Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Miaka 60 AU: Je, Afrika inashindwa kutatua migogoro yake bila nguvu za nje?
- Author, Rashid Abdallah
- Nafasi, Mchambuzi Tanzania
“Migogoro ya ndani ya nchi na ile inayohusisha nchi na nchi, vilevile na ugaidi, bado yanaendelea barani Afrika, matokeo yake amani, usalama, demokrasia na maendeleo viko hatarini katika nchi zetu kadhaa.” Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki, akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Umoja wa Afrika.
Migogoro ni changamoto moja. Namna ya kutatua migogoro ni changamoto nyingine. Bara la Afrika linakumbwa na changamoto zote mbili kwa wakati mmoja. Kuna mataifa yako kwenye sintofahamu kwa miaka mingi, na bado hakuja patikana suluhu.
Historia inaonesha kila vita vinapotokea katika nchi fulani Afrika, risasi na mabomu haviwi chanzo pekee cha vifo. Njaa na maradhi pia huchukua idadi kubwa ya maisha ya watu – hasa watoto na wanawake.
Takribani watu milioni moja walifariki kwa njaa kati ya mwaka 1983 - 1985 wakati wa vita vya mwongo mmoja na nusu nchini Ethiopia. Makadirio ya watu laki mbili hadi tatu waliaga dunia Somalia kwa njaa mwaka 1991 hadi 1992, wakati makundi ya washika silaha yakiharibu nchi.
Hali ya sasa ya Afrika
Wiki hii imetimia miaka 60 tangu kuundwa kwa Umoja wa Afrika (AU), hapo awali ukijulikana kwa jina la Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), ulioanzishwa rasmi Mei 25, 19963, Addis Ababa, nchini Ethiopia.
Umoja wa Afrika umehusika kutafuta suluhu ya migogoro katika nchi wanachama tangu kuanzishwa. Kuna juhudi za kisiasa hufanywa na wakati mwingine nguvu za kijeshi kupitia vikosi vya kulinda amani hutumika. Licha ya juhudi hizo, bado Afrika imezongwa na migogoro na mengine ni ya muda mrefu.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, (OCHA), katika ripoti yake ya Novemba 2022, inayoangazia migogoro barani Afrika kutoka 1989 hadi 2021, inaeleza Afrika inaongoza kuwa na idadi kubwa ya migogoro ya kijamii, kuliko bara lolote.
Hapa kinachokusudiwa ni migogoro mfano ya wafugaji na wakulima, ambayo huacha majeruhi na vifo. Pia, mivutano ya kikabila ambayo hutokea mara kwa mara barani. Vilevile, makundi ya wahalifu wenye silaha na mfano wa hayo.
Taasisi ya Geneva Academy inayotafiti masuala ya sheria za kimataifa na sera katika maeneo ya vita, chini ya Chuo Kikuu cha Geneva, Switzerland, inaiweka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini – kuwa eneo lililoathirika zaidi na migogoro ya kutumia silaha duniani.
Bila shaka, hizi si habari njema. Ikiwa Afrika haijaachwa nyuma kwa idadi kubwa ya migogoro maanake ukubwa wa tatizo nao ni mkubwa. Ripoti hiyo imetaja Afrika Kaskazini pekee, ila Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara nako kuna nchi zinawaka moto.
Cameron, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Somalia, Mozambique, makundi yenye silaha yanayosumbua mataifa ya Afrika Magharibi na Ukanda wa Sahel. Bila kusahau, nchi ya Sudan Kusini na Afrika ya Kati nazo hujikuta katika mapigano ya hapa na pale.
Mfano mmoja kati ya mingi
Makundi hasimu nchini Sudan, Jeshi la Sudan (SAF) na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF),yameingia katika makubaliano ya kusitisha mapigano, ingawa makubaliano hayo yanasuasua. Lengo ni kuruhusu misaada ya kibinadamu kwa mamilioni ya watu waliokwama katikati ya mapigano
Nchi ya Marekani na Saudi Arabia ndizo zinasimamia makubaliano hayo. Makubaliano ya nyuma ambayo yalikiukwa mara kadhaa, nayo yalifanyika Jeddah, Saudi Arabia chini ya upatanishi wa nchi hizohizo.
Ndipo sasa, mjadala kuhusu nguvu ya Afrika na taasisi zake kuu kushughulikia mivutano ya nchi wanachama linazuka; Je, mataifa ya Afrika hayana nguvu za kutosha kushawishiana wao kwa wao? Ama kunakosekana kuaminiana kati yao?
Awali, Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za pembezoni mwa Afrika (IGAD), kupitia marais wa Kenya, Sudan Kusini na Djibouti, zilionekana mstari wa mbele kusaka suluhu, hata hivyo mbio hizo ghafla zikafifia na habari ikawa ni Jeddah.
Kwa hakika kila mmoja anatamani mapigano yanayoendelea Sudan na kwingine Afrika, yafikie tamati; yumkini wapo wasiojali kamwe ni nani atafanikisha hilo. Ila ikiwa suluhu zitaendelea kujadiliwa nje ya bara, na mjadala kuhusu nguvu za Afrika panapohusika migogoro ya wanachama wake hautaondoka.
Ni adimu kukuta mivutano inayoendelea katika nchi yoyote ya bara Ulaya, yanatafutiwa suluhu katika kuta za Ikulu moja wapo ya Afrika. Sio dhambi kusema, ifike muda iwe adimu pia kwa mivutano ya ndani ya Afrika kwenda kujadiliwa nje ya Afrika.
Masuluhisho ya Kiafrika kwa migogoro ya Kiafrika
Kauli ya marehemu, mwanauchumi George Ayittey, kutoka Ghana, ‘masuluhisho ya Kiafrika kwa matatizo ya Kiafrika,’ imejizolea umaarufu mkubwa katika majukwaa ya kisiasa, vyombo vya habari na taasisi za kielimu barani humu.
Hoja ya Ayittey ni kuwa, ikiwa utatengeneza suluhisho lako mwenyewe kwa tatizo lako, utakuwa na kila sababu na motisha kuona suluhisho hilo linafanya kazi. Masuluhisho ya muda mrefu kwa matatizo ya Afrika yatatoka tu kwa Waafrika wenyewe.
Ni ukweli usiopingika - Afrika ina maarifa ya kuzieleza changamoto zake na kuzipatia suluhu kwa kuzingatia maono na mazingira ya Kiafrika. Hilo haliwezi kushindikana ikiwa shauku ya kufanya hivyo ipo miongoni mwa viongozi wake.
Taasisi kuu ya Afrika inaendelea kufanya juhudi zake, ingawa na changamoto bado zingalipo. Miaka 60 ya Umoja wa Afrika, ni wakati wa kuyatazama mafanikio na kuzikabili changamoto na namna ya kuzipatia ufumbuzi – bila kusubiri huruma ya mataifa mengine.