Jinsi poda ya waridi inavyotumiwa kupambana na moto California

Muda wa kusoma: Dakika 3

Huku zimamoto wakipambana na moto mkali kusini mwa California, picha zimeibuka za ndege zikidondosha poda nyekundu na waridi kwenye vitongoji vya Los Angeles.

Maafisa wanasema maelfu ya galoni za poda hiyo zilidondoshwa wiki iliyopita ili kuzuia moto huo kuenea.

Pia unaweza kusoma

Inasaidiaje kupambana na moto?

Poda hiyo inaitwa Phos-Chek, inauzwa na kampuni inayoitwa Perimeter. Imetumika kupambana na moto nchini Marekani tangu 1963, na ndio nyenzo kuu ya kuzuia moto inayotumiwa na Idara ya Misitu na Ulinzi dhidi ya Moto ya California.

Pia ndio nyenzo inayotumika zaidi duniani katika kupambana na moto, kulingana na ripoti ya 2022 ya Associated Press.

Huku mioto ya nyika ikiendelea kusini mwa California, picha zimeonekana za poda ya waridi ikiwa imefunika magari na barabara.

Perimeter, kampuni inayozalisha poda hiyo, imeshauri siku za nyuma kuwa unapaswa kuisafisha mara tu inapokuwa salama kufanya hivyo.

"Kadiri poda hiyo inavyokauka, ndivyo inavyokuwa ngumu zaidi kuindoa," walionya.

Kampuni hiyo imesema, maji ya uvuguvugu na sabuni huondoa poda hiyo katika eneo dogo. Kwa eneo kubwa, mashine zinazotoa maji kwa nguvu (pressure washers), zinaweza kutumika.

Kuhusu rangi yake, kampuni hiyo ilisema ni "kwa ajili ya marubani na wazima kuona sawa sawa." Baada ya siku chache za kupigwa na jua, rangi hufifia na kuingia kwenye udongo.

Poda hiyo kwa kawaida hunyunyiziwa kuzunguka moto wa nyikani na kwenye mimea na ardhi ambayo inaweza kukabiliwa na moto ili kuzuia moto kuenea katika eneo hilo.

Kulingana na Idara ya Misitu ya Marekani, poda hiyo "hupunguza kasi ya kuenea kwa moto kwa kupoza na kufunika, na kuunyima moto hewa ya oksijeni, na kupunguza kasi ya moto."

Utata wa poda hiyo

Matumizi yake yamekuwa na utata katika siku za nyuma juu ya madhara yake kwa mazingira.

Kesi iliyowasilishwa mwaka 2022 na Wafanyakazi wa Idara ya Misitu kwa Maadili ya Mazingira, shirika linaloundwa na wafanyakazi wa sasa na wa zamani wa Idara ya Misitu ya Marekani, iliishutumu idara hiyo ya serikali kwa kukiuka sheria za maji safi ya nchi kwa kutupa kemikali za kuzuia moto kutoka katika ndege hadi kwenye misitu.

Walisema kemikali hiyo inaua samaki na haifai.

Mwaka uliofuata, hakimu alikubaliana na wafanyakazi hao, lakini katika uamuzi wake aliruhusu Idara ya Misitu kuendelea kuitumia huku ikitafuta kibali cha kuitumia kutoka kwa Wakala wa Ulinzi wa Mazingira wa Marekani (EPA).

Kesi hiyo ilivuta hisia za watu waliokumbwa na majanga ya moto wa nyika siku za nyuma, ukiwemo mji wa Paradise, California, ambao uliharibiwa na moto mwaka 2018.

Meya wake wa wakati huo, Greg Bolin, alipongeza uamuzi wa jaji, akisema jamii "zina nafasi ya kupambana" na moto.

Idara ya Misitu iliiambia redio ya NPR mwaka huu, kwamba imezuia matumizi ya aina moja ya Phos-Chek – iitwayo Phos-Chek LC95 - na kupendekeza aina nyingine – iitwayo MVP-Fx - ikisema hii ya pili ina sumu kidogo kwa wanyamapori.

Idara ya Misitu pia imepiga marufuku kuangusha poda hiyo katika maeneo nyeti ya mazingira, kama vile vyanzo vya maji na makazi ya spishi walio hatarini kutoweka.

Lakini marufuku hiyo inaweza kuondolewa pale "maisha ya binadamu au usalama wa umma vitakapo kuwa hatarini."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah