Kura ya maoni CAR: Hofu ya ukandamizaji wa haki za binadamu yaibuliwa

CAR

Chanzo cha picha, Getty Images

Ni siku ya mwisho ya kampeni katika Jamhuri ya Afrika ya Kati huku wananchi wakijiandaa kushiriki katika zoezi la kupiga kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba siku Jumapili.

Rais Faustin Archange Touadera anatumai kupata kura za kutosha kwa rasimu ya katiba mpya ambayo ‘‘itaakisi kwa usahihi matarajio’’ ya watu wa Afrika ya Kati. Amekuwa kwenye kampeni akijaribu kuwashawishi watu kuunga mkono mabadiliko hayo.

''Kura ya kura ya maoni inakupa fursa ya kuamua kuhusu mustakabali bora wa nchi. Kwa hivyo usikubali kupitwa na fursa hii ya kuunda jamhuri mpya kupitia katiba,’’ Alisema.

Kura ya ndiyo itaondoa kikomo cha urais wa mihula miwili na kurumhusu Rais Touadera, aliyechaguliwa mwaka wa 2016 na 2020, kuwania muhula wa tatu mwaka wa 2025. Muhula mpya wa Urais utadumu kwa miaka saba badala ya mitano.

Rasimu ya katiba pia inakusudia kuwapiga marufuku wanasiasa wenye uraia wa nchi mbili kugombea urais, hadi waachane na utaifa wa pili. Afisi ya makamu wa rais pia itaundwa na seneti kuondolewa, ili kubadilisha bunge kuwa chumba kimoja.

Kwanini Upinzani unapinga Kura ya Maoni?

tt

Chanzo cha picha, Getty Images

Kura hiyo ya maoni iliyopangwa imesababisha maandamano huku upinzani ukiitaja kuwa ni kinyume cha sheria na kuwataka wafuasi wake kususia mchakato huo.

Katika maandamano Mahamat Kamoun, mjumbe wa Bloc Républicain pour la Défense de la Constitution (BRDC) alisema ''hawawezi kumruhusu mtu aliyeingia madarakani kupitia mchakato wa kidemokrasia kusalia madarakani maisha yake yote.''

Mwanaharakati Lydia Izedio, ambaye anafanya kazi na Muungano wa Upyaji upya wa Afrika ya Kati, anaamini kuwa marufuku iliyopendekezwa kwa raia wa nchi mbili sio haki.

‘’Wakazi wote wa Afrika ya Kati ni Waafrika wa Kati. Lakini leo, Rais wa Jamhuri amesema kuwa watu ambao asili yao sio CAR hawana haki ya kushiriki katika uchaguzi na kadhalika. Je, watoto wetu, ambao wana uraia pacha watafanyaje?’’

Waziri Mkuu wa zamani na mbunge wa upinzani Ziguele Martin aliambia BBC kuwa kura hiyo ya maoni ni ''mapinduzi ya kikatiba.''

''Kwa kuwa mahakama ya kikatiba ilitoa uamuzi dhidi ya mabadiliko ya katiba mwaka jana, hatuwezi kumuunga mkono mtu kutekeleza uharamu huu unaoitwa kura ya maoni. Ndiyo maana tunawaomba watu wa CAR wasusie zoezi hilo.’’

Hofu ya mashirika ya kutetea Haki za Binadamu ni ipi?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kuna hofu ya kutokea vurugu kwa sababu kampeni ya kura hiyo imezidisha mgawanyiko katika nchi hiyo ambayo bado inakabiliana na athari za vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya makundi mbalimbali yenye silaha yanayochochea migogoro na kudhibiti mikoa tofauti ya nchi.

Human Rights Watch imeshutumu mamlaka kwa kukandamiza mashirika ya kiraia, vyombo vya habari na vyama vya upinzani vya kisiasa.

Enrica Picco, Mwanasheria wa Kimataifa na Mtafiti katika kundi la Crisis, aliambia BBC kwamba hali ya haki za binadamu tayari ni ‘’mbaya sana’’ na kura ya ndiyo inaweza kuzidisha hali hiyo.

‘’Wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati wanahofia ikiwa hawajitokeza kushiriki katika zoezi hilo Julai 30 huenda watashinikizwa kuunga mkono rasimu ya katiba,” alisema.

''Mtafaruku wa kimabavu wa nchi kimsingi unawekwa wazi zaidi na katiba mpya na matokeo yake yanaweza kuwa ukandamizaji wa uhuru wa kujumuika pamoja na kujieleza kwa watu wa CAR.

Mamluki wa Wagner wanafanya nini CAR?

Ushawishi wa kampuni ya kibinafsi ya kijeshi ya Urusi Wagner inafuatia kampeni ya miaka mitano pamoja na uwepo wa vyombo vya habari vilivyosimamiwa kwa uangalifu.

Wapiganaji wa Wagner wametumwa katika nchi kadhaa za Kiafrika ili kupata pesa na kama sehemu ya juhudi za Urusi kuimarisha uwezo wake katika bara hilo.

Mnamo 2018 walituma "wakufunzi wa kijeshi" CAR na Sudan - kisha wakahamia Libya mwaka mmoja baadaye. Inaaminika kuwa nchi hizi zina maliasili ambayo inavutia kikundi hilo. CAR ina utajiri wa almasi, dhahabu, mafuta na madini ya uranium.

Wapiganaji wa Wagner wameendelea kutetea utawala wa Rais Faustin-Archange Touadéra dhidi ya mashambulizi kadhaa ya waasi kwenye mji mkuu, Bangui. Pia wanatumika kama walinzi wake.

Katika kipindi hicho, ushawishi wa mkoloni wa zamani wa CAR Ufaransa ulipungua, na kusababisha kusitishwa kwa uungaji mkono na ushirikiano wa kijeshi mnamo 2021.

Shirika la habari la AFP lilinukuu vyanzo vilivyotaja kujiondoa huko kama jibu la ''kushirikishwa kwa CAR katika madai ya juhudi za upotoshaji za Urusi nchini. .''

Picha zinazoonyesha mamluki wa Wagner wakipokea tuzo kutoka kwa maafisa wa serikali nchini CAR na wakifanya kazi kama usalama katika hafla za kisiasa zimesambazwa sana.

''Kufanya kazi na Wagner ni ukiukaji wa mikataba ya kimataifa. Hao mamluki wanaiba rasilimali zetu kama vile almasi na mbao. Pia wanaingilia maamuzi ya kisiasa ya nchi yetu,’’ Mbunge Martin aliambia BBC.

Na kwa hofu ya kutokea vurugu siku ya kura ya maoni, serikali inategemea kundi hilo kulinda usalama.

Enrica anaamini ushawishi wa Urusi ni mkubwa sana nchini CAR.

''Hii ni ishara kwamba makubaliano kati ya serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na Urusi bado yangalipo na pia ni ishara kwamba kwa sasa, CAR haiwezi kushughulikia masuala ya usalama pekee.