Unajua taarifa zako sasa kuhifadhiwa mwezini? Wanasayansi wanajenga Vituo maalumu huko

Chanzo cha picha, Intuitive Machines
- Author, Emma Woollacott
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Stephen Eisele ana uhakika kwamba siku moja kampuni yake itafungua kituo cha kuhifadhi data huko angani katika mwezi.
"Kwa kuweka kituo cha data angani, kunakuwa na usalama usio na kifani," anasema rais wa kampuni ya Lonestar Data Holdings.
Vituo vya kuhifadhi data ni vituo vikubwa ambavyo huhifadhi rundo la kompyuta zinazohifadhi na kuchakata data zinazotumiwa na tovuti, makampuni na serikali.
Lonestar anasema kuviweka vituo hivi kwenye Mwezi kutawapa wateja usalama wa kuaminika wa data zao, na uwepo wa fursa ya nishati ya jua.
Vituo vya kuhifadhi data kwenye anga za juu vinaweza kuonekana kuwa ni wazo gumu. Lakini kuna uhitaji mkubwa wa hilo kutokana na ugumu wa kupata maeneo yanayofaa duniani.
Uhitaji unaongezeka

Chanzo cha picha, Hugh Kenny
Matumizi yanayozidi kuongezeka ya akili mnemba (AI) katika kompyuta, yanaongeza kiasi cha data zinazohitaji kuhifadhiwa na kuchakatwa kote ulimwenguni.
Kwa hiyo, hitaji la vituo vya data limeongezeka pia, huku mahitaji ya kila mwaka yakitarajiwa kupanda kati ya 19% na 22% ifikapo 2030, kulingana na kampuni ya ushauri ya kimataifa ya McKinsey.
Vituo vipya vinachipuka kila muda - lakini inakuwa vigumu kupata mahali pa kuviweka. Vituo vya data ni vikubwa, na hutumia kiasi kikubwa cha umeme na maji kwa ajili ya kupozea.
Na watu hawataki vijengwe karibu na makazi yao.
Kuweka vituo vya kuhifadhi data angani - ama katika obiti kuzunguka dunia, au mwezi - inamaanisha haviwezi kuleta madhara mengi. Kuna nishati isiyo na kikomo inayopatikana kutoka katika jua, na hakuna majirani wa kulalamika kuhusu athari za mazingira.
Si hivyo tu, vituo vya data vya angani vinaweza kutoa huduma kwa vyombo vya angani na vifaa vingine vya anga, na uhamishaji wa data kutoka vituo hivyo hadi kwenye vyombo vya angani utakuwa wa haraka kuliko kutoka ardhini.
Changamoto

Chanzo cha picha, Starcloud
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Licha ya matumaini kutoka kwa makampuni yanayolenga kuendeleza teknolojia hiyo, Dk Domenico Vicinanza, profesa wa mifumo ya akili na sayansi ya data katika Chuo Kikuu cha Anglia Ruskin nchini Uingereza, anasema kuna changamoto nyingi kabla ya vituo hivyo vya angani kuwa pendekezo linalofaa.
"Hata kwa mchango na maendeleo ya kampuni kama SpaceX, kuweka vituo hivyo kwenye obiti ni gharama kubwa sana," anasema. "Kila kilo inayotumwa angani inagharimu maelfu ya dola.
"Vituo vya data vya angani havitahitaji vifaa vya data pekee bali pia miundombinu ya kuvilinda, kuwasha na kupoza. Yote haya yanaongeza gharama na utata."
Kupoza vifaa hivyo itakuwa changamoto fulani, ingawa angani kuna baridi, mifumo ya kawaida ya kupoza haifanyi kazi bila mvuto wa graviti.
Wakati huo huo, hali ya hewa ya anga inaweza kuharibu vifaa vya kielektroniki, na idadi inayoongezeka ya mabaki ya vifaa vya angani itaviweka vituo hivyo hatarini.
Dk Vicinanza anaongeza: "Na kurekebisha matatizo katika obiti ni changamoto kubwa. Hata kwa roboti na mifumo ya automatiki, yote hiyo ina mipaka juu ya kile inachoweza kukirekebisha.
"Ikiwa kutakuwa na maharibiko makubwa, kutahitaji binaadamu kwenda, safari hiyo inaweza kuchukua wiki au miezi."
Bado makampuni kama Lonestar yanajiamini sana, na yanasema yanaitikia mahitaji yalivyo. "Tusingetaka kufanya hivi, kama wateja wasingetuomba," wanasema.
Umbali kutoka duniani hadi katika mwezi unatoa ulinzi – ni vigumu sana kudukua, na ni vigumu zaidi kufikia. Umbali wa kutoka mwezini inamaanisha kuwa data inachukua kama sekunde moja na nusu kufika ardhini.















