Simba yajiandaa kisaikolojia, Yanga yatamba kuendeleza burudani

Chanzo cha picha, Simba
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Mtaani raia husema, ‘ni noma sana’ , sasa ni hivi..! Pambano la watani wa jadi nchini Tanzania kati ya Simba na Yanga lazima lipate mshindi.
Bila shaka huzuni na butwaa litawakumba mashabiki wa timu moja kati hizo mbili kongwe za Afrika Mashariki kwani timu moja itatakiwa kushiriki fainali ya Ngao ya Jamii.
Timu hizo kubwa na kongwe zinazobeba taswira ya soka la Tanzania na Afrika Mashariki, zitavaana majira ya saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam
Pambano lingine nusu fainali litawakutanisha matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC dhidi ya Coastal Union katika dimba la New Amaan Complex kule visiwani Zanzibar.
Kuelekea mchezo huo, mashabiki wa Yanga wanatamba kuwa kikosi chao kiko kwenye kiwango cha juu kikiongezewa nguvu na wachezaji mastaa wanaolijua vyema soka la Bongo, Clatous Chama (Mzambia) , Duke Abuya ( Mkenya) , Prince Dube (Zimbabwe) na Jean Baleke (Mkongomani) hivyo hivyo wanatamba kuendeleza ubabe wao kwa kuifunga Simba kama walivyofanya msimu uliopita, walipoifunga mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwemo 5-1 kwenye mchezo wa Ligi.
Kwa upande wa wanachama na mashabiki wa Simba nao wameonekana kuwa na matumaini mapya, hasa baada ya kufanya usajili mkubwa wa wachezaji kutoka Ivory Coast, Zambia, Nigeria, Guinea, Burkina Faso na sehemu mbalimbali.
Wachezaji kama Valentin Nouma Joshua Mutale, Debora Fernandes, Jean Ahoua, Augustine Okejepha, Awesu Awesu, na wengineo wameanza kuwapa kiburi mashabiki wa Simba ambao wamesema wanaweza kupata ushindi, lakini hata kama watapoteza mechi hiyo, haitokuwa kizembe kama walivyochapwa mabao 5-1 msimu uliopita.
Simba wajiandaa kisaikolojia
Si kwaajili ya kipigo kikubwa, bali Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema amewaandaa wachezaji wake kisaikolojia kwa ajili ya mechi hiyo.
"Mchezo utakuwa mzuri na mgumu, lakini nimewaandaa wachezaji wangu kisaikolojia kwenda kucheza, wakituliza akili na kufuata maelekezo, haina shaka ya kuibuka na ushindi," alisema na kusema bado kikosi chake hsakijafikia asilimia 100 ya ubora anaoutaka.
Simba inakwenda kucheza mechi hiyo ikiwa ndiyo mshindi wa Ngao ya Jamii iliyopita ilipolitwaa Agosti 23, mwaka jana, Uwanja wa Mkwakwani, ilipoichapa Yanga mabao 3-1 kwa mikwaju ya penalti.
Yanga yatamba kuendeleza burudani

Chanzo cha picha, Yanga Sports Club
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi amesema wanakwenda kucheza mchezo huo kwa lengo la kutoa burudani kwa mashabiki watakaofika uwanjani
"Natumaini wachezaji wangu watacheza soka safi, na siku zote ukiwa bora na kucheza soka zuri, ushindi unakuwa upande wako," alisema kocha huyo raia wa Argentina.
Fainali 19 za ngao ya jamii zachezwa Tanzania bara
Mpaka sasa zimechezwa fainali 19 za ngao ya jamii tangu mwaka 2001. Hata hivyo fainali hizo hazikuchezwa mwaka 2004, 2006, 2007 na 2008 tu.
Simba yaongoza rekodi
Tangu kuanza kwa kombe la Ngao ya Jamii, Simba imetwaa taji hilo mara 10, ikifuatiwa na Yanga mara saba huku Azam na Mtibwa Sugar zikitwaa mara moja moja.
Yanga ya kwanza kutwaa taji hilo
Mwaka 2001, Yanga iliichapa Simba mabao 2-1, wafungaji wakiwa ni Edibily Lunyamila na Ally Yusuph ‘Tigana’ swakati goli pekee la simba likifungwa na Steven Mapunda ‘Garincha’.
Mara ya mwisho, taji lilienda kwa Simba mwaka jana baada ya kuifunga Yanga mikwaju ya penalty 3-1 baada ya dakika tisini ya sare tasa.
SIMBA 5- YANGA 4
Timu hizo zimekutana maraa tisa kwneye kombe hilo na Simba kuifunga yanga na kutwsaa taji mara tano wakati Yanga hao wakishinda mara nne.
Imehaririwa na Lizzy Masinga












