Wafcon 2024: Jinsi michuano hiyo inavyotoa ahueni mashariki mwa DR Congo

Chanzo cha picha, Backpage Pix
- Author, Beng Emmanuel Kum & Rob Stevens
- Nafasi, BBC Sport Africa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Baada ya vurugu za DR Congo mwaka huu, kombel la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (Wafcon) 2024 limeleta maana kubwa kwa wachezaji na mashabiki wa DR Congo.
Wakirejea kwenye michuano hiyo kwa mara ya kwanza tangu 2012, Leopardesses wametoa fursa fupi kwa taifa hilo kusahau kuhusu mzozo huo mbaya ambao umekumba majimbo ya mashariki kwa miongo kadhaa.
Mashambulizi ya waasi wa M23 mwezi Januari, na kusonga mbele hadi kuchukua udhibiti wa eneo ambalo lina utajiri wa madini ya thamani na adimu.
Kuna ushahidi mkubwa kwamba Rwanda, jirani wa DR Congo, inaunga mkono M23 lakini serikali ya Kigali inakanusha kulipatia kundi hilo msaada wa kifedha au kijeshi.
Mkataba wa amani ambao DR Congo na Rwanda zilitia saini mwishoni mwa Juni umetoa matumaini kuwa eneo hilo linaweza kuanza maisha mapya.
Mwezi huu nchini Morocco, wanasoka wa Congo pia wanatafuta kuwapa wenzao kitu cha kushangilia.
"Kuona waathiriwa - watoto, mama, baba ambao wamepoteza wapendwa wao, na familia zimesambaratika – hali ilikuwa ya kusikitisha," kiungo wa kati Marlene Yav Kasaj aliambia BBC.
"Kwangu mimi, ninapokuwa uwanjani, naamini nalazimika kushinda, hata ikiwa hilo litaleta wakati mfupi wa furaha kwa watu wetu."
Makubaliano hayo ya amani, yaliyotiwa saini jijini Washington DC, Marekani yanataka "kuacha mashambulizi, kupokonywa silaha na kuunganishwa kwa makundi yenye silaha yanayopigana mashariki mwa DR Congo.
Wakati huo huo, serikali mjini Kinshasa iko katika mazungumzo na M23 kuhusu kusitisha mapigano. Lakini, katika baadhi ya mikoa iliyoathiriwa zaidi, wakazi wanaendelea kutafuta faraja.
Joseph, shabiki aliyesafiri kutazama mchezo wa kwanza wa kundi lao dhidi ya Senegal mjini Mohammedia, aliiambia BBC Sport Africa, “soka ni aina ya tumaini kwa watu wanaoishi katika eneo lenye vita."
Kutafuta ahueni

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya watu wameuawa na maelfu ya raia wamekimbia makwao kufuatia mashambulizi ya waasi. M23 inapinga takwimu hizo, ikisema ni chini ya watu 1,000 ndio wamefariki.
Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, ulikumbwa na mapigano mabaya mwanzoni mwa mwaka huu na uko chini ya udhibiti wa waasi.
Mkazi mmoja wa jiji hilo ameiambia BBC, “matukio ya kutisha tuliyoshuhudia Januari, miili ikiwa imetapakaa barabarani, athari za mapigano zinaonekana kila mahali, watu kuuawa kiholela na uvundo wa maiti zilizoharibika, zilituacha tukiwa na wasiwasi,” anasema mchangiaji huyo ambaye amechagua kutotajwa jina lake.
Pamoja na uwepo wa wapiganaji huko Goma, raia wanasema nafasi ya kushangilia timu yao huko Wafcon inatoa fursa ya kurejesha fahari na utukufu wa taifa.
Yav Kasaj, anayechezea TP Mazembe yenye maskani yake Lubumbashi, klabu kubwa nchini humo, ameathiriwa binafsi na mzozo huo. Kiungo huyo wa kati mwenye umri wa miaka 22, anasema:
"Nilipoteza rafiki; alikuwa muhanga wa vita. Tumejitolea kupigania furaha ya kila mtu wa Goma."
DR Congo yasahauliwa?

Chanzo cha picha, BBC Sport Africa
Hali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imeshuka katika ajenda ya habari za kimataifa, vita vya Ukraine na mzozo wa Israel na Gaza vinapata muda zaidi.
Kupungua huko kwa ufuatiliaji ni jambo ambalo limewapa msukumo wanasoka wa taifa hilo kutumia jukwaa lao kusukuma amani.
Vijana wa DR Congo walitoa wito wa kukomesha ghasia katika Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka jana, wakitoa ishara za umoja wakati wakiimba wimbo wao wa taifa kabla ya kushindwa katika nusu fainali dhidi ya wenyeji Ivory Coast.
Leopardesses wamepoteza mechi zao mbili za mwanzo dhidi ya Senegal na wenyeji Morocco, na kuruhusu mabao manne katika mechi zote mbili, lakini mshambuliaji Olga Massombo anasema timu hiyo bado ina ari ya kucheza.
"Wazazi wetu, dada zetu huko nyumbani wako vitani, wanaume na wanawake huko bado wanapigana," anasema.
"Kuja kwetu hapa ni heshima. Ni wazi kupoteza mechi hizi tunaweza kuwa tumewaangusha, lakini lengo ni kusonga mbele.
"Ninapozungumzia maendeleo, sio tu kuhusu sisi kama timu lakini [kwa] nchi nzima.
Maumivu ya kupoteza

Chanzo cha picha, Getty Images
Celia, shabiki mwingine aliyekwenda Morocco, anaamini wachezaji wameshindwa kupambana na matatizo mengi ya nyumbani na ya maandalizi ya Wafcon.
"Wameweka juhudi zao zote kwenye mchezo, lakini hawajaweza kushinda," alisema baada ya kushindwa 4-2 na Morocco mjini Rabat.
Mwezi Desemba, timu ya wanaume itafunga safari ya kuelekea Morocco kushiriki Kombe la Mataifa ya 2025.
Joseph anasema: "Kama nchi tunaunga mkono kwa nguvu zetu zote timu zetu za taifa, wanawake na wanaume.”
"Kwa makubaliano ya hivi majuzi ambayo yametiwa saini huko Marekani, kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo tunatumai kuwa mambo yatakuwa bora na tunaweza kuona usitishaji mapigano na kufungua njia ya kibinadamu kwa watu wanaoteseka."
DR Congo lazima washinde mechi yao ya mwisho ya Kundi A dhidi ya Zambia - ili kupata nafasi yoyote ya kutinga robo fainali kama moja ya timu zilizo katika nafasi ya tatu bora.
Yav Kasaj anasema, hali halisi ni kwamba watu wanakufa, na tuko katika matatizo kila wakati."











