Tunachojua kuhusu shambulio la Israel dhidi ya Iran

Muda wa kusoma: Dakika 4

Israel imeanzisha mashambulizi ya anga ambayo inasema ni "sahihi na yaliyolengwa" dhidi ya Iran ili kulipiza kisasi mashambulizi ya makombora ya Tehran dhidi ya Israel mapema mwezi huu.

Ni mashambulizi ya hivi punde zaidi kati ya Israel na Iran ambayo kwa miezi kadhaa yamezua hofu kuwa yanaweza kusababisha vita vya kikanda.

Lakini wakati Iran ikisema kwamba mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi yaliua wanajeshi wawili, dalili za mapema zinaonyesha kuwa mashambulizi hayo yalikuwa madogo na yaliyolengwa zaidi kuliko ilivyohofiwa.

Haya ndiyo tunayofahamu kufikia sasa.

Mashambulizi hayo yalifanyika vipi?

Muda mfupi baada ya 02:00 usiku, vyombo vya habari vya Iran viliripoti milipuko ndani na karibu na mji mkuu, Tehran.

Video zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na kuthibitishwa na BBC zilionyesha makombora angani juu ya mji huo, huku wakaazi katika baadhi ya maeneo wakiripoti kusikia milipuko mikubwa.

Takriban saa 02:30, Jeshi Israel (IDF) lilithibitisha kuwa lilikuwa likifanya mashambulizi yenye "usahihi" kwenye "maeneo ya kijeshi" nchini Iran.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Yoav Gallant walifuatilia operesheni hiyo kutoka katika kituo cha IDF mjini Tel Aviv.

Mara tu baada ya 06:00, IDF ilisema mashambulizi yalikuwa yamekamilika.

Ikulu ya White House ya Marekani ilielezea mashambulizi hayo kama "hatua ya kujilinda". Aidha afisa mmoja mkuu wa serikali alisema Marekani iliwasiliana na Israel ili kuhimiza jibu ambalo "ni la kiwango sawa" na mashambulizi dhidi yake.

Mashambulizi yalikuwa na ukubwa kiasi gani?

Kiwango cha mashambulizi - na uharibifu uliotokea - bado hayajulikani kikamilifu kwa wakati huu.

IDF ilisema ilikuwa imelenga na kushambulia vifaa vya kutengeneza makombora, maeneo ya kurusha makombora kutoka ardhini hadi angani na maeneo mengine ya kijeshi.

Jeshi la Iran lilithibitisha kuwa wanajeshi wawili walikufa "wakikabiliana na makombora".

Mamlaka za Iran zilisema maeneo katika mikoa ya Tehran, Khuzestan na Ilam yalilengwa. Jeshi la ulinzi wa anga la nchi hiyo lilisema kuwa "limefanikiwa kuzuia" mashambulizi, lakini "maeneo mengine yalipata uharibifu mdogo".

Afisa mmoja mkuu wa serikali ya Marekani alisema mashambulizi hayo hayakujumuisha maeneo yenye miundombinu ya mafuta ya Iran au vituo vya nyuklia, maeneo ambayo rais Joe Biden aliishauri Israel isishambulie.

Vyombo vya habari vya serikali ya Syria pia viliripoti mashambulizi katika maeneo ya kijeshi katika eneo la kati na kusini mwa Syria, ingawa Israel haijathibitisha kushambulia taifa hilo.

Kwa nini Israel ilishambulia Iran?

Iran ni taifa linalounga mkono kwa kiasi kikubwa zaidi makundi mbalimbali katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo yana uhasama na Israel, ikiwa ni pamoja na Hamas na Hezbollah, ambayo Israel inapigana nayo kwa sasa.

Mwezi Aprili, Iran ilifanya shambulizi la kwanza la moja kwa moja dhidi ya Israel lililokuwa na takriban makombora 300 na ndege zisizo na rubani, kulipiza kisasi shambulio la anga la Israel katika ubalozi wa Iran nchini Syria na kuua makamanda kadhaa wakuu wa tawi la Jeshi la Iran linalojulikana kama Iran’s Revolutionary Guard Corps (IRGC).

Israel ilijibu kwa shambulio "ndogo" lililolenga mfumo wa ulinzi wa makombora katika eneo la Iran la Isfahan.

Kisha, mwezi Julai, Israel ilimuua kamanda mkuu wa Hezbollah katika shambulio la anga huko Beirut. Siku iliyofuatia, kiongozi wa kisiasa wa Hamas Ismail Haniyeh aliuawa katika mlipuko uliotokea Tehran. Iran iliilaumu Israel, lakini Israel haikusema chochote.

Mwishoni mwa Septemba, Israel ilimuua kiongozi wa Hezbollah Hassan Nasrallah huko Beirut pamoja na Abbas Nilforoushan, afisa wa ngazi ya juu wa Iran.

Mnamo Oktoba 1, Iran ilirusha makombora 200 dhidi ya Israel, ikisema ilikuwa inalipiza vifo vya Haniyeh na Nasrallah.

Nini kinatokea baada ya hapa?

Dalili za mapemaa zinaashiria kuwa shambulio hili halikuwa kubwa kama baadhi walivyohofia.

Gazeti la Axios la Marekani liliripoti kuwa kabla ya mashambulizi hayo, Israel ilituma ujumbe kwa Iran ikitoa maelezo fulani kuhusu shambulio hilo, na kuionya Tehran dhidi ya kujibu.

Hiyo inaweza kuashiria kuwa Israel haitaki kuzidisha mzozo uliopo - angalau kwa sasa.

"Tunazingatia kwa kiasi kikubwa malengo yetu ya kivita katika ukanda wa Gaza na Lebanon. Ni Iran ambayo inaendelea kushinikiza kutokea kwa mzozo mkubwa wa kikanda," IDF ilisema katika taarifa.

Afisa mmoja mkuu wa Marekani alisema "huu unapaswa kuwa mwisho wa makabiliano haya ya moja kwa moja ya kushambuliana kati ya Israel na Iran."

Iran, hadi kufikia sasa, haijatoa taarifa nyingi.

Chanzo kilichonukuliwa na shirika la habari la Tasnim lenye uhusiano wa karibu na IRGC kilisema: "Iran ina haki ya kujibu uchokozi wowote na hakuna shaka kuwa Israel itapata jibu sawia kwa hatua yoyote inayochukua."

Imetafsiriwa na Peter Mwangangi na kuhaririwa na Ambia Hirsi