Kwanini Lamine Yamal hawezi kukwepa kulinganishwa na Messi

Muda wa kusoma: Dakika 6

Mshambulizi chipukizi wa Barcelona Lamine Yamal alisema hatajilinganisha na Lionel Messi - na baadaye kucheza mchezo ambao Messi mwenye umri wa miaka 17 angeweza tu kutamani katika moja ya mechi kubwa za muda wote za nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Ilimfanya aitwe mtu mwenye 'kipaji cha ajabu'

Barca na Inter Milan zilitoka sare ya 3-3 katika pambano lao la mkondo wa kwanza, huku beki Denzel Dumfries akihusika katika mabao yote matatu ya Inter, akifunga mara mbili, na kutangazwa mchezaji bora wa mechi.

Lakini vichwa vingi vya habari duniani vitamuhusu Yamal mwenye umri wa miaka 17, ambaye alifunga bao lake la 22 katika mchezo wake wa kihistoria wa 100 wa Barcelona.

Alionesha kiwango bora cha mchezo, haswa katika kipindi cha kwanza na kuisaidia timu yake kurudi katika mchezo baada ya Inter kuwa mbele 2-0 katika dakika ya 21.

Yamal alifunga bao zuri la nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa sawa na alivyofanya katika mashindano ya Euro 2024 msimu uliopita. Tayari ni mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani kabla ya kufikisha umri wa miaka 18.

"Sidhani kama nimeona mchezaji akitawala dakika 45 hapo awali maishani mwangu. Ni jambo la kushangaza," alisema mchambuzi wa TNT Sports Ally McCoist wakati wachezaji wakitoka nje ya uwanja wakati wa mapumziko.

Bosi wa Inter Milan Simone Inzaghi alimpa Yamal sifa za juu zaidi baadaye.

"Lamine ni aina ya talanta inayokuja kila baada ya miaka 50, na kumuona kwa karibu kulinivutia sana," alisema.

"Alitusababishia matatizo makubwa kwa sababu tulimuwekea wachezaji wawili lakini haikutosha ."

Mkufunzi wa Barca, Hansi Flick alisema: "Yeye ni maalum, ni mtu mwenye kipaji. Katika mechi kubwa, anajitokeza.

"Ikiwa kipaji hiki hujitokeza kila baada ya miaka 50 kama Simone alivyosema, nina furaha ni kwa Barcelona."

Mchambuzi wa BBC Stephen Warnock alimwita "mshindi wa baadaye wa Ballon d'Or".

Mojawapo ya mechi kuu za msimu huu - kila mmoja sasa amevutiwa na mechi ya mkondo wa pili huko San Siro Milan wiki ijayo, ikiwa ni mabadiliko ya kasi kutoka kwa ushindi wa 1-0 wa Paris St-Germain dhidi ya Arsenal siku moja kabla.

Pia unaweza kusoma

Je, Yamal alifanya nini?

Kulikuwa na eti eti kabla ya mchezo wakati Yamal alionekana kupata jeraha katika sehemeu yake ya nyonga wakati wa mapumziko na uvumi ukaenenea kwamba huenda hatoendelea kucheza.

Alikuwa ameanzishwa lakini hakuwa na athari yoyote kabla ya Inter kuongoza 2-0 kupitia mabao mawili ya ajabu kupitia - Marcus Thuram aliyefunga kwa kisigino katika sekunde 30 kutoka kwa krosi ya Dumfries, kabla ya Dumfries' kufunga bao la pili.

Lakini Yamal - ambaye alikuwa amekabwa na wachezaji wawili kuwachenga na kufunga kwa urahisi wa kushangaza na kujiamini.

Muda mfupi baadaye, aliwachenga mabeki zaidi na akapiga shuti ambalo kipa wa Inter Yann Sommer alilipangua .

Ferran Torres kisha akamalizia mpango mzuri wa kuisaidia Barca kusawazisha kabla ya mapumziko.

Dumfries, hata hivyo, alipata bao la pili kwa mpira wa kichwa na kuwarudisha mbele mabingwa hao wa Itali..

Lakini muda mfupi baadaye Barca walisawazisha tena huku Yamal akitoa pasi kwa ustadi na Raphinha akapiga shuti ndani ya umbali wa yadi 25 ambalo liligonga mwamba wa goli na kumpiga kipa Sommer mgongoni na kuwa bao la kujifunga.

Henrikh Mkhitaryan alidhani amefanya kuwa mambo 4-3 kwa Inter lakini bao lake lilikataliwa kwa kuotea.

Yamal alikaribia kufunga bao la tatu wakati alipowachenga mabeki na kupiga shuti ambalo lilipiga mmwamba wa goli na kutoka nje.

Rekodi zinaendelea kuvunjwa

Ni vigumu kuelewa ni mafanikio kiasi gani Yamal amepata katika umri wake.

Hii ilikuwa mechi yake ya 100 kwa Barcelona, na bao lake la 22 katika mechi 19 alizochezea Uhispania.

Yamal ana asisti 27 pia, zikiwemo mbili katika ushindi wa mwisho wa muda wa ziada wa Copa del Rey Jumamosi dhidi ya Real Madrid.

Wachezaji wawili wakubwa wa kizazi hiki - Messi na Cristiano Ronaldo - hawakucheza mechi zao za kimataifa hadi walipokuwa na umri wa miaka 18, wakati Yamal alishinda Euro 2024 siku moja baada ya kuzaliwa kwake 17.

Messi alifunga bao moja kabla ya kufikisha miaka 18, huku Ronaldo akifunga mabao matano.

Yamal ndiye mchezaji mdogo zaidi wa Barcelona La Liga (akiwa umri wa miaka 15) na ndiye mwenye umri mdogo zaidi kufunga na kusaidia katika La Liga kwa timu yoyote.

Pia anashikilia rekodi za kuwa mwanzilishi mdogo zaidi wa Ligi ya Mabingwa, mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kufunga katika mchezo wa mtoano, robo fainali na sasa nusu fainali.

Yamal ndiye mchezaji na mfungaji mdogo zaidi wa Uhispania na ndiye mchezaji na mfungaji mwenye umri mdogo zaidi katika michuano ya Ulaya.

Yamal hawezi kukwepa kulinganishwa na Messi

Wachezaji wachache sana wamekuwa na athari katika soka wakiwa umri wa Yamal. Atafikisha miaka 18 mwezi Julai.

Anaonekana kuwa na kipaji cha karibu zaidi ambacho tumeona kwa nyota wa Barcelona na Argentina Messi, ambaye sasa yukokatika klabu ya Inter Miami na bila shaka mwanasoka bora zaidi katika historia.

Wawili hao wote walikuja kupitia akademi ya Barca, La Masia, na wote wanachezea wingi ya kulia.

"Sijilinganishi naye, kwa sababu sijilinganishi na mtu yeyote - na zaidi na Messi," Yamal aliwaambia waandishi wa habari katika maandalizi ya mchezo huo, huku pia akimtaja Muargentina huyo kama "mchezaji bora zaidi katika historia".

Lakini Messi alikuwa na matumaini makubwa sana akiwa na umri wa miaka 17, badala ya kuonekana kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi duniani.

Yamal aliongeza: "Sidhani kama ulinganisho huo una mantiki, na Messi hata kidogo - nitajifurahisha mwenyewe, na kuwa mimi mwenyewe."

Lakini ana historia isiyo ya kawaida na Messi, ambaye alipigwa picha naye akiwa mtoto.

Picha iliibuka, kutoka kwa picha ya kalenda ya hisani iliyopigwa katika Nou Camp ya Barcelona mwaka 2007.

Ndani yake, Messi mwenye umri wa miaka 20 alimbeba mtoto Yamal na kumsaidia kuoga. Ndiyo kweli.

Picha hizo zilitokea baada ya Unicef kufanya shindano la bahati nasibu katika mji wa Mataro ambako familia ya Lamine iliishi.

"Tulishuka hadi katikati ya jiji na unaweza kusema kuwa kuna nyota katika mji huu kwa sasa Lamine Yamal," alisema mlinzi wa zamani wa Uingereza Rio Ferdinand kwenye TNT Sports.

"Kulikuwa na pengo wakati Messi alipoondoka Barcelona, mtoto huyu anafanya mambo akiwa na umri wa miaka 17 ambayo hatujawahi kuona. Starehe na urahisi anaocheza nao ni wa ajabu na anafurahia akiwa uwanjani."

'Kila mtu aondoke njiani'

Wataalamu wa mambo walishangaa kwa kile walichokiona kutoka kwa Yamal.

Owen Hargreaves, kiungo wa zamani wa Bayern Munich, Manchester United na England, alimwita "msimbo wa kudanganya" kwenye TNT.

"Nataka tu kuona Lamine Yamal akipata mpira na kila mtu mwingine akitoka katika njia yake," aliongeza.

Beki wa zamani wa Liverpool na Uingereza Warnock, akitazama Mechi Bora ya Siku ya Ligi ya Mabingwa ya BBC, alisema: "Alikuwa hachezewi nyakati fulani. Bao lake lilikuwa la kushangaza

'' Inashangaza ukimtazama Yamal. Unajua, kwa ufanisi, kile anachotaka kufanya siku zote - anataka kuingia ndani kwa mguu wake wa kushoto. Kwa hivyo unatatizika kupita kiasi na ana uwezo wa kuuburuta mpira kwa mguu wake wa kushoto hadi mguu wake wa kulia, na anaweza kufunga bao zuri kwa mguu wake wa kulia pia.

"Yeye ni kipaji cha ajabu na ninapenda kumtazama."

Naye Ferdinand aliandika kwenye mtandao wa kijamii: "Kama kuna talanta ya kandanda basi nadhani Lamine Yamal yuko katika kiwango kingine kwa mchezaji yeyote anayecheza mchezo huo katika ligi tano bora za kandanda duniani. Kweli ni ajabu."

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Seif Abdalla Dzungu