Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mkutano wa kilele wa Nato utakuwa kuhusu maswali magumu juu ya matumizi ya ulinzi
- Author, Katya Adler
- Nafasi, Mhariri wa Ulaya
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Wakati ulimwengu ukishusha pumzi baada ya Marekani kutangaza usitishwaji vita kati ya Israel na Iran, Rais wa Marekani Donald Trump amewasili nchini Uholanzi kwa mkutano wa kilele wa Nato.
Huu ni mkutano wa kwanza wa Trump wa Nato tangu achaguliwe tena. Trump amewahi kukosoa wanachama wa muungano huo kwa kupata dhamana ya bure ya usalama kutoka Marekani. Washirika hao wa Ulaya wanatamani sana kumuonyesha kuwa hilo si la kweli. Wanataka kumshawishi asilitoe jeshi la Marekani katika bara hilo.
"Uhusiano na Ulaya umekuwa mbaya sana tangu Trump arudi White House – kwa sababu ya ushuru katika biashara na mambo mengine, mwaka mmoja nyuma hatukuwa na uhakika kuwa angeshiriki mkutano huo," mwanadiplomasia mmoja wa ngazi ya juu - alizungumza nami kwa sharti la kutotajwa jina.
Katibu Mkuu wa Nato, Mark Rutte ameandaa mkutano huu akilenga kumshangaza Trump kwa kukubaliana na ongezeko kubwa la matumizi katika ulinzi, ili kuonyesha kwamba Waulaya sasa watawajibika zaidi kwa usalama wao wenyewe.
Trump anapenda kushinda na ana hasira za karibu. Hatataka kukosolewa katika mkutano wa Nato.
Huku nchi za Ulaya zikijitolea kutumia asilimia 5 ya Pato la Taifa katika ulinzi - kama vile alivyotaka katika wiki zake za kwanza huko White House. Lakini washirika wengine barani Ulaya ambao wanatatizika kupata pesa za ziada, wanatatizika zaidi.
Jambo la msingi: Ulaya inahitaji kuiweka karibu Marekani, nchi yenye nguvu kubwa za kijeshi na nyuklia.
Nato na Marekani
Haijabainika iwapo Marekani itatia saini tamko la mwisho la mkutano wa kilele wiki hii linaloitaja Urusi kama tishio kuu kwa muungano wa Nato.
Imani ya Ulaya kwa Marekani kama mlinzi wake mkuu imetikiswa na mtazamo wa Trump wa kuipendelea Moscow, na shinikizo lake kubwa kwa Kyiv, wakati akijaribu kumaliza vita nchini Ukraine.
Anaweza kuwa mtu asiyetabirika, lakini Trump si rais wa kwanza wa Marekani kutaka kuhamisha uwekezaji wa kijeshi kutoka Ulaya na kuupeleka maeneo mengine, hasa Indo-Pacific. Rais Obama alikuwa wazi kuhusu hilo mwaka 2011.
Marekani ina silaha za nyuklia zilizohifadhiwa nchini Italia, Ubelgiji, Ujerumani na Uholanzi. Ina wanajeshi 100,000 walio tayari kwa vita kote Ulaya, 20,000 kati yao katika nchi za Nato za Ulaya Mashariki, waliotumwa huko na Rais Biden baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Bara hilo litaongeza idadi ya wanajeshi wake, haswa Ujerumani na Poland ambazo zimepanga kuongeza vikosi vyao vya ardhini katika miaka michache ijayo. Lakini utegemezi wa Ulaya kwa Marekani unaongezeka zaidi, anasema Malcolm Chalmers, naibu mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Royal United Services.
Ulaya inaitegemea Washington kupata taarifa za kijasusi, ufuatiliaji, uwezo wa jeshi la anga na kamandi kuu. Marekani imefanya kazi kubwa ya kiuongozi Nato, kwa kuwaleta pamoja wanachama na vikosi.
Ni aina ya uwezo ambao unakosekana na unahitajika na jeshi la Marekani barani Asia, anasema Chalmers. Ikiwa wataondolewa Ulaya, watachukua muda mrefu sana kujijenga Asia.
Sasa Ulaya inalazimika kusimamia zaidi usalama wake, sio tu kujaribu kuishawishi Washington kubaki - lakini pia ikiwa rais wa Marekani ataamua kujiondoa Nato.
Nia ya Trump
Hakuna anayejua nia ya Trump ni nini. Viongozi wa Nato barani Ulaya walifarijika sana hivi karibuni, wakati utawala wake ulipotangaza kwamba Luteni Jenerali wa Jeshi la Wanaanga la Marekani Alexus Grynkewich atachukua nafasi iliyozoeleka ya NATO kama Kamanda Mkuu wa Muungano huo.
Lakini Washington inafanya ukaguzi wa matumizi yake ya kijeshi. Matangazo yanatarajiwa katika msimu wa vuli. Inafikiriwa hakutakuwa na ufadhili wowote mpya wa Marekani kwa Ukraine. Na kuna uwezekano mkubwa kwamba wanajeshi 20,000 wa ziada waliopo Ulaya mashariki watakuwa wa kwanza wa Marekani kuondolewa katika bara hilo.
Licha ya hayo, Poland inasema itahudhuria mkutano wa kilele wa Nato wa wiki hii katika hali ya kujiamini. Inaongeza mapato yake ya kitaifa katika ulinzi (sasa 4.7% ya Pato la Taifa) kuliko mwanachama mwingine yeyote wa Nato, ikiwa ni pamoja na Marekani. Inalenga, kujenga jeshi la nchi kavu lenye nguvu zaidi barani Ulaya.
Wakati wa Vita Baridi, Poland iliishi chini ya kivuli cha Umoja wa Kisovieti. Kwa kinachoendelea nchi jirani ya Ukraine. Si vigumu kuwashawishi Wapoland kwamba ulinzi ni kipaumbele cha juu.
Kwa wanasiasa katika nchi zilizo mbali zaidi na Urusi, hoja hiyo ni ngumu kuikubali.
Udhaifu wa Ulaya
Kuitetea Ulaya hakuhusu tu kiasi gani serikali itatumia. Udhaifu mkubwa wa Ulaya ni kwamba kuna aina nyingi ya silaha zisizofanana barani humo.
Inaripotiwa kuwa kuna aina 178 za mifumo ya silaha na aina 17 tofauti za vifaru katika Umoja wa Ulaya. Kuweka kando kandarasi za ulinzi wa taifa na kuunganisha rasilimali za Ulaya ili kuleta ufanisi zaidi, ni changamoto nyigine.
Kwa hivyo ni matokeo gani tutayaona katika mkutano huo?
Hilo litategemea Rais wa Marekani, anayewasili Uholanzi kwa Airforce One.
Balozi wa Trump katika Nato anasema mkutano huo unaweza kuwa wa kihistoria.
"Ni wakati wa mabadiliko" mwanadiplomasia mwingine wa ngazi amesema – ni "mkutano muhimu zaidi wa Nato tangu Vita Baridi." Wakati ambao Ulaya ilitumia kiasi sawa na cha Marekani katika ulinzi na kuchukua jukumu la usalama wake.