Mossad: Operesheni 6 zenye utata za shirika la kijasusi la Israel

Chanzo cha picha, Getty Images
Katika opersheni ya kipekee inayoshukiwa kutekelezwa na Israel na kuzidisha mzozo katika eneo zima la mashariki ya kati vifaa vya 'pager' za mawasiliano vya Hezbollay na simu za upepo za kundi hilo vililipuka na kusababisha maafa ya makumi ya watu na wengine malefu kujeruhiwa .
Vifaa hivyo vilikusudiwa kuwa njia salama ya kukwepa ufuatiliaji wa hali ya juu wa Israeli, lakini vililipuka mikononi mwa watumiaji , huko Lebanon.
Serikali ya Lebanon iliishutumu Israel kwa mashambulizi hayo, ikiyaita "uchokozi wa jinai wa Israel," huku Hezbollah ikiapa "kulipiza kisasi."
Israel bado haijajibu madai hayo, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa baraza la mawaziri la serikali limewaagiza mawaziri kutotoa taarifa hadharani kuhusu tukio hilo.
Israel kwa kawaida inafuatilia kwa karibu shughuli za Hezbollah, ikipendekeza operesheni hiyo inaweza kuwa sehemu ya mzozo unaoendelea kati ya pande hizo mbili.
Iwapo Israel itawajibika, hii itakuwa moja ya oparesheni zake za kushangaza na za kipekee, na kufufua kumbukumbu za misheni za zamani zilizodaiwa kutekelzwa na nchi hiyo, na haswa shirika lake la kijasusi la kitaifa, Mossad.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mafanikio ya Mossad
Mossad imedaiwa kufanikisha misheni kadhaa za Israel dhidi ya watu,mashirika na nchi zinazodaiwa kuwa adui wa nchi hiyo .
Hizi ni baadhi ya misheni hizo ambazo ni mashuhuri zaidi.

Chanzo cha picha, Getty Images
1. Msako dhidi ya kiongozi wa Nazi Adolf Eichmann
Kutekwa nyara kwa kiongozi wa Nazi Adolf Eichmann huko Argentina mnamo 1960 ni moja ya matukio ya kijasusi maarufu ya Mossad.
Eichmann, mmoja wa wasanifu wakuu wa mauaji ya Wayahudi -Holocaust, alihusika na mateso ya Wayahudi katika kambi za mateso za Nazi wakati wa Vita vya pili vya dunia, ambapo takriban Wayahudi milioni sita waliuawa na Ujerumani chini ya uwatala wa Nazi.
Baada ya kukwepa kukamatwa kwa kuhamia nchi kadhaa, hatimaye Eichmann aliishi Argentina.
Timu ya maajenti 14 wa Mossad walimfuatilia, wakamteka nyara na kumpeleka Israel, ambako alihstakiwa na hatimaye kuuawa.
2. Operation Entebbe

Chanzo cha picha, Getty Images
Operesheni ya Entebbe nchini Uganda inachukuliwa kuwa mojawapo ya misheni ya kijeshi yenye mafanikio makubwa ya Israel.
Mossad walitoa taarifa za kijasusi, huku jeshi la Israel likifanya operesheni hiyo.
Vikosi vya makomando wa Israel vilifanikiwa kuwaokoa mateka 100 kutoka kwa ndege iliyokuwa ikisafiri kutoka Tel Aviv kuelekea Paris kupitia Athens. Ndege hiyo ilikuwa imebeba takriban abiria 250, wakiwemo Waisraeli 103.
Watekaji nyara hao - wanachama wawili wa chama cha Popular Front for the Liberation of Palestine na washirika wawili wa Ujerumani - waligeuza ndege kuelekea Entebbe, Uganda.
Operesheni hiyo ilisababisha vifo vya mateka watatu, watekaji nyara, wanajeshi kadhaa wa Uganda na mwanajeshi wa Israel Yonatan Netanyahu, nduguye Waziri Mkuu wa sasa wa Israel Benjamin Netanyahu.
3. Operation Brothers

Chanzo cha picha, Raffi Berg
Katika operesheni isiyo ya kawaida mwanzoni mwa miaka ya 1980, Mossad - wakitekeleza maagizo kutoka kwa Waziri Mkuu wa wakati huo Menachem Begin - walisafirisha zaidi ya Wayahudi 7,000 wa Ethiopia hadi Israeli kupitia Sudan, wakitumia kituo bandia cha kupiga mbizi .
Sudan ilikuwa adui wa Jumuiya ya Waarabu, kwa hivyo timu ya mawakala wa Mossad, wakifanya kazi kwa siri, walianzisha hoteli ya mapumziko kwenye pwani ya Bahari ya Shamu ya Sudan, ambayo walitumia kama ngome.
Wakati wa mchana, walijifanya kuwa wafanyakazi wa hoteli hiyo ya mapumziko, na usiku, walisafirisha Wayahudi, ambao walikuwa wamesafiri kisiri kutoka nchi jirani ya Ethiopia, nje ya nchi kwa ndege na kupitia bahari.
Operesheni hiyo ilidumu kwa takriban miaka mitano na hadi ilipogunduliwa, maajenti wa Mossad walikuwa tayari wametoroka.
4. Kulipiza kisasi baada ya utekaji nyara wa Olimpiki ya Munich

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 1972, kikundi cha wanamgambo wa Palestina Black September kiliwaua wanachama wawili wa Timu ya Israeli kwenye Michezo ya Olimpiki ya Munich - na kuwakamata wengine tisa.
Mateka hao waliuawa baadaye katika jaribio la kuwaokoa lililofeli la polisi wa Ujerumani Magharibi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya hapo, Mossad waliwashambulia wanachama kadhaa wa Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina, akiwemo Mahmoud Hamshari.
Aliuawa na kilipuzi kilichowekwa kwenye simu katika nyumba yake huko Paris.
Hamshari alipoteza mguu katika mlipuko huo na kufariki kutokana na majeraha yake.
5. Yahya Ayyash na simu ya rununu iliyolipuka

Chanzo cha picha, EPA
Katika operesheni sawa na hiyo mwaka 1996, Yahya Ayyash, mtengenezaji mabomu mkuu wa Hamas, aliuawa baada ya simu ya mkononi ya Motorola Alpha kujazwa gramu 50 za vilipuzi.
Ayyash, kiongozi mashuhuri wa tawi la kijeshi la Hamas, alijulikana kwa kuhusika kwake katika kutengeneza mabomu na kupanga mashambulizi tata dhidi ya malengo ya Israel.
Hili lilimfanya kuwa lengo kuu la mashirika ya usalama ya Israeli, mmoja wa watu wanaosakwa sana na Israeli.
Mwishoni mwa 2019, Israeli iliondoa udhibiti juu ya maelezo fulani ya mauaji, na televisheni ya Israeli Channel 13 ilitangaza rekodi ya simu ya mwisho kati ya Ayyash na baba yake.
Mauaji ya Hamshari na Ayyash yanaangazia historia ndefu na tata ya kutumia teknolojia ya hali ya juu kwa mauaji ya watu waliolengwa na Israel
6. Mahmoud al-Mabhouh: Aliuawa kwa kunyongwa

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 2010, Mahmoud al-Mabhouh, kiongozi mkuu wa kijeshi wa Hamas, aliuawa katika hoteli huko Dubai, Falme za Kiarabu.
Hapo awali, ilionekana kuwa kifo cha kawaida, lakini polisi wa Dubai waliweza kutambua timu ya wauaji baada ya kuchambua picha za kamera za usalama.
Polisi baadaye walifichua kwamba al-Mabhouh aliuawa kwa shoti ya umeme na kisha kunyongwa.
Operesheni hiyo inashukiwa kupangwa na Mossad, ambayo ilizua hasira ya kidiplomasia katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Wanadiplomasia wa Israel walidai, hata hivyo, kwamba hakuna ushahidi unaohusisha Mossad na shambulio hilo.
Lakini hawakukanusha kuhusika, jambo ambalo linaendana na sera ya Israel ya kudumisha “utata” katika masuala ya aina hii.
Majaribio ya mauaji yaliyofeli
Licha ya operesheni nyingi zilizofanikiwa, Mossad pia ina mapungufu yanayojulikana.
Khaled Meshal, kiongozi wa kisiasa wa Hamas

Chanzo cha picha, Getty Images
Moja ya oparesheni zilizosababisha mgogoro mkubwa wa kidiplomasia ni jaribio la Israel mwaka 1997 kumuua Khaled Meshaal, mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas nchini Jordan kwa kutumia sumu.
Misheni hiyo ilishindwa wakati maajenti wa Israeli walipokamatwa, na kulazimisha Israeli kutoa dawa ya kuokoa maisha ya Meshaali.
Mkuu wa Mossad Danny Yatom alisafiri kwa ndege hadi Jordan kutoa matibabu kwa Meshaal.
Jaribio hili la mauaji liliharibu kwa kiasi kikubwa uhusiano kati ya Jordan na Israel.
Mahmoud al-Zahar, kiongozi wa Hamas

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 2003, Israel ilifanya mashambulizi ya anga katika nyumba ya kiongozi wa Hamas Mahmoud al-Zahar katika mji wa Gaza.
Ingawa al-Zahar alinusurika katika shambulio hilo, operesheni hiyo ilisababisha vifo vya mkewe na mwanawe, Khaled, pamoja na wengine kadhaa.
Shambulio hilo la bomu liliharibu kabisa makazi yake, likiangazia madhara makubwa ya operesheni za kijeshi katika maeneo yenye watu wengi.
Kesi ya Lavon

Chanzo cha picha, Getty Images
Mnamo 1954, mamlaka ya Misri ilisambaratisha operesheni ya kijasusi ya Israeli iliyojulikana kama Operesheni Susannah.
Mpango uliovunjwa ulikuwa wa kutega mabomu kwenye sehemu muhimu za Marekani na Uingereza nchini Misri kuishinikiza Uingereza kuweka vikosi vyake kwenye Mfereji wa Suez.
Tukio hilo lilijulikana kama kesi ya Lavon, iliyopewa jina la Waziri wa Ulinzi wa Israeli wakati huo, Pinhas Lavon.
Inaaminika alihusika katika kupanga shughuli hiyo.
Mossad, kwa upande wake, ilionekana wakati huo kuwajibika kwa kufeli kwa misheni hiyo ya kijasusi.
Vita vya Yom Kippur

Chanzo cha picha, Getty Images
Tarehe 6 Oktoba 1973, Misri na Syria zilianzisha mashambulizi ya kushtukiza dhidi ya Israeli ili kuteka tena Rasi ya Sinai na Milima ya Golan.
Muda wa shambulio hilo, lililotekelezwa wakati wa Yom Kippur, Siku ya Kiyahudi ya Upatanisho, uliwashtua Waisraeli mwanzoni mwa vita.
Misri na Syria zilishambulia Israeli kwa pande mbili.
Majeshi ya Misri yalivuka Mfereji wa Suez, yakipata hasara ndogo tu ya waliotarajiwa, huku majeshi ya Syria yakishambulia maeneo ya Israel na kuvuka Milima ya Golan.
Umoja wa Kisovieti ulisambaza vifaa kwa Syria na Misri, na Marekani ilitoa shehena ya vifaa vya dharura kwa Israeli.
Israel ilifanikiwa kuvirudisha nyuma vikosi vya jeshi, na vita vilimalizika Oktoba 25 - siku nne baada ya azimio la Umoja wa Mataifa la kutaka mapigano yasitishwe.
Shambulio la Oktoba 7, 2023

Chanzo cha picha, AFP
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Almost 50 years later, Israel was again surprised by a surprise attack, this time launched by Hamas against cities near the Gaza border, on October 7, 2023.
The Mossad's failure to predict the attack is considered a major fiasco, reflecting what analysts say is a projected weakness in Israel's deterrence policy toward Hamas.
The October 7 attack resulted in the deaths of approximately 1,200 people, most of them civilians, according to Israeli authorities. About 251 other people were taken to Gaza as hostages.
In response to the Hamas attack, Israel launched a war in the Gaza Strip, which has so far resulted in more than 40,000 deaths, most of them civilians, according to the Gaza Health Ministry.
Takriban miaka 50 baadaye, Israel ilishangazwa tena na shambulio la kushtukiza, mara hii lililozinduliwa na Hamas dhidi ya miji iliyo karibu na mpaka wa Gaza, Oktoba 7, 2023.
Kushindwa kwa Mossad kufahamu kuhusu shambulio hilo kunachukuliwa kuwa sakata kubwa , kuakisi kile wachambuzi wanasema ni udhaifu unaotarajiwa katika sera ya Israel ya kuzuia Hamas.
Shambulio la Oktoba 7 lilisababisha vifo vya takriban watu 1,200, wengi wao wakiwa raia, kulingana na mamlaka ya Israeli. Takriban watu wengine 251 walipelekwa Gaza kama mateka.
Katika kujibu mashambulizi ya Hamas, Israel ilianzisha vita katika Ukanda wa Gaza, ambayo hadi sasa imesababisha vifo vya zaidi ya 40,000, wengi wao wakiwa raia, kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza.Vita hivyo vimeongeza uhasama wa Israel na kundi la Hezbollah la Lebanon.Baada ya milipuko ya vifaa vya mawasiliano vya kundi hilo,Israel sasa imeanzisha mashambulizi ya moja kwa moja ndani ya Lebanon huku kundi hilo na washirika wake likirisha makombora dhidi ya Israel.Hatua hiyo inahatarisha zaidi hali tete ya usalama wa kanda nzima ya mashariki ya kati.
*Ripoti ya ziada na Raffi Berg wa BBC News.Imetafsiriwa na Yusuf Jumah












