Je, kuna watu huzaliwa wakimbiaji?

Chanzo cha picha, University of Bath
- Author, Katherine Latham
- Nafasi, BBC
Kwa wengine, kukimbia ni kitu cha kawaida, lakini kwa wengine, kukimbia kwa kasi au masafa marefu wanaweza kuhisi kama vita. Unaweza kujiuliza: Je, nimezaliwa mkimbiaji?
Kukimbia ni moja wapo ya mazoezi maarufu duanini. Nchini Marekani pekee, kuna wakimbiaji wapatao milioni 64 - na idadi ni kubwa kwenye kila nchi ulimwenguni.
Pengine urahisi wa kukimbia ndio hufanya wengi kupenda. Huhitaji chumba cha mazoezi au vifaa vya gharama kubwa. Unaweza tu kuvaa viatu vyako na nguo nyepesi na utoke nje ya mlango na uko tayari kukimbia.
Lakini kipi kinachowatofautisha wale wanaoweza kukimbia haraka sana, na wale wanaokimbia kwa mwendo wa polepole? Kuna ushahidi kuhusu vinasaba.
Wanasayansi wanasema nini?

Chanzo cha picha, Getty images
Wanasayansi wamekuwa wakichunguza kuhusu "jeni ya kasi" kwa zaidi ya miongo miwili sasa, huku kukiwa na ushahidi unaoongezeka kwamba maumbile yako ya kijeni yanaweza kuwa na uhusiano na uwezo wako katika ukimbiaji.
Kuna zaidi ya aina 200 za jeni ambazo zinaweza kuathiri utendaji wako katika michezo na 20 kati ya hizo zinaweza kuchangia mtu kuwa mwanariadha bora.
Ingawa ni muhimu kusema, jeni pekee hazitamgeuza mtu kuwa mwanariadha bora. Kwa kweli, kuna njia nyingi zinazoweza kumfanya mtu kuwa mwanariadha bora.
Njia hizo ni kama mafunzo sahihi na mambo mengine mengi ya kimazingira, lakini kuwa na aina fulani ya jeni kunaweza kuwapa baadhi ya watu uwezo bora zaidi wa kukimbia.
Matokeo ya Utafiti

Chanzo cha picha, Getty Images)
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Misuli ya mifupa imeundwa na mamia, wakati mwingine maelfu, ya nyuzi ambazo zimefungwa pamoja katika tishu.
Nyuzi za Aina ya I, au "slow-twitch" mara nyingi hupatikana kwa wingi kwa wanariadha wa mbio ndefu na waendesha baiskeli.
Wakati huo huo, nyuzi za aina ya II au "fast-twitch" zinapatikana kwa wingi kwa wanamichezo kama vile wanyanyua vyuma na wanariadha wa mbio fupi za kasi.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Exeter nchini Uingereza wamechunguza uhusiano wa jeni katika michezo.
Mwanasayansi Henry Chung na timu yake walichunguza maelfu ya jeni kutoka kwa wanaume na wanawake 45 wa Uingereza wenye umri kati ya miaka 20 na 40. Kwa wiki nane, washiriki walikimbia kwa dakika 30, mara tatu kwa wiki.
"Kwa wiki nane, tuliona uwezo wa kupumua ukiimarika kwa wastani wa 10%. Baadhi ya watu waliimarika kwa 20%, wengine kwa 5% tu. Na wengine uwezo wao haukiimarika hata kidogo," anasema Chung.
"Tuliangalia zaidi ya jeni 3,000 tofauti. Na tukapata jeni 19 zilizojitokeza mara kwa mara. Zote zinahusiana na aina fulani ya mabadiliko ya kuimarika."
"Watu ambao waliimarika kwa karibu 20% walikuwa na jeni zote hizo 19, wakati watu ambao hawakuimarika walikuwa na jeni moja au mbili," anasema.
Kati ya jeni 19 zilizotambuliwa, moja ilikuwa ile inayoitwa" jeni shujaa," inayojulikana kama jeni ya monoamine oxidase A (MAOA), ambayo inahusishwa na tabia ya uchokozi na tabia ya kufanya vitu vya hatari.
"Jeni shujaa hukuruhusu kubadili tabia na fikra, 'ninahitaji kukimbia, ninahitaji kusonga mbele'," anasema Chung.
Lakini utafiti huo uligundua kuwa chini ya 31% ya watu wana muundo wa jeni zinazosaidia katika mazoezi.
Tafiti Nyingine
Lakini zipo tafiti zinazoonyesha maendeleo makubwa ya rekodi za dunia katika kukimbia tangu Olimpiki ya kwanza yamechochewa na maendeleo ya mbinu za mafunzo, pamoja na uboreshaji wa maeneo ya kukimbia na viatu.
Wataalamu wanasema, kwa kutumia mafunzo, unaweza kuwa na uwezo wa kubadilisha nyuzi za misuli yako kutoka mwendo wa polepole hadi kwa haraka. Hili linaleta matumaini kwa sisi ambao tuna changamoto ya kukimbia kwa kasi.
"Kuweza kukimbia haraka ni nguvu kidogo," anasema Steffi Colyer, mtaalamu wa nishati ya mwili kutoka Chuo Kikuu cha Bath, Uingereza.
"Lakini ni lazima uweze kutumia nguvu kubwa sana kuzidi uzito wa mwili. Ikiwa unataka kukimbia kwa kasi, ni lazima utumie nguvu."
Ili kudumisha kasi yako ya juu kwa muda mrefu iwezekanavyo, anasema Colyer, unahitaji kuamsha misuli yako na kuzalisha nguvu. Unakuwa ni mchanganyiko wa uimara, nguvu na mbinu.
Faida za Kukimbia

Chanzo cha picha, PACE Sports Management
ili kukimbia haraka, Mageean anashauri kukimbia milimani wakati wa mafunzo yako: "Jaribu kukimbia juu ya kilima haraka uwezavyo. Rudi chini ya mlima. Kisha upande tena."
Wakati unafanya hivyo, zingatia umbo lako, anasema Mageean. "fikiria mtu ana kamba iliyounganishwa kwenye kifua chako, na anaivuta kwa kwenda mbele, na kamba inakuvuta juu ya kilima."
Mageean pia anakushauri kubadilisha kasi yako, kwa hivyo ongeza kasi yako ya mbio kwa kila hatua. Mageean anasema, "ndipo unapokimbia kwa kusema dakika tatu [haraka], dakika moja [polepole], na kurudia."
Kuna faida nyingi za kukimbia. Kukimbia kuna faida kwa moyo wako na mifupa yako. Inaweza kuboresha afya yako ya akili, na kukusaidia kuishi muda mrefu zaidi.
Utafiti unaonyesha "kukimbia polepole kunaweza kuwa na manufaa zaidi kuliko haraka, kupunguza hatari ya kuumia, na husaidia kuongeza uwezo wako wa kupumua na hatimaye kasi yako .
Mageean anatoa pongezi kwa wale ambao hawana uwezo wa kuzaliwa, lakini wana nidhamu ya mafunzo. "Ninajua wanariadha wengi wenye vipaji ambao wana chembechembe za urithi, lakini hawana mawazo ya kusalia katika mchezo huo," anasema.
"Kwa hivyo, ninaheshimu sana wale ambao labda hawana bahati na kile walichozaliwa nacho, lakini wanajitahidi sana kujiimarisha wao wenyewe."
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah












