Je, muungano wa Urusi na Kim Jong Un unatia wasiwasi kwa kiasi gani?

Mpango wa kuzuru Urusi mwezi huu wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un umezusha wasiwasi miongoni mwa Marekani na washirika wake.

Yeye na Rais Vladimir Putin wananuia kujadili uwezekano wa Korea Kaskazini kuipa Moscow silaha ili kusaidia vita vyake nchini Ukraine, maafisa wa Marekani wanasema.

Kwa nje, makubaliano ya silaha kati ya Korea Kaskazini na Urusi yana maana kubwa kibiashara.

Moscow inahitaji sana silaha, haswa risasi na makombora, kwa vita vya Ukraine, na Pyongyang ina silaha nyingi kama hizo.

Kwa upande mwingine, Korea Kaskazini iliyokabiliwa na njaa inahitaji pesa na chakula. Zaidi ya miaka mitatu ya kufungwa kwa mpaka, bila kusahau kuvunjika kwa mazungumzo na Marekani mnamo 2019, kumeiacha nchi hiyo kutengwa zaidi kuliko hapo awali.

Lakini chini ya sakafu, inafungua uwezekano wa Pyongyang na Moscow kuanza kufanya kazi kwa karibu zaidi. Marekani imekuwa ikionya juu ya uwezekano wa makubaliano ya silaha kati ya nchi hizo mbili kwa muda, lakini mkutano wa ngazi ya juu wa viongozi wa mataifa hayo mawili Kim Jong Un na Vladimir Putin unafanya mpango huo kuwa na uwezekano mkubwa.

Wakati kipaumbele kwa Marekani, kwa muda mfupi, inaonekana kuwa kuzuia silaha za Korea Kaskazini kufika mstari wa mbele nchini Ukraine, wasiwasi hapa Seoul ni juu ya kile Korea Kaskazini itapata kwa ajili ya kuuza silaha zake kwa Urusi. .

Huku Urusi ikiwa katika hali ya kukata tamaa, Bw Kim huenda akafaidika zaidi.

Labda angeweza kudai msaada wa kijeshi kutoka kwa Urusi. Jana, idara ya ujasusi ya Korea Kusini iliarifu kwamba Bw Shoigu alipendekeza Urusi, China na Korea Kaskazini kufanya mazoezi ya pamoja ya jeshi la majini, sawa na yale yaliyofanywa na Marekani, Korea Kusini na Japan, ambayo Kim Jong Un anachukia sana.

Bw Kim anaweza kuomba silaha za Urusi katika siku zijazo.

Lakini kwa sasa kinachotia wasi wasi ni kwamba huenda Kim anaweza kumuomba Putini silaha za kisasa na usadizi wa teknolojia, pamoja na ujuzi kumsadia kufanikiwa katika mipango yake ya kutengeneza silaha za kisasa za kinyuklia.

Kim bado anatatizika kumiliki silaha muhimu za kimkakati, haswa satelaiti ya kijasusi na nyambizi yenye silaha za nyuklia.

Hata hivyo maafisa wa Seoul wanaamini ushirikiano katika ngazi hii hauwezekani, kwani unaweza kuishia kuwa hatari kimkakati kwa Urusi.

Yang Uk, mtafiti katika Taasisi ya Asia ya Mafunzo ya Sera, alibainisha kuwa hata iwapo Urusi haitazuia silaha za Korea Kaskazini, bado inaweza kufadhili mpango wake wa nyuklia. "Iwapo Urusi inalipa mafuta na chakula, inaweza kufufua uchumi wa Korea Kaskazini, ambao kwa upande mwingine unaweza kuimarisha mfumo wa silaha wa Korea Kaskazini. Ni chanzo cha ziada cha mapato kwao ambacho hawakuwa nacho."

Bw Yang, mtaalamu wa mikakati ya kijeshi na mifumo ya silaha, aliongeza: "Kwa miaka 15 tumejenga mtandao wa vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, ili kuizuia kutengeneza na kufanya biashara ya silaha za maangamizi makubwa. Sasa Urusi, mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inaweza kusababisha mfumo huu wote kuporomoka."

Huku vikwazo vikiongezwa, Korea Kaskazini imezidi kutegemea China kuwafumbia macho wale wanaokiuka vikwazo na kuipatia chakula cha msaada.

Kwa mwaka uliopita Beijing imekataa kuiadhibu Korea Kaskazini kwa majaribio yake ya silaha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kumaanisha kuwa imeweza kutengeneza silaha zake za nyuklia bila kuadhibiwa.

Nafasi ya Korea Kaskazini Kijiografia inaifanya nchi hiyo kama kinga kwa Beijing dhidi ya vikosi vya Marekani vilivyoko Korea Kusini, na huenda China inajeresha mkono

Lakini Pyongyang daima imekuwa na wasiwasi kuhusu kuitegemea China pekee. Huku Urusi ikiwa katika kuwatafuta washirika wapya, inampa Bw Kim fursa ya kuongeza mtandao wake wa usaidizi.

Na huku Urusi, ikihitaji silaha mno, kiongozi wa Korea Kaskazini huenda akatumia mwanya huo ili kupata manufaa zaidi kutoka kwa Moscow kuliko Beijing.

Putin huenda akaridhia majaribio ya silaha za nyuklia ya Korea Kaskazini lakini kwa upande mwingine, hatua hiyo inaweza kumghadhabisha rais wa China Xi Jinping.

"Wakati wa Vita Baridi, Korea Kaskazini ilikuwa ikilicheza taifa la Urusi kwa kuitumia China , sawa na jinsi watoto wanavyowachezea wazazi wao kwa wao," Dkt. Bernard Loo wa Shule ya Kimataifa ya S Rajaratnam huko Singapore alisema.

Lakini bado kuna alama ya kuuliza ikiwa mkutano huo utaendelea.

Ni nadra kwa Kim kusafiri kutoka nje ya Korea Kaskazini na haondoki nchini humo ispokuwa kwa mada kuu na muhimu. Anajali sana kuhusu usalama wake na ana mtizamo kwamba safari nje ya nchi yake zinaweza kutia hatarini maisha yake.

Kwa safari zake za mwisho za kimataifa - kwenda Hanoi kukutana na Donald Trump mnamo Februari 2019, na kukutana na Bw Putin huko Vladivostok mnamo Aprili 2019 - alipanda treni ya kivita. Safari ya kwenda Hanoi ilichukua siku mbili ndefu kupitia China.

Haijulikani ni jinsi gani viongozi hao wawili walikusudia mkutano wao uwe wa faragha, lakini inawezekana Marekani inatumai kwamba kwa kuiweka hadharani, inaweza kumtisha Bw Kim na hivyo kukwamisha mkutano huo na mpango wa silaha unaowezekana.

Dkt Loo hafikirii Bw Kim angekuwa na nafasi kubwa ya kutetereka, hata hivyo: "Kwa kuzingatia ripoti kuhusu mazoezi ya kijeshi ya pande tatu, itakuwa vigumu kughairi matukio ya aina hii bila kila mtu kuishia na yai usoni."

Sehemu ya mkakati wa Marekani tangu uvamizi wa Urusi nchini Ukraine imekuwa kutoa taarifa za kijasusi ili kujaribu kuzuia makubaliano kutokea.

Korea Kaskazini na Urusi hadi sasa zimekanusha kila pendekezo wanalotoa kwamba wanataka kufanya biashara ya silaha. Wala hawataki mpango huu kuwa jambo la umma.