Fainali WAFCON 2024: Morocco kuandika historia, au Nigeria kuendeleza ubabe?

Chanzo cha picha, Getty Images/Backpage Pix
Nigeria inawania taji la 10 la Afrika ili kuongeza rekodi itakapomenyana na wenyeji Morocco katika fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2024 siku ya Jumamosi ya Julai 26, 2025.
Timu zote mbili hazijafungwa huku wenyeji miamba ya Afrika Magharibi, Nigeria imeruhusu bao moja pekee katika mechi tano kuelekea fainali katika uwanja wa Olimpiki wenye uwezo wa kuchukua watu 21,000 huko Rabat.
Washindi wa pili katika uwanja huo huo katika fainali za mwaka 2022, Morocco wanatafuta kutwaa kombe lao la kwanza kabisa.
Iwapo Morroco (Atlas Lionesses au Simba jike wa Atlas) itanyanyua kombe hilo kwa mara ya kwanza itatoa faida fulani kwa uwekezaji mkubwa ambao ufalme huo umeutumia katika mchezo wa wanawake katika miaka ya hivi karibuni.
Kubashiri timu inayoweza kushinda fainali na kutwaa kombe sio rahisi.
Morocco kutoka Afrika Kaskazini, wanaonolewa na Kocha Mhispania aliyetwaa Kombe la dunia la Wanawake akiwa na Hispania mwaka 2023, Jorge Vilda dimbani, walihitaji mikwaju ya penalti kuwatoa Ghana, huku Nigeria, timu inayoshika nafasi ya juu katika ubora Afrika kwa soka la wanawake, ikifunga bao muhimu na kuwatupa nje mabingwa watetezi, Afrika Kusini.
Imani, hata hivyo, iko juu katika kambi ya (Nigeria) Super Falcons, na kampeni yao iliyopewa jina la 'Mission X'.
"Mission X - ndivyo mashindano haya yote yalivyokuwa," beki Michelle Alozie aliambia BBC Sport Africa.
"Inaenda hadi fainali na kushinda. Tunakua kama timu na nadhani hiyo inajionyesha katika kila mchezo."
Bingwa atajinyakulia $1m (£743,000) kama pesa za zawadi pamoja na kombe jipya la Wafcon.
Wasikilizaji wa Idhaa ya Dunia ya BBC barani Afrika wanaweza kusikiiza matangazo ya moja kwa moja ya redio (michezo saa 20:00 GMT- sawa na saa mbili za usiku kwa saa za Afrika Mashariki), wakati mechi itatangazwa moja kwa moja kwa watazamaji nchini Uingereza kwenye iPlayer na tovuti na programu ya BBC Sport.
Simba jike wa Atlas wanahitaji ushindi mmoja kuweka historia

Chanzo cha picha, Confederation of African Football
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Morocco 'Simba jike wa Atlas' ilirejea Wafcon kwa mara ya kwanza tangu 2000 wakati nchi hiyo ilipoandaa fainali za 2022, lakini wenyeji hao ambao pia watashiriki fainali za 2026 mwezi Machi, sasa wamejiimarisha kama moja ya timu bora zaidi barani.
Hata hivyo, uchezaji wao mwezi huu haujawa wa kuridhisha kama miaka mitatu iliyopita, ikizingatiwa kuwa walitoka nyuma mara mbili dhidi ya Zambia katika mchezo wa ufunguzi na baadaye wakawafunga Ghana.
Kipa Khadija Er-Rmichi ameonekana kuyumba mara kadhaa, mchezaji nyota na nahodha mwenye umri wa miaka 34 Ghizlane Chebbak ubora wake haukuonekana katika hatua ya mtoano na winga Sanaa Mssoudy hajaonyesha ujanja na matokeo ambayo yalimfanya kutajwa kuwa mchezaji bora wa mwaka jana wa Ligi ya Mabingwa Afrika ya Wanawake.
Hata hivyo Chebbak, mfungaji bora wa katika michuano hiyo akiwa amefunga mabao manne, bado ana uwezo wa kutengeneza nafasi katika wakati muhimu pamoja na mshambuliaji Ibtissam Jraidi ambaye ni mkali wa mabao.
"Nimeona timu ya Morocco ambayo haikati tamaa hata inapokuwa mkiani," Desire Oparanozie, mshindi mara nne wa Wafcon akiwa na Nigeria, aliiambia BBC Sport Africa.
"Wamekuwa na soka la kuvutia sana. Wanaendelea kuja na jambo chanya."
Uteuzi wa Vilda ulikuwa wa kutatanisha, ikizingatiwa kwamba aliacha kazi ya kuinoa Hospania huku kukiwa na hali mbaya ya kisa cha fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake 2023 wakati rais wa shirikisho la wakati huo Luis Rubiales alipombusu mchezaji Jenni Hermoso bila ridhaa yake.
Rubiales alipatikana na hatia ya unyanyasaji wa kijinsia na kutozwa faini, huku Vilda akiondolewa mashtaka ya kulazimishwa.
Hata hivyo kuwepo kwake katika dimba la Morocco kumegawanya wafuasi - hata kama angeweza kutengeneza historia kwa kuisaidia timu ya Afrika Kaskazini kushinda Wafcon kwa mara ya kwanza huku pia akifanikiwa kushinda mara mbili ya kipekee.
"Morocco itahitaji kocha wa kuwafanya kuwa zaidi ya kuwa bora kwa baadhi ya wachezaji tu ili kushinda fainali hii," mwandishi wa habari wa Algeria Maher Mezahi aliiambia BBC World Service.
"Nimeona hata hoja za kusema kwamba Morocco inapaswa kumuajiri Vilda, ikiwa atawawezesha kushinda Wafcon, litakuwa ni jambo la thamani kwasababu itafanya mengi zaidi kwa mchezo wa wanawake hata kama hilo litaleta dosari kidogo kwa yeye kuwa kocha."
Je, Super Falcons wanaweza kukamilisha Misheni X?

Chanzo cha picha, Backpage Pix
Wakati huohuo, Nigeria, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiongoza katika soka la wanawake barani Afrika, haijaona haya kueleza nia yao ya kutwaa tena taji hilo waliloshinda mara ya mwisho mwaka 2018.
Shirikisho la soka nchini humo lilitangaza Mission X kabla ya fainali hizo na imekuwa gumzo wakati wanahabari wakizungumza na wachezaji.
Kocha Justin Madugu amepata uwiano kwenye kikosi chake ambacho kimeonyesha kuwa imara nyuma, ubabe katika safu ya kati na safu ya tatu ya mbele ikiongozwa na uchezaji mahiri wa Esther Okoronkwo.
Tishio la Super Falcons kutoka uwanjani linasisitizwa na kuwa na wafungaji tisa tofauti, na timu hiyo ilipata ushindi dhidi ya Afrika Kusini wakati beki wa kulia Alozie alipofunga na kuipa ushindi Nigeria katika hatua ambayo haikutarajiwa beki kuamua mechi.
"Tumezaliwa na ari ya kupigana na kutaka kushinda kila mchezo," mshambuliaji Okoronkwo aliambia BBC Sport Africa.
Kipa Chiamaka Nnadozie, ambaye amesajiliwa na Brighton inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake, amekua likizo langoni bila kuoigiwa michomo na mara pekee amepigiwa michomo kuelekea langoni kwake hadi sasa ni mkwaju wa penalti.
Mshambuliaji wa zamani wa Nigeria, Desire Oparanozie anafikiri Super Falcons wataingia uwanjani kwa lengo la "kulipiza kisasi" baada ya kutolewa nusu fainali na Wamorocco mnamo 2022 - mchezo ambao uliwafanya wachezaji wawili kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 72 na hatimaye kupoteza kwa mikwaju ya penalti.
Udhibiti wa mashabiki katika uwanja wa ugenini
Umati wa watu wengi unatarajiwa katika mji mkuu wa Morocco, Rabat lakini Oparanozie hatarajii kwamba uungwaji mkono mkubwa kwa wenyeji utaathiri wachezaji wa taifa lake.
"Nigeria inajulikana kwa matukio makubwa kama haya," kijana huyo mwenye umri wa miaka 31 alisema.
"Mnamo 2016 tulicheza dhidi ya wenyeji Cameroon (katika fainali). Uwanja ulijaa watu 40,000 hata hiyo haikuzuia Nigeria kushinda."
Mashindano hayo ya 2024, yaliyocheleweshwa kwa mwaka mmmoja kwa sababu ya maswala ya ratiba, yamekiwa ya kipekee ambapo timu za chini kabisa za bara hilo zimeleta upinzani mkunwa kwa timu za juu, lakini fainali hii wengi waliitabiri.
Ikiwa Morocco inaweza kuziba pengo la nafasi 24 katika viwango vya ubora duniani na kuipa Nigeria kipigo chao cha kwanza kabisa kwenye fainali hizo - itajitengenezea jina jipya kwenye mashindano hayo ya Wafcon.
Ushindi kwa wenyeji unaweza kuleta usawa wa mamlaka barani Afrika, pamoja na kuleta shinikizo kwa timu ya taifa ya wanaume ya Morocco itakayoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) , ambayo itaanza katika ufalme huo mwezi Disemba mwaka huu.













