Je, picha za satelaiti zinaonyesha nini kuhusu mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Picha za satelaiti zilizochambuliwa na kitengo cha BBC cha uthibitishaji wa taarifa, BBC Verify, zinaonyesha uharibifu wa maeneo kadhaa ya kijeshi nchini Iran kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel siku ya Jumamosi.

Ni pamoja na maeneo ambayo wataalamu wanasema yalitumika kwa utengenezaji wa makombora na mifumo ya ulinzi wa mashambulizi ya anga, pamoja na maeneo yaliyohusishwa hapo awali na mpango wa nyuklia wa Iran.

Unaweza pia kusoma:

Picha za satelaiti za baada ya mashambulizi ya Israel zinaonyesha uharibifu wa majengo katika kile ambacho wataalamu wanasema ni kituo kikuu cha kutengeneza silaha kilichopo katika eneo la Parchin, lililopo takriban kilomita 30 (maili 18.5) mashariki mwa Tehran.

Eneo hilo limehusishwa na utengenezaji wa roketi kulingana na wataalamu kutoka taasisi ya kimataifa ya mafunzo ya kimkakati (IISS).

Ikilinganisha picha za satelaiti zenye ubora wa juu zilizopigwa tarehe 9 Septemba na picha iliyopigwa tarehe 27 Oktoba, inaonekana kwamba angalau miundo minne imeharibiwa kwa kiasi kikubwa

Moja ya miundo hii, inayojulikana kama Taleghan 2, imehusishwa hapo awali na mpango wa nyuklia wa Iran na Shirika la kimataifa la nishati ya atomiki (IAEA).

Mnamo mwaka wa 2016 IAEA lilipata ushahidi wa chembe za uranium kwenye tovuti , na kuibua maswali kuhusu shughuli za nyuklia zilizopigwa marufuku huko.

Tovuti nyingine ambayo inaonekana kulengwa katika mashambulizi ya anga ya Israel ni ile ya Khojir, iliyopo takriban kilomita 20 kaskazini-magharibi mwa Parchin.

Fabian Hinz wa taasisi ya ISS anasema "Khojir linajulikana kama eneo lenye mkusanyiko wa juu wa miundombinu inayohusiana na makombora ndani ya Iran."

Lilikuwa ni eneo la mlipuko mkubwa wa ajabu mnamo 2020 .

Picha za satelaiti zinaonyesha angalau majengo mawili katika jumba hilo yanaonekana kuharibiwa vibaya.

Eneo la kijeshi la Shahroud, takriban kilomita 350 mashariki mwa Tehran, pia limepata uharibifu, kulingana na picha za satelaiti zilizochukuliwa baada ya mashambulizi ya Israel.

Eneo hili liko katika mkoa wa kaskazini wa Semnan, na ni muhimu kwa sababu limehusika katika utengenezaji wa mitambo ya kutengeneza makombora ya masafa marefu, kulingana na Fabian Hinz kutoka taasisi ya IISS.

Karibu na eneo hili kuna kituo cha anga cha Shahroud, kinachodhibitiwa na Jeshi la walinzi wa mapinduzi, na ndipo ambapo Iran ilirusha satelaiti ya kijeshi angani mnamo 2020 .

Israel imedai kuwa ilifanikiwa kulenga mifumo ya ulinzi ya anga ya Iran katika maeneo kadhaa lakini ni vigumu kuthibitisha hili kwa picha za satelaiti zilizopo.

Tumepata picha za setilaiti ambazo zinaonekana kuonyesha uharibifu wa eneo lililoelezwa na wataalamu kama mfump mpya wa rada.

Iko kwenye mlima wa Shah Nakhjir karibu na mji wa magharibi wa Ilam, na Jeremy Binnie, mtaalamu wa Mashariki ya Kati huko Janes, kampuni ya kijasusi ya ulinzi, anasema huu unaweza kuwa mfumo mpya wa ulinzi wa rada.

Eneo lenyewe lilianza kutumika miongo kadhaa iliyopita, lakini picha za satelaiti zilizochambuliwa na wataalam wa chanzo huria zinaonyesha kuwa limefanyiwa ukarabati mkubwa katika miaka ya hivi karibuni.

Tumetambua pia kile kinachoonekana kuwa uharibifu wa kitengo cha kuhifadhi katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Abadan kilicho katika mkoa wa kusini-magharibi wa Khuzestan.

Hata hivyo, hatujui ni nini kiliisababisha na huenda kukawa na uharibifu katika baadhi ya maeneo kote nchini Iran unaosababishwa na vifusi au mifumo ya ulinzi kurusha makombora.

Gazeti la New York Times limewanukuu maafisa wa Israel wakisema kuwa kiwanda cha kusafisha mafuta cha Abadan ni mojawapo ya maeneo yaliyolengwa katika mashambulizi yake ya anga Jumamosi asubuhi.

Mamlaka ya Irani ilithibitisha Jumamosi kwamba mkoa wa Khuzestan ulilengwa na Israeli.

Kiwanda cha kusafisha mafuta cha Abadan ndicho kikubwa zaidi nchini humo, chenye uwezo wa kuzalisha mapipa 500,000 kwa siku, kulingana na mtendaji mkuu wake .

Taswira ya setilaiti sio bora kila mara katika kuitambua miundo iliyoharibika.

Kwa mfano, picha ambayo tumethibitisha inayoonyesha moshi ukifuka karibu na kituo cha ulinzi wa anga cha Hazrat Amir Brigade iliashiria kuwa ilikuwa imelengwa kwa ufanisi. Lakini picha za setilaiti za eneo zilizopigwa siku ya Jumapili hazionekani vyema vya kuthibitisha uharibifu wowote kwenye eneo.

Iran ilifanya shambulizi la kombora dhidi ya Israel mwanzoni mwa Oktoba kwa mara ya pili mwaka huu, baada ya kurusha makombora 300 na ndege zisizo na rubani mwezi Aprili.

Ripoti ya ziada ya Tom Spencer na Daniele Palumbo

Unaweza pia kusoma:

Imetafsiriwa na Dinah Gahamanyi na kuhaririwa na Seif Abdalla