Wanasayansi wagundua kwa mara ya kwanza tembo wakiwazika na kuwafanyia tambiko watoto wao waliokufa

Wanadamu sio viumbe hai pekee ambao wana matambiko ya kushughulikia kifo.

Wanyama wengine pia huonesha tabia fulani wakati mmoja wao anapokufa.

Mfano wa hawa ni tembo wa Asia, na kutokana na utafiti mpya ibada hizi zilipigwa picha kwa mara ya kwanza.

Ugunduzi huo pia unaonesha kuwa tembo hubeba maiti za watoto wao kwa siku kadhaa hadi wapate mahali pazuri pa kuzikia, huku wakitoa vilio kutoka kwenye mikonga yao.

Katika utafiti uliofanywa kati ya mwaka 2022 na 2023, Akashdeep Roy wa Taasisi ya Elimu ya Sayansi na Utafiti huko Pune na Parveen Kaswan wa Huduma ya Misitu ya India alipata matukio matano vya kuzikwa kwa watoto wa tembo.

Matukio hayo yalirekodiwa huko Bengal, kaskazini mashariki mwa nchi, na, kulingana na wanasayansi, hakuna wanadamu waliohusika.

"Mazishi ya watoto wachanga ni matukio adimu sana katika maumbile," Roy aliliambia jarida la New Scientist.

Jambo la pamoja

Nyayo na kinyesi kilichoachwa njiani ambazo watafiti walizipata kwenye makaburi hayo matano zinaonesha kuwa tembo wa rika zote walichangia kila maziko.

Hii, kulingana na ripoti, ni ushahidi wa "tabia ya huruma na msaada" iliyooneshwa na washirik.

Maiti zote zilipatikana katika nafasi sawa, zikiwa zimezikwa kwenye mifereji ya maji iliyofunguliwa na wakulima na kufunikwa na ardhi na miguu yao juu.

"Ni nafasi inayofikika zaidi ya kushikilia na kuweka maiti kwenye mitaro," Roy alielezea tovuti ya Live Science portal.

"Nafasi hii pia inaruhusu zaidi ya mwanachama mmoja kushiriki katika mchakato wa mazishi."

Baada ya maziko, wakulima waliohojiwa walidai kuwa walisikia tembo wakipiga tarumbeta ya mikonga yao.

Roy anaamini kwamba sauti hizi zilipaswa "kuonesha uchungu na maumivu" na pia "kutoa heshima kwa viumbe vilivyokufa."

Kwa nini watoto wachanga pekee hupokea matibabu haya wanapokufa? Kwa sababu "haifai" kusafirisha na kisha kuwazika vijana wazima au watu wazima, kutokana na ukubwa na uzito wao, uchunguzi unaeleza.

Tafiti za awali zilifichua kwamba tembo wa Asia huomboleza kama familia, mtafiti wa Taasisi ya Sayansi ya India Raman Sukumar aliambia jarida la National Geographic.

Vivyo hivyo, waliona kwamba wanyama hao waliitikia huzuni kwa kuwabembeleza na matendo mengine ya upendo.

Mbali na wanadamu

Tayari ilikuwa imeonekana kwamba tembo wa Kiafrika hufanya ibada ya mazishi, wakiwafunika watoto wao kwa matawi na majani, lakini utafiti huu na tembo wa Asia ni rekodi ya kwanza ya tembo kuweka miili katika nafasi maalum na kuizika kwa udongo, ripoti Live Science .

Tembo wa Asia hawaziki watoto wao popote pale.

Pachyderm huchagua "mahali pa pekee, mbali na wanadamu na wanyama wanaokula nyama , huku wakitafuta mifereji ya maji na mifereji ya kuzika maiti," ripoti hiyo inasema.

Miili hiyo mitano iliyofanyiwa utafiti ilipatikana katika maeneo yanayolima chai, mbali na maeneo yenye watu wengi.

Wanasayansi waliifukua miili hiyo ili kuifanyia uchunguzi na kugundua kuwa ilikuwa na umri wa kuanzia miezi 3 hadi mwaka, na baadhi yao walikuwa na utapiamlo au walikuwa na maambukizi.

Michubuko iliyopatikana kwenye migongo ya kila mtoto wa tembo inaonesha kwamba waliburutwa kwa umbali mrefu hadi kwenye maeneo ya kuzikia.

"Kuna ripoti ambazo hazijachapishwa kutoka Idara ya Misitu ya Bengal Magharibi ya tembo jike kubeba mzoga kwa hadi siku mbili kabla ya kuutelekeza katika eneo lililojitenga huko Bengal Kusini," ripoti hiyo inaeleza.

“Viumbe hao wenye hisia hawaachi maiti hadi uchakavu uanze au hadi maafisa wa Idara ya Misitu wachukue jukumu la kuisimamia maiti,” iliongeza.

Tofauti na tembo wa Kiafrika, tembo wa Asia hawarudi kwenye eneo la kuzikia, bali huchagua njia nyingine mbadala za kusafiri.

Tafsiri ya kwanza ya matokeo

Kwa mwanabiolojia na mhifadhi Chase La Due, utafiti huo ni muhimu, kwa sababu unatoa "ushahidi wa kushangaza wa matatizo ya kijamii ya tembo," alisema mwanabiolojia Chase La Due, anayefanya kazi katika Zoo, katika mahojiano na gazeti la New Scientist. na Oklahoma City Botanical Garden, USA.

"Wengine wamebaini kuwa tembo wanaonekana kuwa na tabia ya kipekee kwa ndugu zao waliofariki, (lakini) utafiti huu ni wa kwanza kuelezea kile kinachoonekana kuwa ni utaratibu na wa makusudi wa kuzikwa watoto wa tembo baada ya kuletwa kwenye eneo la kuzikwa," Alisema LaDue.

Zaidi ya hayo, mtaalamu alitoa wito wa tahadhari wakati wa kutafsiri matokeo haya.

"Maisha ya kiakili na kihisia ya tembo bado kwa kiasi kikubwa ni fumbo," alisema.

Mwanabiolojia huyo anaeleza kuwa aina hizi za tafiti zinaweza kuruhusu uundwaji wa mikakati mipya ya kuhakikisha uhai wa wanyama hawa.

Tembo wa Asia, ambao huishi kwa wastani kati ya miaka 60 na 70 porini, wako kwenye orodha ya viumbe vilivyo hatarini kutoweka iliyotengenezwa na Muungano wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira.

Inakadiriwa kwamba kwa sasa takribani vielelezo 26,000 huishi porini, hasa nchini India na baadhi ya nchi nyingine za Kusini-mashariki mwa Asia.

Imetafsiriwa na Lizzy Masinga na kuhaririwa na Ambia Hirsi