Marekani inataka kuzungumza na Korea Kaskazini lakini haijui ni kwa jinsi gani

Kwa miongo kadhaa, Magharibi – hasa Marekani – imekuwa ikijiuliza swali: inawezaje kutatua tatizo kama Korea Kaskazini?

Sasa hili linaweza kuwa la dharura zaidi kuliko hapo awali kwani tawala za Kim Jong Un na Vladimir Putin zilizowekewa vikwazo vikali zinaingia katika kile kinachoonekana kuwa enzi mpya ya urafiki.

Lakini Marekani, inaonekana kuumiza kichwa chake, ikitafakari namna ya kukabiliana na hili.

Maelezo ya makubaliano yoyote ambayo Moscow na Pyongyang wanaweza kuwa wamefikia ni machache, lakini wasiwasi mkubwa ni juu ya uwezekano wa Urusi kugawana teknolojia, haswa inayohusisha makombora ya balistiki au mifumo ya nyambizi ya nyuklia.

Kufikia sasa Washington imejibu kwa maneno ya kejeli - Bw Putin anatapatapa "akiomba" taifa la asiyekubalika msaada, na alilazimika kusafiri " kwa unyenyekevu " kote nchini mwake - na maonyo ya madhara makubwa, na ambayo bado hayajabainishwa.

Lakini hakuna mengi yaliyosalia katika uchumi wa Marekani ili kushawishi Korea Kaskazini.

Kwa hivyo ni jinsi gani Rais Joe Biden, ambaye amekuwa na shughuli nyingi za kujenga ushirikiano ili kukabiliana na China, anaweza kumleta mezani kiongozi huyo wa Korea Kaskazini?

Fusra zilizopotea kati ya Marekani na Korea Kaskazini

Wakati wa ziara yake mjini Seoul Mei mwaka jana, Rais Biden aliulizwa na wanahabari iwapo alikuwa na ujumbe wowote kwa Bw Kim. Alijibu: "Halo. Mwisho."

"Ikiwa Bw Biden alikuwa tayari kwa mazungumzo, kama Wizara ya Mambo ya Nje inavyoonekana kupendekeza, hii ilikuwa njia ya kuchekesha ya kujibu," alisema Frank Aum, mtaalam wa Asia ya kaskazini-mashariki kutoka Taasisi ya Amani ya Marekani.

Anasema hii ilikuwa fursa nyingine iliyopotea: "Msururu wa makosa na fursa zilizopotea kwa pande zote mbili katika miongo saba iliyopita kwa jumla kulisababisha hali ngumu tuliyo nayo leo."

Bw Kim anaweza kuonekana kutokuwa na haja. Hajajibu ofa ya sasa ya Marekani ya kushiriki katika mazungumzo popote pale na wakati wowote.

Lakini pia amejitahidi kadiri awezavyo kuthibitisha kuwa yeye ni tishio asiyeweza kupuuzwa huku akiendelea kutengeneza silaha zake za nyuklia.

Amefanya majaribio zaidi ya mara 100 ya makombora tangu 2022 na amejaribu mara mbili, na kushindwa, kurusha satelaiti ya kijasusi - yote haya akiwa chini ya vikwazo vikali zaidi kuwahi kuwekewa serikali yake.

"Nadhani Marekani ilipuuza jinsi Korea Kaskazini ilivyokuwa imara na ilivyodhamiria kukabiliana na shinikizo la kimataifa," Bw Aum alisema.

"Watu wengi katika tawala tofauti pengine walilitaja suala la Korea Kaskazini kama suala la usalama la ngazi ya tatu na hawakulipa kipaumbele lililohitaji, ama kwa sababu ni nchi ndogo au mara kwa mara ilionekana kuwa karibu kuporomoka."

Wataalamu wanaamini kuwa hii ilimweka Bw Kim chini zaidi katika orodha ya kipaumbele kuliko vile angependa.

Hatari inayoonekana kutoka Beijing "inazidi hatari kutoka Pyongyang", kulingana na Christopher Greene, mchambuzi wa Kikorea wa Crisis Group.

"Nadhani Marekani imeamua tu kwamba mkakati wa kuzuia na kudhibiti ni bora zaidi kwao kutumia. Na ninaweza kuelewa kwa nini. Tuko katika hali ambayo Korea Kaskazini inaweza kutegemea Urusi na China zaidi kuliko ilivyokuwa miongo iliyopita.

Lakini Marekani ina nini hasa ambacho Korea Kaskazini ingejibu?"

Anasema "diplomasia ya ubunifu ingekaribishwa", lakini anaongeza, "Sidhani kama kuna njia ya kusonga mbele kwa sasa".

Ghadhabu kali na urafiki

Mnamo mwaka wa 2017, Pyongyang ilidai kuwa ilifanikiwa kuunda bomu ndogo ya haidrojeni iliyotengenezwa kutoshea ndani ya makombora yake - hatua kubwa katika matarajio yake ya nyuklia.

Kisha Rais wa Marekani Donald Trump aliitishia Korea Kaskazini kwa " ghadhabu kali ambayo ulimwengu haujawahi kuona", na kuongeza mvutano.

Bw Kim kisha akatangaza kuwa ana silaha kamili za nyuklia na kitufe kwenye meza yake - tishio baya ambalo alitarajia kujikweza ili kupata afueni kutokana na vikwazo.

Hatimaye Bw Trump alimpa ofa ya kufanya mazungumzo ambayo hayajawahi kushuhudiwa na wawili hao walisalimiana kwa mara ya kwanza Singapore mnamo Juni 2018.

Ingawa hii inaweza kuhesabiwa kama "diplomasia ya ubunifu", viongozi wote wawili walionekana kufika kwenye mikutano mitatu waliyokuwa nayo - huko Singapore, Hanoi na mpaka wa Korea – wakiwa hawajajiandaa vizuri kufanya majadiliano.

Lakini mikutano hiyo ya kilele ilibadilisha diplomasia kati ya Korea Kaskazini na Marekani.

Beijing mhusika mkuu

Tangu mkutano wa kilele wa Trump na Kim, China bila shaka imeibuka kama wasiwasi mkubwa kwa Washington.

Bw Biden na utawala wake wamefanya msukumo mkubwa wa kidiplomasia barani Asia - kutoka kuanzisha tena mazungumzo ya ngazi ya juu na China, hadi kuimarisha ushirikiano na kuongeza ushawishi wao katika eneo hilo.

Lakini inaonekana kuwa imekuja kwa gharama ya kupuuza Korea Kaskazini kwa muda mrefu sana - na kufikia hatua ambayo inaonekana hakuna njia za kidiplomasia.

Wakati huo huo Beijing, ambayo bado ina uhusiano na Moscow na Pyongyang, pia ni mhusika muhimu katika hesabu za Marekani kuhusu Korea Kaskazini.

Inapenda utulivu katika kanda.

Ushirikiano mkubwa kati ya Urusi na Korea Kaskazini unaweza kuleta mali nyingi zaidi za kijeshi za Marekani katika Asia ya Mashariki, jambo ambalo Beijing haitataka.

Bw Xi pia amejaribu kujiweka kama mtunza amani duniani, na ameelezea suluhu la China kwa vita nchini Ukraine.

Hangetaka kuonekana akiunga mkono Pyongyang au Moscow katika juhudi zozote zinazoweza kurefusha vita hivyo.

Kwa upande mwingine, China inaweza pia kuona muungano wa Urusi na Korea Kaskazini kama njia ya kukabiliana na ushawishi wa Marekani barani Asia.

"Naweza kufikiria taarifa nyingi kuhusu uwezekano wa uhusiano wa Korea Kaskazini, China na Urusi zinaweza kuzunguka simulizi ya "Vita Baridi" mpya," Bw Green alisema, lakini akapuuzilia mbali kuwa ni "kurahisisha kupita kiasi".

"Ninashuku kuwa Kim Jong Un angependa kubadilisha uhusiano wake na kuiweka China na Urusi dhidi ya kila mmoja ili kupata kile anachohitaji," aliongeza.

"Kile ambacho Marekani inahitaji kufanya sasa ni kuangalia ni fursa gani ambazo inaweza kuwapa."