Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wagner Afrika: Mustakabali usioeleweka baada ya kifo cha Prigozhin
- Author, Dkt. Alex Vines
- Nafasi, Chatham House
Akiwa amebeba bunduki na kuvalia mavazi ya kijeshi katika jangwa, Yevgeny Prigozhin alikuwa na ujumbe kwa Afrika. Kundi lake la Wagner, "linaifanya Urusi kuwa kubwa zaidi katika kila bara - na kuifanya Afrika kuwa huru Zaidi. Haki na furaha kwa mataifa ya Afrika," alieleza.
Video hiyo, inayodhaniwa kurekodiwa nchini Mali, ilitolewa Jumatatu. Siku mbili baadaye, kiongozi wa Wagner aliripotiwa kufariki katika ajali ya ndege nchini Urusi. Wagner imekuwa ikifanya kazi katika nchi kadhaa Afrika - haswa Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Mali.
Wakati wa kilele cha Vita Baridi, na hasa muda mfupi baada ya uhuru wa mataifa ya Afrika, mamluki walitumiwa mara kwa mara Afrika kushawishi vita vya wenyewe kwa wenyewe na kuchochea vurugu.
Kanali Callan huko Angola; Bob Denard huko Congo na baadaye Comoro; Mad Mike Hoare huko Congo na baadaye Shelisheli; Mmarekani Robert Mackenzie nchini Sierra Leone na Mwingereza Simon Mann nchini Equatorial Guinea mwaka wa 2004.
Nilipomjadili Prigozhin na wachambuzi wa siasa za Afrika na Urusi, huko Moscow mwishoni mwa 2019, walinikumbusha kwamba Prigozhin alikuwa sawa na mtawala wa kibeberu wa Uingereza Cecil Rhodes, ambaye alikuwa anataka tu kupata utajiri.
Ushawishi wa Prigozhin Afrika ulijengwa juu ya damu na mali - mikataba ya kutoa rasilimali muhimu ilifanywa kwa malipo ya msaada wa kijeshi. Nilishuhudia Kampuni za Kijeshi zikifanya kazi miaka zaidi 20 iliyopita: Sandline International nchini Sierra Leone. Walitoa ulinzi na mafunzo kwa malipo ya usimamizi wa migodi, mafuta na rasilimali nyingine.
Hakuna kitu cha kipekee kuhusu Wagner na namna inavyojiendesha Afrika. Nilipokutana na baadhi ya wapiganaji wa Wagner huko Moscow mwaka 2019, walikuwa na hamkani wakati wakitafuta fidia kwa operesheni iliyokwenda vibaya nchini Msumbiji.
Operesheni za Wagner nchini Libya, Sudan, Mali na CAR zimetoa matokeo mseto. Mafanikio makubwa zaidi ya kijeshi ya Wagner pengine ni kufanya kazi ya ulinzi wa viongozi wa juu na kuzuia mapinduzi ya kijeshi katika mji mkuu wa CAR, Bangui.
Operesheni walizoshindwa ni ikwemo ya Msumbuji. Wagner walitumwa Septemba 2019 kwa operesheni za kukabiliana na waasi, lakini mauaji ya wapiganaji wake saba na wanajeshi 20 wa Msumbiji Oktoba, wakati wa mapigano ya kimakosa yalisababisha Wagner kujiondoa mapema 2020.
Wagner na maslahi yake Afrika
Uwekezaji wa Wagner katika habari za uongo na kukang’anya, zinazochochea hisia za chuki dhidi ya Magharibi, umekuwa na mafanikio makubwa. Kwa sasa inaendesha shughuli nyingi za kijeshi nchini Sudan na Mali. Wagner wamekuwepo nchini Sudan tangu 2017, wakitoa huduma za usalama na kusimamia makubaliano ya uchimbaji dhahabu.
Idara ya Hazina ya Marekani inadai kuwa Wagner pia imekuwa ikivipatia Vikosi vya Msaada wa Haraka vya Sudan makombora ya kutoka ardhini na kushambulia angani hivi karibuni.
Septemba 2021, viongozi wa kijeshi Mali walifikia makubaliano ya usalama na Wagner na kutumwa wapiganaji 1,000 kwa gharama ya kila mwezi ya dola za kimarekani milioni 10.8. Utendaji wa Kundi la Wagner dhidi ya ugaidi umekuwa duni na kuna madai ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu huko Mali.
Ingawa kutumwa kwa kundi hilo nchini Mali kumezusha ukosoaji kutoka Umoja wa Afrika (AU), Wagner bado inataka kupanua shughuli zake hadi Burkina Faso.
Ofa ya mwishoni mwa 2022 ilikataliwa, lakini Urusi inaendelea kuwashawishi watawala, ambao kiongozi wao Kapteni Ibrahim Traore alihudhuria mkutano wa pili wa Urusi na Afrika huko St Petersburg Julai mwaka huu.
Burkina Faso ni mojawapo ya nchi sita za Afrika kupokea nafaka za bure kutoka Moscow. Mara tu baada ya mapinduzi ya Septemba 2022 nchini Burkina Faso ambayo yalisababisha Capt Traore kuchukua serikali ya kijeshi, Prigozhin alimtaja kama "shujaa wa Afrika."
Wagner itaendelea kuwepo Afrika?
Kiongozi wa Wagner pia alisifu mapinduzi ya kijeshi ya Niger mwezi Julai mwaka huu kuwa habari njema na kutoa ofa kuwa wapiganaji wake watasaidia kuleta utulivu. Lakini kutokana na uasi wake ulioshindwa nchini Urusi mwezi Juni, operesheni zake Afrika zilikuwa hatarini.
Kwa mujibu wa Rais Vladimir Putin, Prigozhin alikuwa amerejea Urusi kutoka Afrika siku ya kifo chake na alikuwa amekwenda kukutana na maafisa wa Urusi mjini Moscow. Putin alimuelezea Prigozhin, "alifanyakazi katika nchi yetu, lakini pia nje ya nchi, barani Afrika.’’
Ukosoaji wa wanamajumui wa KiAfrika kuhusu mamluki ulianza mara tu walipoanza kushiriki kuondoa ukoloni katika miaka ya 1960. Mnamo 1977, Mkataba wa Afrika na Mamluki ulitiwa saini huko Libreville na ulianza kutekelezwa Aprili 1985.
Mikataba hii inaweza kukosa ufanisi, na serikali nyingi za Afrika hazitaki kurudiwa kwa matumizi ya mamluki wa kigeni katika ardhi ya Afrika na kuendeleza ushindani wa mataifa ya nje ambao ulitokea wakati wa Vita Baridi.
Msumbiji iligundua kuwa utumiaji wa wakandarasi wa kijeshi wa kibinafsi haukuwa mzuri na ikageukia Rwanda kwa usaidizi. Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alihitimisha kwamba jeshi lenye ufanisi na lenye nidhamu lilihitajika kusaidia vikosi vyake vya kijeshi, na Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) limefanikiwa, na kupunguza kwa kiasi kikubwa uasi.
Hali mbaya ya usalama katika eneo la Sahel kulisababisha Rais wa Nigeria Bola Tinubu, pamoja na washirika wa Afrika Magharibi, kuandaa mipango ya kuimarisha kikosi cha kikanda - kupambana na ugaidi na kupambana na mapinduzi.
Lakini kwa serikali za kijeshi katika eneo hilo, Mali, Burkina Faso na sasa Niger, wahudumu wa Urusi wanaweza kuwa mbadala wa kuvutia. Wagner, ikiwa itasalia, au vikundi vingine vya mamluki vya Urusi vinavyoibuka, vitazidi kupata soko kwa serikali zinazowatumia kama washirika wa usalama.
Huu ni wakati wa viongozi wa Afrika kutekeleza kiukweli suluhu za Kiafrika kwa matatizo ya Afrika, kwa kutekeleza mikataba yake na kujenga taasisi na vikosi vya usalama vinavyoaminika, vinavyowajibika.