Kwa nini waislamu hawaridhishwi na serikali ya Ahmed inayofuata mfumo wa sheria za kislamu?

    • Author, Mina Lamy
    • Nafasi, Kitengo cha BBC Monitoring
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Mwaka mmoja tangu Ahmed al-Sharaa, aliyewahi kuwa kamanda wa kundi la Kiislamu Tahrir al-Sham na kiongozi wa "Dola ya Uokozi" kaskazini-magharibi mwa Syria, achukue madaraka kufuatia kuporomoka kwa ghafla kwa utawala wa Bashar al-Assad, kumekuwa na taswira mbili zinazokinzana kuhusu uongozi wake.

Kwa upande mmoja, serikali za Magharibi ambazo kwa miaka zilimhukumu yeye na kundi lake kuwa magaidi, sasa zinamwona kama kiongozi mwenye uhalisia na mwenye uwezo wa kushirikiana.

Zimeondoa jina lake na lile la kundi lake kwenye orodha za ugaidi na zimeanza kumwalika katika miji mikuu kama Washington na Paris.

Lakini kwa upande wa waumini wa kiislamu na mitandao ya wanajihadi, hali ni tofauti.

Sehemu kubwa ya wanazuoni na wanaharakati waliomsherehekea Al Sharaa kama ishara ya ushindi wa kundi la Wasunni na "Mrengo wa Mapinduzi" sasa wanamsema kwa kuacha mradi wa Sharia, kujiunga na muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani dhidi ya ISIS, na kuvuka mistari nyekundu ya zamani kuhusu mahusiano na nchi za Magharibi na jamii za wachache.

Kwao, mwenendo wa mwaka mmoja uliopita hauonekani kama mkakati wa hatua kwa hatua, bali kama uthibitisho kwamba Al Sharaa amekuwa akielekea upande wa Magharibi kwa muda mrefu na sasa mwelekeo huo umefikia upeo wake.

Hata hivyo, duru za Kiislamu zilizo karibu na serikali zinasisitiza kuwa mazingira ya Syria ni dhaifu mno kulazimisha Sharia kutekelezwa mara moja, zikisisitiza dhana ya "kuoanisha uhalisia na malengo."

Kwa mtazamo wao, kukata mahusiano ya nje na kuanzisha mfumo wa sheria za kiislamu papo hapo kungedhoofisha utawala na msimamo wa Wasunni katika ushindani na nguvu nyingine za kikanda.

Mvutano huu ndiyo umekuwa kitovu cha mjadala miongoni mwa waumini wa kislamu wa Syria na mitandao ya wanajihadi nje ya nchi katika mwaka wa kwanza wa utawala wa Sharia.

Kutoka kamanda hadi Rais: taswira mbili tofauti

Kwa Waislamu wengi, mjadala kuhusu Al Sharaa hauanzii kwa safari zake za kimataifa bali katika historia yake ya mapambano.

Kwa miaka mingi, alijulikana kama kamanda aliyekuwa akijaribu kuonyesha mfano wa utawala wa Kiislamu katika maeneo yaliyodhibitiwa na kundi lake.

Baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad mnamo Desemba 2024, swali kuu likawa ni namna uzoefu wake huo ungeathiri usanifu mpya wa madaraka nchini Syria.

Katika miezi ya mwanzo, Waislamu wengi walichukua msimamo wa kusubiri na kuona.

Kwa baadhi yao, kuingia kwake Ikulu ya Damascus kulikuwa tukio la kihistoria: kwa mara ya kwanza baada ya miongo mingi, rais Msunni aliyeibuka kutoka upinzani alikuwa amechukua madaraka.

Lakini wakati huohuo, walifuatilia kwa makini kama Al Sharaa angeendeleza lugha na fikra alizokuwa nazo akiwa ndani ya kundi la Tahrir al-Sham, au kama angebadilika na kuanza kuzungumza kama kiongozi wa dola ya kawaida.

unaweza pia kusoma:

Kadiri miezi ilivyopita, mgawanyiko ukaongezeka.

Kundi lililokuwa karibu na serikali lilisisitiza kuwa Al Sharaa yuko katika kipindi cha mpito na anajaribu kuzuia Syria kuangukia katika kutengwa kimataifa kama Taliban.

Kwao, mabadiliko yake hayakuwa usaliti wa mfumo wa sheria za kiislamu, bali jitihada za kuepusha nchi kuingia katika mgogoro mkubwa zaidi.

Upande mwingine, wenye ushawishi miongoni mwa wafuasi wa harakati za Kiislamu, waliona kila hatua ya Sharia kuelekea "utawala wa kawaida" kama uthibitisho wa kujitenga kwake na mradi wa awali alioupigania.

Waliona anguko la Assad kama nafasi adimu ya kujenga dola inayotawaliwa na mfumo wa sheria ya kiislamu kikamilifu nafasi ambayo, kwao, Al Sharaa ameipoteza kwa kujificha nyuma ya maneno ya "uhalisia wa kisiasa."

Matokeo yake ni sura mbili tofauti.

kwa upande mmoja, Al Sharaa anaonekana kama kiongozi anayejiondoa katika fikra kali za kijihadi na kuelekea Uislamu wa kiserikali wenye uhalisia; upande mwingine, anaonekana kama mtu aliyefanya "ujivue-itikadi," kiasi kwamba kazi yake kama rais imejitenga kabisa na historia yake kama kamanda wa Kiislamu.

Mgeuko wa magharibi na muungano dhidi ya ISIS

Kiini cha tuhuma za wanaitikadi kali wa kiislamu ni dai kwamba Al Sharaa ameigeukia Magharibi.

Wanaunganisha taarifa mbalimbali za kiusalama na kauli za maafisa wa Magharibi kudai kwamba Al Sharaa alianza kushirikiana na vyombo vya usalama vya Uturuki, Marekani na Uingereza hata kabla ya anguko la Assad ikiwamo kubadilishana taarifa kuhusu mitandao ya al-Qaeda na ISIS.

Ripoti za kuondolewa kwake kwenye orodha ya magaidi baada ya kuwa rais ziliweka mafuta katika moto wa tuhuma hizi.

Kujiunga kwa Syria na muungano wa kupambana na ISIS mnamo Novemba 2025 ndiko kulitibua hali zaidi.

Wapiganaji wengi wa Tahrir al-Sham walikuwa wamepigana na ISIS kwa miaka, lakini sasa wanalazimika kufanya kazi chini ya mwavuli wa muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya kundi ambalo baadhi ya wanazuoni wakali, japokuwa hulikosoa vikali, bado huliona kuwa "Waislamu waliokosea."

Kwao, kushirikiana na "makafiri" yaani watu wasiofata sheria za kiislamu kupigana na Waislamu ni kosa linalokaribia ukafiri.

Serikali, kwa upande wake, inatoa hoja za kiusalama na kisiasa.

Waziri wa Sheria Mazhar Weiss anasema ushiriki huo ni wa kijasusi zaidi na unalipa Syria nafasi ya kuwa na usemi katika masuala ya kimataifa.

Abdullah Muhaisni, mmoja wa wanazuoni wenye ushawishi, anasema kutoshiriki kungesababisha mahasimu kama SDF kutawala uwanja.

Lakini hoja hizi hazijawashawishi wakosoaji, na ISIS imezidisha propaganda ikitumia mvutano huo kujijenga upya.

Mjadala wa utekelezaji wa sharia, nafasi ya Mujahidin, na sera kwa Israel

Kutopitishwa kwa mfumo wa kisheria wa kiislamu yaani Sharia kama sheria kuu mara moja na kupitishwa kwa katiba ya mpito kumekuwa eneo jingine la mvutano.

Katiba ya Machi 2025 ilitaja Uislamu kuwa chanzo kikuu cha sheria, lakini haikukifanya kuwa chanzo pekee.

Wanazuoni kama Hani al-Seba'i waliona hili kuwa "kukataa utawala wa Sharia."

Fatwa zinazohusishwa na Abu Muhammad al-Maqdisi zinamwita Sharia "murtadi," na kushiriki katika uchaguzi kuwa kukubali sheria zisizo za Kiislamu.

Kwa upande wa serikali, wanazuoni wake wanasisitiza kuwa hali ya Syria hairuhusu hatua za ghafla: kuanzisha Sharia kikamilifu sasa kungesababisha vikwazo, kutengwa, au hata mashambulizi kutoka nje.

Mazungumzo haya yanahusiana pia na suala la "mujahidin."

Wakosoaji wanasema waliopigana kwa miaka dhidi ya Assad hawakupewa nafasi ya kutosha, na kwamba mamlaka imejikita mikononi mwa kundi dogo la makamanda wa karibu na Sharia.

Ingawa kwa uhalisia viongozi wengi wa Tahrir al-Sham wamepata nyadhifa rasmi, madai ya "kusaliti mujahidin" yanaendelea.

Kauli juu ya Israel zimezua ukosoaji zaidi.

Wakosoaji wanasema serikali haijaitikia ipasavyo mashambulizi ya angani ya Israel ndani ya Syria.

Huku kukiwa na madai kwamba Marekani inaisukuma Damascus kuelekea "kurekebisha uhusiano" na Israel, shaka miongoni mwa Waislamu imeongezeka.

Makundi ya wachache, wapiganaji wa kigeni, na wafungwa

Sera za serikali kuhusu wachache wa kidini na kikabila, wapiganaji wa kigeni, na wafungwa wa Kiislamu zimeongeza mvutano.

Wahafidhina wanasema kuwa Wasunni waliobeba mzigo mkubwa wa vita hawajapewa nafasi wanayostahili, na kwamba serikali inatoa upendeleo kwa Alawite, Druze na Wakurdi ili kujipatia uungwaji mkono wa kimataifa.

Kwa Druze na Wakurdi, tuhuma zinachochewa pia na hofu ya madai ya kujitenga.

Mapigano ya hivi karibuni katika pwani na Sweida yametumiwa na Waislamisti kuhimiza jamii za Kisunni kutokukabidhi silaha zao, kinyume na maagizo ya serikali.

Wapiganaji wa kigeni kuanzia Uyghur wa Turkestan Mashariki hadi Waarabu na Wazungu waliopigana sambamba na Tahrir al-Sham wana hofu ya kukabidhiwa nchi zao kama sehemu ya makubaliano ya kisiasa.

Kauli ya Sharia mjini Paris kuhusu uwezekano wa kuwapa uraia wale "waliopigana zamani bila matatizo" imeongeza mashaka.

Kwa wafungwa wa Kiislamu, serikali imekataa wito wa kuachiliwa kwao, ikisema watasababisha wimbi jipya la misimamo mikali.

Wakosoaji wanadai Sharia amekuwa mkali zaidi kwa washirika wa zamani kuliko kwa maadui wa nje.

Kampeni za Mtandaoni na Hisabati za Kisiasa

Ingawa kelele za ukosoaji ni kubwa, hakuna muungano wa kijeshi uliojitokeza kupambana na serikali ya sasa ya Al Sharaa.

Hali hii inatokana na udhaifu wa miundo ya kijihadi baada ya vita vya miaka mingi, pamoja na ukosefu wa mbadala wa kuaminika wa Kisunni.

Aidha, hesabu za kisiasa kuhusu mustakabali wa Wasunni nchini Syria zinazidi kuwa ngumu.

Kwa wengi wao, licha ya mapungufu ya serikali ya Sharia, bado anaonekana kuwa chaguo pekee linaloweza kudumisha nafasi fulani ya utawala wa Wasunni Damascus.

Kuanguka kwake, bila mbadala thabiti, kunaweza kuibua uingiliaji wa nje na kuimarisha makundi pinzani.

Kwa wakati huu, ISIS inajaribu kutumia mgawanyiko uliopo na kujionyesha kama mshindani "aliethibitika," ingawa chuki ya Waislamu wengi dhidi ya mbinu zake imedhoofisha uwezo wake wa kupata uungwaji mkono.

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid