Wagner Group: Kwanini EU ina wasiwasi kufuatia kuwepo mamluki wa Urusi Afrika ya Kati?

Central Africa Republic's armed forces parade to celebrate the 61st anniversary of independence at Camp Kasai in Bangui on August 13, 2021

Chanzo cha picha, AFP

Wiki hii Muungano wa Ulaya, EU uliliwekea vikwazo Kundi la Wagner, ambao ni muungano wa mamluki wa Urusi wanaolaumiwa kwa ukiukaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR.

Muungano wa Ulaya sasa unasema huwezi tena kuwapa mafunzo wanajeshi wa serikali ya CAR kwa sababu ya uhusiano wao na kundi la Wagner.

Barani Afrika wapiganaji wake pia wako nchini Libya, Sudan na Musumbiji na wanaonekana kuwa na wajibu nchini Mali.

Kwa nini Kundi la Wagner lipo CAR?

Mamluki hao wapo CAR kumsaidia Rais Faustin-Archange Touadéra kuwapiga vita waasi, ambao bado wanadhibiti sehemu nyingi za nchi licha ya mafanikio ya hivi majuzi ya serikali.

Nchi hiyo imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu Rais François Bozizé alipopinduliwa mwaka 2013.

Bw Touadéra, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 2016, amekuwa na wakati mgumu kuwashinda waasi licha ya uwepo wa wanajeshi wa Ufaransa na vikosi vya Umoja wa Mataifa.

Serikali ya CAR inaamini kuwa mamluki wa Urusi wamekuwa na mafanikio makubwa.

Kundi la Wagner linaamiwa kuanza shughuli zake nchini CAR mwaka 2017, baada ya baraza la Ulinzi la Umoja wa Mataifa kuidhinisha huduma za utoaji mafunzo za Urusi nchini humo na kuondoa vikwazo vya silaha vilivyotangazwa mwaka 2013.

Oktoba 2017, Rais Touadéra alisafiri kwenda Urusi kusaini makubaliano kadhaa ya usalama na serikali ya Urusi.

Hii ilijumuisha ombi la msaada wa kijeshi, kwa ahadi ya kupata migodi ya madini ya almasi, dhahabu na urani nchini CAR.

Umoja wa Mataifa ulikuwa umekubaliana kutumwa watoa mafunzo 175 wa Urusi kwa jeshi la CAR.

Faustin Archange Touadera (L), President of the Central African Republic, and Russia's President Vladimir Putin

Chanzo cha picha, Getty Images

Licha ya Urusi kukana, kuna shutuma zikiwemo kutoka Muungano wa Ulaya kuwa kuna ushirika kati ya Wagner na serikali ya Urusi.

Wachambuzi wanasema uhusiano huu ulisabisha kundi la Wagner kuanza kufanya kazi nchini CAR baada ya makubaliano na Urusi kusainiwa.

Tangu wakati huo uwepo wa kundi hili katika taifa hilo lenye utajiri wa madini umeongezeka.

Urusi inasema kuwa imetuma watoa mafuzno wasio na silaha nchini CAR na zaidi ya 550 hawajakuwepo nchini humo kwa wakati mmoja.

Hata hivyo wataalamu wa umoja wa Mataifa wanaamini kuwa huenda kuna watoa mafunzo zaidi ya 2,000 waliotumwa na Urusi nchini CAR, wakiwemo wengine kutoka Syria na Libya ambapo Kundi la Wagner limekuwa likihudumu.

Hili linazua wasi wasi kwa UN na Ufaransa ambao wote wanalilaumu kundi hilo kwa kuchochea mzozo na kwa kutekeleza ukiukaji wa haki za binadamu na mauaji ya kiholela kwa wale wanaokisiwa kuwa waasi.

Ni kipi haswa Kundi la Wagner linalaumiwa kufanya?

Kundi la Wagner na vikosi vya serikali, vimebaka na kuwaibia raia maeneo ya vijijini, kwa mujibu wa UN na Ufaransa.

Kwenye ripoti ya mwezi Agosti kuhusu haki za binadamu nchini CAR, Umoja wa Mataifa ulirekodi zaidi ya visa 500 kuanzia Julai 2020. Kati ya hizo yalikuwepo mauaji ya kiholela, mateso na ukatili wa kingono.

A statue of soldiers

Mwezi Oktoba, jopo la wataalamu wa Umoja wa Mataifa lilisema wale waliokamatwa na watoa mafunzo wa Urusi na pia jeshi la Serikali mara nyingi hawakupata haki.

Mapema mwezi huu, waziri wa masuala ya sheria nchini CAR Arnaud Abazene alikiri kwa mara ya kwanza kuwa ukatili uliendeshwa na watoa mafunzo wa Urusi.

Huku akisema kuwa visa vingine vilitekelezwa na waasi, ilikuwa ndio mara ya kwanza serikali ilikiri kuwa ukatili ilifanywa na wanajeshi wake au washirika.

Ni kwa nini EU imeamua kuchukua hatua?

Msemaji wa EU Nabila Massrali aliiambia BBC kuwa muungano huo una wasi wasi kutokana na vitendo vya kundi la Wagner. Sawa na shutuma nchini CAR, Umoja wa Mataifa umelaumu kundi la Wagner kwa kuendesha uhalifu wa kivita nchini Libya.

Uchunguzi wa BBC ulifichua kuwa watu kutoka Kundi la Wagner waliwaua raia na wafungwa nchini Libya na kutega milipuko.

EU kwa sasa imefuta shughuli zake za utoaji mafunzo nchini CAR kufuatia wasi wasi kuwa mamluki hao walikuwa wakiongoza vikosi vilivyopewa mafunzo na EU.

EU ni mmoja wa wafadhili wakubwa wa misaada ya kibinadamu kwa CAR baada ya kutoa zaidi ya dola bilioni 1.6 tangu mwaka 2014.

Uhusiano wa Kundi la Wagner na serikali ya Urusi ni wa aina gani?

Hamna ushirika rasmi lakini kuna tuhuma kuwa kuna uhusiano wa karibu.

Kati ya wake waliowekewa vikwazo na EU ni Valery Zakharov, mwanachama wa zamani wa idara ya usalama ya seriakli nchini Urusi, na mshauri wa masuala ya ulinzi kwa rais Touadéra.

Kulingana na EU Bw Zakharov ni muhusika mkuu kwenye kundi la Wagner na amedumisha uhusiano wa karibu na serikali ya Urusi.

Wagner lilipata umaarufu mwaka 2014 wakati lilikuwa likipigana na waasi waliokuwa wakiungwa mkono na Urusi kwenye mzozo mashariki mwa Ukraine. Tangu wakati huo kundi hilo limeendesha shughuli zake mashariki ya kati sawia na Afrika ya kati na pia kusini mwa Afrika.

Linaaminiwa kufadhiliwa na Yevgeny Prigozhin, mfanyabiashara tajiri aliye na uhusiano na Rais Vladimir Putin. Bw Prigozhi amekanusha kila mara uhusiano wake na Kundi la Wagner.

Ni wapi tena Wagner linaendesha shughuli zake barani Afrika?

Kando na Libya, EU pia imesema mamluki wa Wagner wanaendesha oparesheni zao nchini Sudan na Musumbiji.

Poster in Bangui showing Vladimir Putin

Nchini Sudan wanaaminiwa kuhusika kwenye utaoaji mafunzo na kuwalinda maafisa na pia migodi.

Nchini Musumbiji, Wagner imewasaidia wanajeshi kwenye vita dhidi ya wanamgambo wa kiislamu kaskazini mwa nchi.

Hivi majuzi, Mali, mshirika wa miaka mingi wa nchi za magharibu kwenye vita dhidi ya makundi ya jihadi huko Sahel, ilisema inataka kuwaajiri wanachama 1,000 wa Wagner kusaidia kutoa usalama.

Hii ilifuatia tangazo la Ufaransa kuwa itaondoa karibu nusu ya wanajeshi wake 5,000 kutoka nchi hiyo.

Waziri wa mashauri ya nchi za kigeni nchini Mali Abdoulaye Diop, anasema jitihada za jamii ya kimataifa hazijafanikiwa na hivyo nchi itachukua hatua mpya.

Kuingia kwa Wagner nchini Mali inawakumbusha waangalizi wengine jinsi kundi hilo lilianza kuhudumu nchini CAR.