Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Fahamu tofauti kati ya Eid ul-Fitr na Eid ul-Adha
Maelfu ya Waislamu kote duniani wanasherehekea siku kuu ya Eid ul Fitri leo Jumatatu na wengine walisheherekea jana Jumapili wakati ambapo kuna hali ngumu ya maisha huku bei za bidhaa tofauti zikipanda kutokana na mfumuko.
Kutamatika kwa ibada ya kufunga huadhimishwa kwa sherehe maalumu za Eid, zinazoitwa Eid Al-Fitr
Lakini je tofauti iliyopo kati ya Eid al-Fitr na Eid Al-Adha ni ipi?
Eid Al-Fitr
Eid Al-Fitr maana yake ni "sikukuu ya kumaliza mfungo" na kutumiwa kuadhimisha mwisho wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Siku hii huwa ni siku rasmi ya mapumziko katika mataifa mengi yenye waumini wengi wa Kiislamu.
Hata hivyo idadi ya siku za mapumziko huwa tofauti katika nchi mbalimbali.
Waislamu huanza sherehe hizi kwa kukusanyika kwa maombi ya kila mwaka ambayo hufanyika muda mfupi baada ya macheo.
Ni kawaida kuwaona Waislamu wakikusanyika katika misikiti na viwanja vya wazi kwa maoni ya pamoja.
Kabla ya ibada hiyo, huwa wanatoa sadaka kwa maskini (huitwa Zakat) ambayo ni moja ya nguzo kuu katika dini ya Kiislamu.
Ni kawaida kwa miji mikuu mataifa ya Kiislamu kupambwa sana na sherehe kubwa kuandaliwa, watoto kununuliwa nguo mpya na kupewa zawadi mbalimbali.
Siku hii huadhimishwa baada ya kuonekana kwa mwezi wa Shawwal.
Eid Al-Adha
Eid al-Adha ndiyo sikukuu kuu zaidi ya kidini miongoni mwa Waislamu kote duniani na pia huwa ni siku ya mapumziko mataifa mengi yenye Waislamu.
Nchini Kenya Eid al-Fitr huwa ni siku ya mapumziko lakini Eid Al-Adha awali haikuwa siku ya mapumziko lakini katika miaka ya hivi karibuni imekuwa ikiadhimishwa kama siku ya kitaifa na watu hupumzika.
Eid Al-Adha maana yake ni "sikukuu ya kutoa kafara/kuchinja" kwa Kiarabu na hutumiwa kukumbuka wakati nabii Ibrahimu alipotaka kumtoa kafara mwanawe Ishmael alivyoamriwa na Allah, lakini akapewa kondoo na Mungu amtoe kafara badala yake.
Sikukuu ya Eid Al-Adha huadhimishwa kuanzia siku ya 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhul Hijjah.
Ibada ya Hajj kwenda Mecca huanza siku mbili kabla ya Eid al-Adha na tarehe yake huthibitishwa baada ya kuoenakana kwa mwezi huo wa Dhu al-Hijjah.
Eid al-Adha ina majina mbalimbali katika mataifa ya Kiislamu:
- Eid el-Kabir nchini Nigeria na Morocco
- Tabaski nchini Senegal na Gambia.
- Kurban Bayrami nchini Uturuki
- Hari Raya Haji nchini Indonesia, Malaysia na Singapore.
- Eid è Qurbon, nchini Iran.
- Bakr-Id or Qurbani Eid, nchini India, Bangladesh, na kwa Kiurdu pia.
- Idi kubwa nchini Tanzania
Waislamu pia huvalia mavazi yao mazuri na ya kupendeza siku hii na huenda msikitini kwa maombi.
Baadhi humchinja ng'ombe, mbuzi au kondoo kukumbuka kitendo cha imani cha nabii Ibrahimu.
Hula chakula chenye nyama na huwapa jamaa, majirani na maskini nyama ya mnyama waliyemchinja.
Katika baadhi ya mataifa na miji hairuhusiwi watu kuwachinja wanyama kwao nyumbani hivyo vichinjio hutumiwa. Waislamu pia hutoa pesa za hisani kipindi hicho.
Waislamu hutumia Eid Al-Adha kusherehekea utiifu kamili wa nabii Ibrahimu kwa amri ya Mungu na kuwakumbusha wenyewe kuwa tayari kutoa kafara chochote ili kutimiza maagizo ya Mungu na kumfuata.
Nguvu ya Mwezi
Wakati mwisho wa Ramadhani umefika, Waislamu wengi karibu bilioni 2 duniani wamekuwa na wakati mzuri kusherehekea Eid Al-fitr.
Kila mwaka, kila mwezi wa kalenda ya mwandamo hutokea karibu siku 11 nyuma ukilinganisha na ilivyotokea mwaka uliopita.
Kufuata kalenda ya mwezi ni muhimu sana kwa Waislamu na ina athari kubwa juu ya jinsi watu wanavyopitia Ramadhani.
Kwa kufuata kalenda ya mwezi, kila Mwislamu hupata uzoefu wa kufunga katika misimu tofauti (na hivyo ana muda mrefu au mfupi wa kila siku wa kufunga) katika kipindi cha miaka 33 ya maisha yao.
Utata wa kuadhimisha Eid
Sikukuu ya Eid Al-Fitr huangukia siku ya kwanza ya mwezi wa kumi wa Shawwal, lakini ndani ya Uislamu kuna mjadala juu ya wakati huu hasa.
Ingawa wengine hufuata kalenda iliyowekwa ya mwezi na wengine hutumia uchunguzi wa unajimu kutangaza kuonekana kwa Mwezi mpya, Waislamu wengi huadhimisha mwezi mpya baada ya Mwezi mpevu kuonekana angani.
Hii kwa kawaida hufanywa na maafisa kutoka kwa mamlaka ya Kiislamu, badala ya watu binafsi kuangalia angani wenyewe.
Eid Mubarak
Eid Mubarak kwa Kiarabu maana yake ni "sherehe au sikukuu njema au yenye Baraka".
Ni salamu za kawaida wakati wa sikukuu za Eid.
Wakati wa Eid ul-Fitr, salamu nyingine maarufu ni
- Ciid wanaagsan - Somalia.
- Mutlu Bayramlar - Uturuki.
- Selamat Idul Fitri - Indonesia.
- Selamat Hari Raya - Malaysia, Brunei, na Singapore.
- Barka da Sallah - baadhi ya maeneo ya Nigeria.