Wanawake waliozalishwa na kutelekezwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa

- Author, Ian Wafula
- Nafasi, BBC News
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Licha ya jua kali, Dimitri mwenye umri wa miaka kumi na mbili, sio jina lake halisi, anajificha ndani ya nyumba ya mama yake iliyotengezwa kwa mabati katika mtaa wa Birere, huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
"Hataki kutangamana na watoto wengine wanaomtania kwa kuwa mweupe na nywele zilizosokotana ," alisema mama yake, Kamate Bibiche, alipozungumza na BBC kabla mji wa Goma kuangukia mikononi mwa waasi wa M23 manamo mwezi Januari.
"Yeye (Dimitri) ni Mrusi, lakini hatawahi kuishi kwa urithi wake wa kweli," anasema.
Dimitri ni ukumbusho wa urithi wa maumivu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUSCO).
Tangu ulipopelekwa DRC mwishoni mwa mwaka 1999, ujumbe huo umekabiliwa na madai mengi ya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana wadogo.
Kamate anasitasita kabla ya kuchomoa kisanduku chenye vumbi kilichofichwa chini ya kitanda chake.
Ndani ya kisanduku hicho kuna kofia ilichakaaa na picha za zamani walizopiga pamoja-kumbukumbu aliyosalia nayo ya Yuriy, mwanamume anayesema ni baba yake Dimitri.
Kamate alikutana na Yuriy alipokuwa akijivinjari nyakaati za usiku na alivutiwa na hulka yake ya utulivu. Wawili hao walikuwa katika mahusiano ya kimapenzi kwa miezi mitatu.
"'Hakuwa kama wanaume wengine. Alinipenda na kunienzi. Ni miezi mitata ambayo sijawahi kuwa nayo maishani," Kamate anakumbuka.
Yuriy, sawa na walinda amani wengine waliotangamana na wenyeji, alisema machache kuhusu historia yake halisi au stakabadhi za kweli.
"Alikuw amlinda amani wa Umoja wa Mataifa," Kamateanasema.
"Alijua nilikuw amjamzito na kuahidi kuwa atanituna mimi na mwanawe atakapozaliwa. Likini alitoweka bila kusema lolote, kana kwamba hatumaanisha chochote kwake," Kamate anasema.
Anasema hana njia ya kumfikia mpenzi wake Mrusi, kwani nambari ya simu aliyotumia imekatwa
Matumizi mabaya ya madaraka
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ijapokuwa Kamate akiingi akatika uhusiano wa kimapenzo kwa hiari, chini ya azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa na baraza kuu mwaka 2005, bado inachukuliwa kuwa ya mahusiano ya kinyonyaji.
Sera hii inatambua usawa wa asili wa mamlaka kati ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na wakazi wa eneo walio katika mazingira magumu, ambayo inaweza kufanya mahusiano yoyote ya kingono kuwa ya kinyonyaji, hata kama yanaonekana kuwa ya makubaliano.
Azimio hilo linazitaka nchi wanachama kutoa haki kwa waathiriwa kwa kuwawajibisha wahalifu pindi watakaporejeshwa katika nchi zao.
Alipoulizwa kuhusu aliko mpenzi wa Kamate, msemaji wa MONUSCO Ndeye Lo aliiambia BBCIdhaa ya Kirusi kuwa haina wanajeshi katika misheni hiyo, akisema "ni maafisa wachache wa polisi na maafisa wa wafanyikazi wanaofanya kazi katika makao makuu".
Anasema misheni haiwezi kutoa ufikiaji wa rekodi za maafisa maalum wa Urusi ambao walihudumu mnamo 2012 "kwa sababu za kisheria".
BBC ilijaribu kumtafuta Yuriy, ikiwa ni pamoja na kwenye mitandao ya kijamii ya lugha ya Kirusi, lakini haikufanikiwa kumpata.
Tuhuma nzito

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumekumbwa na mzozo wa miongo kadhaa huku vikosi vya serikali vikipambana na makundi ya waasi wanaotaka kudhibiti eneo hilo lenye utajiri wa madini.
Mnamo Januari, Goma iliangukia mikononi mwa waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda. Takriban watu 7,000 walifariki katika mapigano hayo wakati wanamgambo hao wakiuteka mji huo, kwa mujibu wa waziri mkuu wa DR Congo.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu milioni nane kwa sasa wameyahama makazi yao, na kuifanya kuwa moja ya janga kubwa zaidi la wakimbizi wa ndani duniani. Watu wengi wanahangaika kwa umaskini uliokithiri na ukosefu wa mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, maji na malazi, jambo linalowaweka wazi wanawake na wasichana hasa katika hatari ya kudhulumiwa.
Wakati BBC ilipozungumza na Maria Masika (sio jina lake halisi), alikuwa amewasili Goma kutoka mji wa Sake, kaskazini mwa jiji hilo.
Vikosi vya serikali vilikuwa vikipambana na wapiganaji wa waasi lakini hatimaye walishindwa na kusalimu amri. Maria alishtuka sana - kutokana na milio ya risasi aliyoshuhudia wakati wa makabiliano hayo.
'Alijuwa nilikuwa mdogo'
Masika alikuwa ametembelea mji wa Goma kumsabahi binti yake Queen aliye na umri wa miaka 8, ambaye anaishi na bibi yake mjini kwa usalama.
Akiwa na umri wa miaka 17, Masika alijihusisha mwanajeshi wa kulinda amani wa Afrika Kusini aliyekuwa akihudumu katika kambi ya Minugugi.
"Alijua mimi ni mtoto," anasema.
"Alikodi nyumba karibu na kambi na alinitembelea wakati wowote alipokuwa na nafasi."
Baada ya kuzaliwa kwa mtoto wao Malkia, afisa huyo alitoweka na kumuacha Masika akijikimu kimaisha mwenyewe.
Akiwa bado na nia ya kumlea binti yake, anasema sasa anahatarisha maisha yake kutafuta riziki kama mfanyabiashara ya ngono huko Sake.
Ilipoulizwa kuhusu uhusiano kati ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa na wenyeji, Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini ilisema kuwa inachukulia kwa uzito madai hayo.
"Vikao vya mahakama ya kijeshi vinafanyika katika eneo la misheni ambapo kuna ushahidi wa kuaminika wa unyanyasaji wa kingono, kwa lengo la kuwachukulia hatu za kinidhamu dhdi ya wahusika," anasema msemaji wa jeshi Siphiwe Dlamini.

Katika makaazi ya Congo ya Family for Joy, ambayo yanatoa hifadhi kwa watoto waliotelekezwa, takribani watano wanaripotiwa kuwa wa walinda amani wa MONUSCO ambao waliwapachika mimba mama zao na hatimaye kuwatoroka.
"Kwa ushirikiana na wahisani wengine, tunatoa msaada kwa wanawake 200 na wasichana wadogo ambao wamedhulumiwa kingono na wafanyakazi wa MONUSCO," anasema Nelly Kyeya, mkurugenzi wa kituo hicho.
"Wengi wao wanakabiliwa na unyanyapaa mkubwa katika jamii zao kwa kugeukia kufanya ukahaba kujikimu kimaisha. Hali hiyo huwafanya baadhi yao kuwatelekeza watoto wao," anasema.
Sandrine Lusamaba, mratibu wa kitaifa wa Sofepadi, shirika la kutetea haki za wanawake nchini DRC, aliiambia BBC kwamba ukosefu wa mamlaka ya moja kwa moja na Umoja wa Mataifa ya kuwashtaki wahalifu wa unyanyasaji wa kijinsia ina maana kwamba wengi wanatembea huru.
Anasema nchi nyingi wanachama hazishirikiani kuwashtaki wanajeshi wao.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa Machi 2024 inaonyesha kuongezeka kwa madai ya unyanyasaji wa kijinsia na unyonyaji unaohusishwa na kulinda amani na ujumbe maalum wa kisiasa.
Kesi 100 ziliripotiwa dhidi ya ujumbe huo mwaka 2023, ikiwa ni ongezeko la visa 79 vilivyoripotiwa mwaka 2022. Matukio haya yanahusisha waathirika 143, ikiwa ni pamoja na watu watu 115 na watoto 28 kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.
Hasa, MONUSCO - ikiwa ni pamoja na Ujumbe wa zamani wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUC) - ilichangia visa 66 kati ya 100, ikionyesha wasiwasi kuhusu uwajibikaji ndani ya ujumbe huo.
Sera ya kutovumilia
"Wakati taarifa kuhusu madai ya uwezekano wa unyanyasaji na unyanyasaji wa kijinsia inapokewa, taarifa hiyo inatathminiwa na hatua madhubuti kuchukuliwa," anasema msemaji wa MONUSCO Ndeye Lo.
"Mfanyakazi yeyote ambaye madai yaliyotolewa dhidi yake yatathibitishwa atachukuliwa hatua)."
Ujumbe huo unasema kuwa unawawezesha waathiriwa na watoto wao kupitia Mfuko wa Msaada wa Waathiriwa kwa kutoa mafunzo ya ujuzi na elimu.
Lakini baadhi ya wanawake na wasichana wadogo kama Kamate na Maria wanasema hawakuwa na ufahamu kuhusu usaidizi unaopatikana huku wengine wakibaki na kiwewe cha kutafuta haki.
Imetafsiriwa na Ambia Hirsi












