza kuzuilika ulikuwa umewashwa: " Hali ilizidi kuwa mbaya, hasa walipojaribu kujua jina langu na anwani yangu.
"Nilikuwa kwenye mitandao ya kijamii. Nilitoroka nyumbani. Zilikuwa siku za kutisha zaidi maishani mwangu, bila shaka wangeniua laiti wangenipata."
Mwezi mmoja baadaye, Ofisi ya Amani na Usalama ya Addis Ababa ilitangaza msako mkali dhidi ya wapenzi wa jinsia moja katika hoteli na baa na kufungua simu ya dharura, na kuwataka umma kuripoti kile walichokiita "vitendo vya kuchukiza".
Baada ya kujificha kwa rafiki, Arnold aliunganishwa na kikundi cha watu watano wenye makao yake Ulaya waliojitolea kuwasaidia wanaoshiriki mapenzi ya jinsia nchini Ethiopia .
Wanajulikana kama House of Guramayle, wanafanya kazi ili kupata fedha na njia salama kwa watu wa LGBTQ+ kutoka Ethiopia na kumsaidia Arnold kuikimbia nchi.
Watu waliojitolea walikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuona mtindo wa video za TikTok zinazowanyanyasa watu na ulaghai wao - uvujaji wa habari za kibinafsi mtandaoni.
Faris Cuchi Gezahegn, ambaye anatumia "wao" na "wao" kama viwakilishi vya kibinafsi na mwanzilishi mwenza wa House of Guramayle, anasema suala la Arnold kutengwa kwenye mitandao ya kijamii ni jambo ambalo Waafrika wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja hukumbana nayo katika maisha yao ya kila siku.
"Kujitokeza kwa ajili yetu, wakati mwingi sio rahisi," anasema Gezahegn kutoka nyumba yao huko Vienna. Walikimbilia Austria baada ya harakati zao za kuunga mkono LGBT+ kuweka maisha yao hatarini.
Mwanaharakati huyo amekusanya video 110 za TikTok mbazo sasa zimefutwa, zikiwemo zile zilizomfichua Arnold.
Baadhi huonyesha watu wakipigwa, teke au ngumi hadharani. Zengine zina picha za watu, wakiuliza majina na anwani zao kwenye maoni.
Katika tukio moja, mchungaji maarufu wa kiinjilisti anatoa wito kwa watu wa LGBTQ+ kuvuliwa nguo na kuchapwa mijeledi hadharani.
Video hizi zilibaki kwenye TikTok kwa wiki kadhaa kabla ya kufutwa, wakati huo zilikusanya maelfu ya maoni.
"Moja ya masuala makubwa ni kwamba maudhui haya yanatayarishwa zaidi, yakiandikwa kwa lugha yetu ya asili, ambayo ni Kiamhara na pia wakati mwingine Afaan Oromoo na Kitigrinya," anasema Gezahegn, akifafanua kwa nini ilichukua muda mrefu kutambuliwa na kuondolewa mtandaoni.
House of Guramayle sasa inafanya kazi na kampuni ya mitandao ya kijamii kuripoti video zinazohimiza vurugu dhidi ya watu wa LGBTQ+ katika lugha hizi.
TikTok ilikataa kuhojiwa kwa ajili ya makala haya lakini ilijibu ombi la BBC kwa miongozo ya jumuiya yake: "Tumejitolea kuhakikisha kwamba sera yetu inazingatia haki na ya usawa, ndio maana tunashirikiana na mashirika ya kimataifa kushauriana nao tunapounda sera mpya, kuimarisha zilizopo na kuunda vipengele vipya vya usalama ambavyo vinaweza kunufaisha jamuiya ya LGBTQ+."
Masuala haya ya unyanyasaji kwenye mtandao wa TikTok hayako Ethiopia pekee.
Celia, anayeshiriki mapenzi ya jinsiamoja nchini Uganda ambaye pia aliomba jina lake libadilishwe kwa ajili ya usalama wake, anasema alikumbana na matukio kama hayo.
Mahusiano ya watu wa jinsia moja yalipigwa marufuku nchini Uganda tangu ilipopata uhuru mwaka 1962.
Lakini mwaka huu, serikali iliidhinisha sheria kali zaidi dhidi ya wapenzi wa jinsia moja - sasa mtu yeyote anayepatikana na hatia ya kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja anakabiliwa na kifungo cha maisha na adhabu ya kifo kwa visa vya " tabia ya kuchukiza", ambayo inaweza kuhusisha ngono na watoto au watu walio katika mazingira magumu.
Baada ya kuripotiwa na jirani yake katika mji mkuu, Kampala, Celia anasema yeye na mpenzi wake walikamatwa: "Waliniambia [polisi]: 'Tukithibitisha kwamba unashiriki mapenzi ya jinsia moja, utafungwa gerezani kwa miaka 20.'"
Wenzi hao walizuiliwa rumande kwa siku mbili. Nyaraka rasmi za kukamatwa zinasema kwamba walishikiliwa kwa washukiwa wa kupatikana na mihadarati.
"Hicho ndicho walichoweka [kwenye faili langu] ili kuniachilia, kwa sababu hawakuwa na ushahidi kwamba nashiriki mapenzi ya jinsia moja," anasema Celia.
Kufuatia kukamatwa kwao, wenzi hao, ambao ni watumiaji wa TikTok, walipokea vitisho vya walipochapisha maudhui kwenye jukwaa hilo. Kwa kuhofia usalama wao, walikimbilia Kenya mwezi Machi.
Baada ya TikTok kukua na kuendelea kupata umarufu barani Afrika, kumekuwa na miito kutoka nchi kwa kadhaa kote barani kudhibiti au kukagua yaliyomo. Mnamo Agosti, Senegal na Somalia zilichukua uamuzi wa kupiga marufuku programu hiyo ya mitandao ya kijamii.
Nchini Senegal ilifungiwa kwa misingi ya kisiasa, baada ya madai kuibuka kwamba ilikuwa ikitumiwa na upinzani kuandaa maandamano. Mamlaka ya Somalia ilisema ilikuwa inatumiwa na makundi ya kigaidi na watu wengine "wanaohusika na kueneza uasherati".
Kenya yenye uhafidhina wa kijamii, mfanyabiashara aliwasilisha ombi bungeni mwezi Agosti akiwataka wabunge kuharamisha TikTok, akionya kuwa baadhi ya maudhui yanaweza kuwa "tishio kubwa kwa maadili ya kitamaduni na kidini nchini Kenya".
Hili lichangia msukumo kutoka kwa watayarishi wa maudhui nchini Kenya ambao waliomba mifumo ya udhibiti izingatiwe badala ya kupiga marufuku moja kwa moja. Mnamo Septemba mwaka huu Rais wa Kenya William Ruto alizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa TikTok Shou Zi Chew ili kuweka vikwazo mbalimbali.
"Maudhui yasiyofaa au ya kuudhi yatafutwa kwenye jukwaa," ofisi ya Rais Ruto ilisema baada ya mkutano huo wa mtandaoni.
Bado licha ya matumizi ya TikTok kuwahangaisha na kuwanyanyasa wanachama wa jumuiya ya LGBTQ+, wale walioathiriwa hawataki ipigwe marufuku.
"Tunakabiliwa na matatizo mengi hapa nje lakini nadhani TikTok itakuwa jukwaa nzuri la kuwafundisha watu wengine sisi ni nani; kwamba hatuna nia ya kumdhuru mtu yeyote," anasema Celia.
"Sisi ni wanadamu tu."
Arnold anakubali. Anatumai siku moja atarejea nyumbani Ethiopia na anajaribu kutumia hali yake kwa njia chanya.
“Nataka kusomea saikolojia na haki za binadamu kwa sababu inanipa msukumo wa kusaidia jamii yangu,” anasema.
"Sitaki mtu yeyote apitie yale niliyopitia."
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi